Thursday, 28 August 2014

TAMBUA AINA TOFAUTI ZA UVIMBE KWENYE KIZAZI CHA MWANAMKE-2



WIKI iliyopita nilianza kujadili mada inayohusu aina tofauti za uvimbe kwenye kizazi cha mwanamke. Nilianza na aina ya kwanza kuwa ni fibroid (s ), yaani uvimbe kwenye mji wa mimba. Nilieleza dalili zake ni hedhi nzito kupita kiasi, utokwaji wa uchafu ukeni, mimba kuharibika, maumivu chini ya kitovu kwa katikati, kuongezeka kwa tumbo kadiri uvimbe huu unavyoongezeka, n.k.
Chanzo cha moja kwa moja cha tatizo hili hakijawa wazi na tafiti za kitabibu bado zinaendelea, japo kwa matokeo ya tafiti zilizokwisha fanyika zinaonesha kuwa ni tatizo la kurithi. Kama kuna mwanamke katika ukoo ambaye aliwahi kuwa na Fibroids basi kuna uwezekano wa wengine kukumbwa na tatizo hili.
Chanzo kingine ni kuwa na ongezeko kubwa la homoni ya Estrogen ambayo huchochea ukuwaji wa uvimbe huu na kuufanya kuwa mkubwa mithili ya tikitimaji.
Madhara ya aina hii ya uvimbe ni kumfanya mgonjwa kupoteza uwezo wake wa kushika ujauzito au kusababisha kuharibika kwa mimba muda wowote inapofikisha miezi zaidi ya miwili.
Mwanamke ambaye amekuwa na tatizo la mimba kuharibika mara kwa mara au kukosa ujauzito kabisa kwa zaidi ya mwaka mmoja wakati hatumii kinga yoyote kuna uwezekano akawa ana uvimbe wa aina hii kwenye mji wa mimba au fuko la uzazi hasa hasa kama ina ambatana na maumivu wakati wa tendo la ndoa, hivyo anatakiwa kutafuta tiba mapema bila kudharau ili kulinda afya yake ya uzazi.
Ovarian Cyst
Hii ni aina ya pili ya uvimbe kwenye kizazi cha mwanamke. Hutokea kwenye vifuko vya mayai ya uzazi, kwa ndani au kwa nje, na yaweza ikawa kwenye kifuko kimoja cha mayai au vyote viwili.
Dalili kubwa ya uvimbe wa aina hii ni kichomi chini ya kitovu na sehemu moja.
Kichomi huzidi sana mgonjwa anapocheka kwa nguvu au kuinama au anapobeba vitu vizito.
Dalili nyingine kubwa ni kuwa na tatizo la hedhi inayokoma kwa zaidi ya miezi mitatu, tatizo ambalo kitaalamu huitwa Amenorrhea,
maumivu wakati wa kutoa haja ndogo na kutoa haja ndogo mara kwa mara, maumivu ya kiuno kwa nyuma, maumivu wakati wa kujamiiana, maumivu makali wakati wa hedhi, kupoteza hamu ya kula, kuongezeka uzito na unene kwa kiasi.
Mwanamke anapoona dalili zaidi ya moja kati ya hizi awahi kwenda hospitali. 

0 comments:

Post a Comment