Aina hii ya mapenzi ni yale yanayowaunganisha vijana wawili; msichana na mvulana kwa lengo la kuwa na wakati wa furaha pamoja. Hawa hutoka pamoja kwenda kwenye sehemu za burudani kwa ajili ya kustarehe na kufurahika. Lengo mahsusi huwa ni kila mmoja wao kupata mwenza. Wao wenyewe huita ‘company’
Je, wewe kama mwanaume, unajua kinachokufanya upende? Kitu gani hukufanya umpende mwanamke mmoja na usimpende mwingine? Je, umewahi kustajabu kwa nini ndugu yako au rafiki yako anampenda mwanamke fulani ambaye wewe unaona hana mvuto wowote unaomfanya astahili kupendwa?
Wanaume wengi niliowauliza ni kitu gani huwafanya wapende walinijibu kuwa huvutiwa na uzuri wa sura. Ni wachache tu waliotaja sababu nyingine kama vile tabia, utajiri au umaarufu.
Pamoja na kukubaliana kuwa watu wengi huvutiwa na uzuri wa sura wakaingia katika penzi bado kuna swali moja ambalo hatuna budi kujiuliza. Kwa nini watu hutofautiana katika suala la uzuri? Mara nyingi nimewasikia watu mbalimbali hasa mwanaume wakibishana kuhusu uzuri wa wapenzi wao. Kila mmoja akisema mpenzi wake ni mzuri kuliko wa mwenzake. Hata nilipobahatika kuwaona wapenzi waliokuwa wakisifiwa, wakati mwingine hata mimi pengine sikuona kama walikuwa na uzuri wowote wa kusifika.
Lakini, kisaikolojia wala siwezi kujisifu nikasema kuwa mimi nilikuwa sahihi na kwamba wenzangu hawakuwa sahihi. Hili ni moja kati ya maswali magumu katika maisha yetu, ambalo halina jibu la moja kwa moja. Je, uzuri una kipimo tunachoweza kukitumia kuupima na kufikia mwafaka?
Mathalani, tunapotaka kupima urefu wa kitu kama vile nyumba tutatumia sentimeta na meta. Vile vile tunapopima uzito tutatumia kilo na hadi tani. Imethibitika hakuna kipimo cha mfano kama huu kinachoweza kutumika kwa kupima uzuri wa sura isipokuwa macho na hisia ya mtazamaji. Kipimo cha uzuri wa mtu, kimo katika macho ya mtazamaji. Hivyo mwanaume anaposema mwanamke fulani ni mzuri, kipimo chake ni jinsi yeye anavyomuona. Hicho ndicho kipimo chake sahihi cha uzuri, wala hana kosa lolote.
Ili tuweze kuelewa vyema kuhusu jinsi mtu anavyopenda, hatuna budi tufahamu tofauti iliyopo baina ya kupenda na hali ya kuwa katika penzi. Kisaikolojia, kupenda ni hatua ya kwanza ya mapenzi na kuwa katika mapenzi ni hatua ya pili. Hatua ya kwanza ndiyo ambayo katika makala hii tutaiita mapenzi ya mahaba ambayo kwa hakika yameenea zaidi katika siku hizi kuliko ilivyokuwa zamani.
Aina hii ya mapenzi ni yale yanayowaunganisha vijana wawili; msichana na mvulana kwa lengo la kuwa na wakati wa furaha pamoja. Hawa hutoka pamoja kwenda kwenye sehemu za burudani kwa ajili ya kustarehe na kufurahika. Lengo mahsusi huwa ni kila mmoja wao kupata mwenza. Wao wenyewe huita ‘company’
Kwa kawaida wanaume hupenda hadi wakalemewa na mapenzi kuliko wanawake. Aidha, mwanaume huvutiwa na penzi la mwanzo hata kabla ya kuamua lengo la penzi lake. Watafiti waliochunguza mwenendo wa mapenzi walihusisha wanaume vijana 250 na wanawake vijana 450. Waligundua kuwa zaidi ya robo ya wanaume waliingia katika penzi na wanawake waliotoka nao nje mara nne, lakini kwa upande wa wanawake walikuwa asilimia 15 tu. Kwa hakika karibu nusu ya wanawake hawakuingiwa na penzi
hata baada ya kutoka mara 20 na mwanaume, ambaye hata kama baadaye alikuja kuwa mpenzi. Walihitaji muda zaidi wa kukutana na kuongea na kijana, ndiyo aingie katika mapenzi. Ilibainika kuwa hali hii inatokana na ukweli kwamba wanaume huwa siyo wapambanuzi sana kama walivyo wanawake. Mara nyingi wanaume huweza kuvutika kwa mwonekano wa kwanza tu. Yaani wanaume huweza kuamua katika sikunde chache tu katika akili yake kama angependelea kuwa na uhusiano na hata kujikuta ameingiwa na hamasa ya kuwa na mapenzi ya mahaba.
Wanawake mara chache sana huweza kuwa na hali kama ya wanaume. Wao hulitazama penzi zaidi katika muktadha wa ndoa na hatima yao kimaisha. Wako makini zaidi katika uhalisia wa uhusiano unaokusudiwa kuanzishwa. Hadi miaka ya hivi karibuni ndoa kwa mwanamke kilikuwa ndicho kiini cha maisha yake yote.
Kwa mwanaume, pengine hakuwa anakabiliwa na changamoto nyingi kama ilivyo kwa mwanamke. Kwa mfano hata kama mwanaume ataghiribika na kuingia katika penzi kama ameoa au hajaoa, angeweza kuendelea bila kuathirika sana kwa sababu maisha yake yamewiana zaidi na kazi yake. Hata katika siku hizi ambazo kuna asilimia japo ndogo ya wanawake wanaofanya kazi, bado wanabeba sehemu kubwa ya dhamana ya kusimamia shughuli za nyumbani ili ziende vyema hususan kuhakikisha hali nzuri ya familia yake kama wale wanawake wanaokaa nyumbani wakati wote.
Katika makala hii sikusudii kuacha picha kuwa wanawake huwa hawana mvuto wa penzi la mwanzo, lakini wanawake wengi huviachia vichwa vyao, yaani akili zao zidhibiti mioyo yao hasa katika siku za mwanzo za penzi.
Kabla ya kuhitimisha makala hii napenda kusisitiza kuwa ile hali ya kuwa katika penzi ambalo nimeiita hatua ya pili ya penzi, ndiyo iliyo bora zaidi katika maisha. Hii ni kwa sababu hujenga hali ya kuelewana, kuhurumiana, kujaliana, kuthamiana na kuaminiana. Hali hii ndiyo ambayo huweza kuwavusha watu wawili hata katika mitihani midogo midogo ya maisha. Hata watu wawili wanaopendana wanapohitilafiana kwa kuwa penzi lao huwa imara, huwa halisambaratiki ila hugawanyika katika nusu mbili na kila mmoja akabaki na nusu yake. Penzi likiwa katika hali hii huwa rahisi kuliunga na kulirudisha katika hali yake ya awali.
0 comments:
Post a Comment