Thursday, 28 August 2014

TAMBUA AINA TOFAUTI ZA UVIMBE KWENYE KIZAZI CHA MWANAMKE-3



Wiki zilizopita nilijadili kuhusu Fibroids, Ovarian cysts yaani uvimbe kwenye vifuko vya mayai ya uzazi na tatizo la mwanamke kuwa na vijivimbe vingi vidogo vidogo kwenye vifuko vya mayai ya uzazi, tatizo ambalo kitaalamu hujulikana kama Polycystic Ovarian Syndrome ( PCOS). Leo nitamalizia somo hili.
Leo ninamalizia somo letu ambalo linahusu kutambua aina mbalimbali za uvimbe kwenye kizazi cha mwanamke.
Salpingitis
Hili ni tatizo la kuvimba kwa kuta za mirija ya uzazi. Hutokea kutokana na vyanzo vingi mfano maambukizi ya magonjwa ya zinaa ambayo pamoja na mambo mengine huchangia katika tatizo ili na husababisha mirija ya uzazi kuziba na hivyo mwanamke hujikuta katika matatizo ya kutafuta ujauzito kwa muda mrefu bila mafanikio.
Dalili za tatizo hili ni kutokwa na majimaji machafu ukeni, maumivu ya kiuno na tumbo hasa chini ya kitovu kushoto na kulia, uchovu wa mara kwa mara bila hata kufanya kazi nzito, maumivu wakati wa kushiriki tendo la ndoa, nk.
Ovaritis
Hii ni tofauti na Ovarian cyst. Hii siyo kuwa na uvimbe kwenye vifuko vya mayai ya uzazi bali ni kuvimba kwa kifuko chote cha mayai ya uzazi.
Pia matatizo ya hedhi kama hedhi kukoma zaidi ya miezi mitatu au kutoka bila ukomo au kutokuwa na mpangilio maalum pia huhusishwa na tatizo hili.
Madhara ya uvimbe wa aina mbalimbali kwenye kizazi cha mwanamke kwa ufupi,
kukosa hamu ya kushiriki tendo la ndoa kutokana na maumivu anayoyapata wakati wa tendo au baada.
Kupoteza uwezo wa kushika ujauzito kwa zaidi ya miezi sita au zaidi ama kupoteza uwezo wa kutunza mimba hadi ifikie wakati wa kujifungua, kwa maana kwamba aina fulani za uvimbe kama Fibrids huchangia kwa kiasi kikubwa mimba kuharibika.
Ushauri/Hitimisho
Mwanamke anapohisi maumivu chini ya kitovu, wakati wa tendo la ndoa, wakati wa kutoa haja ndogo, hedhi kupishana na ikiambatana na matatizo ya kiuno na utokwaji wa uchafu asipuuze hata kidogo bali atafute vipimo na tiba hadi dalili hizi zipotee mwilini mwake.


0 comments:

Post a Comment