TATIZO hili pia kitaalamu linaitwa ‘Vaginal Atrophy’ au ‘Urogenital Atrophy’. Ni matatizo yanayotokea ukeni na kusambaa sehemu ya nje na kushambulia hadi maeneo ya njia ya mkojo.
Katika hali hii sehemu za siri za mwanamke hadi ndani ukeni husinyaa na huwa kavu na hata yale majimaji ya ukeni hukauka. Tatizo hili pia huchangiwa na upungufu au ukosefu wa vichocheo vya ‘Estrogen’.
Upungufu wa homoni au vichocheo hivi hutokea kutokana na jinsi mwili unavyofanya kazi na wakati mwingine huwatokea zaidi wanawake wanaokaribia kukoma hedhi au waliokoma hedhi kabisa.
Tatizo pia huwatokea hata wanawake walio katika umri wa kati yaani miaka 25 hadi 40 hata kama bado hawajafikia umri wa kukoma hedhi kutokana na sababu mbalimbali.
Chanzo cha tatizo
Kama tulivyoona sababu kubwa ni kupungua kwa vichocheo vya ‘Estrogen’ lakini pia sababu nyingine zinazosababisha hali hii ni maambukizi ya mara kwa mara ukeni, upungufu wa kinga mwilini, matumizi ya baadhi ya dawa za homon kwa muda mrefu.
Maambukizi ya mara kwa mara ukeni ni kama vile fangasi, kuwepo na maambukizi ya kaswende, vioteo sehemu za siri, malengelenge, kutokwa na vipele na kuungua moto.
Matatizo haya yakijirudia mara kwa mara husababisha tatizo hili.
Dalili za tatizo
Mwanamke hulalamika muwasho ukeni, muwasho huwa sehemu ya nje na husambaa hadi ndani, ngozi ya ukeni huwa kavu na hutokwa na vidonda sehemu ya nje ambavyo hutoa majimaji na huwa kama vipele au vijipu uchungu.
Mgonjwa hulalamika maumivu makali wakati wa kukojoa na huhisi muwasho mkali kwenye njia ya mkojo.
Mwanamke hupata maumivu wakati wa tendo la ndoa na hutokwa na damu baada ya tendo la ndoa na kushindwa kufanya tendo kutokana na ukavu wa ukeni, uke kubana na kutoweza kufanya tendo kabisa.
Hali hii huambatana na kuhisi joto kali sehemu za siri, vidonda na kuhisi sehemu za siri nzito, kutokwa na uchafu mwingi mweupe ukeni unaotoa harufu mbaya huku ndani ukihisi kama viwembe vinakatakata.
Tatizo hili husababisha mwanamke aliyekoma hedhi kuona anatokwa tena damu, matatizo kwenye njia ya mkojo pamoja na maumivu wakati wa kukojoa, kutokwa na damu katika njia ya mkojo na kukojoa mara kwa mara.
Ukubwa wa tatizo
Tatizo hili pia huwapata wanawake wenye magonjwa sugu kama kisukari hasa kama kimepanda, mgonjwa wa kifua kikuu na muathirika wa virusi vya Ukimwi.
Tatizo pia huwatokea hata ambao hawana maradhi haya kama vile wanawake wenye matatizo katika mfumo wa homon hasa wale wanaotumia dawa za homoni kwa muda mrefu na wanaotumia dawa za antibayotiki kwa muda mrefu.
Matumizi ya vipodozi sehemu za siri husababisha mzio au ‘allergy’ ambao humfanya mwanamke alalamike mara kwa mara kuhusu tatizo la muwasho na kutokwa na uchafu ukeni kujirudiarudia, yaani unatibu baada ya muda fulani linarudi tena.
Uchunguzi na tiba
Uchuguzi hufanyika katika hospitali za mikoa na wilaya katika kliniki za magonjwa ya kinamama.
Vipimo ni kama vile vya kuangalia ukeni, vipimo vya damu na hata Ultrasound endapo mwanamke atalalamika anapata maumivu ya chini ya tumbo usawa wa kitovu kushuka chini.
Matibabu hutolewa baada ya uchunguzi wa kina.
Mwanamke azingatie usafi na aepuke kutumia dawa bila ya kufanyiwa uchunguzi wa kina.
0 comments:
Post a Comment