Wednesday, 9 July 2014

UNAZIJUWA ATHARI ZA KUTOMNYONYESHA MTOTO MAZIWA?






Unazijua athari za kutomnyonyesha mtoto maziwa? Masisterdoooo wote ambao hampemdi kunyonyesha somemi hapa

 


Taasisi ya Chakula na Lishe kwa kushirikiana na World Vision Tanzania wameandaa wiki ya unyonyeshaji duniani ambapo itaadhimishwa kuanzia Agosti mosi hadi 7 jijini Dar es Salaam.



Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo, Kaimu Mkurugenzi Idara ya Elimu na Mafunzo ya Lishe Onesmo Mella anaeleza kuwa wiki ya unyonyeshaji duniani hutoa fursa maalum kwa watu wote kuungana pamoja katika kuadhimisha na kukumbushana umuhimu wa kuendeleza na kuimarisha unyonyeshaji maziwa ya mama.



“Tunatumia wiki hii kuhamasisha jamii kuhusu njia bora za kumsaidia mama ili aweze kunyonyesha kwa ufanisi pamoja na kutoa taarifa muhimu zinazohusu ulishaji watoto wadogo hususani unyonyeshaji wa maziwa ya mama,” anasema.



Pamoja na hayo, anasema unyonyeshaji watoto maziwa ya mama unahimizwa kwasababu maziwa ya mama ni mlo bora, kamili na muhimu kwa mtoto wa binadamu kuliko chakula kingine katika siku za mwanzo za maisha yake.



Utafiti umeonyesha kuwa hali ya lishe ya mtoto ikiathirika katika siku za mwanzo wa maisha yake yaani kuanzia wakati wa ujauzito hadi kufikia miezi 18 ya kuzaliwa basi athari hizo haziwezi kurekebishwa kamwe.



Mella anasema mtoto atakuwa na upungufu katika ukuaji wake na maendeleo hivyo husababisha kupungua kwa uwezo wake kitaaluma, utendaji kazi na hata athari za kupata magonjwa mara kwa mara. Kwa hiyo ni muhimu kuhimiza unyonyeshaji maziwa ya mama ili kuwa na uhakika wa msingi bora wa maendeleo na ukuaji wa watoto ambao ni nguvu kazi ya taifa baadaye.




Kwa upande wa Tanzania tafiti zilizofanyika zinaonyesha kuwa unyonyeshaji watoto maziwa ya mama pekee kwa miezi sita ya mwanzo tangu wanapozaliwa, bila kuwapa chakula kingine chochote hata maji, hupunguza vifo vyao kwa asilimia 13.



Kiasi hicho ni karibu sawa na idadi ya watoto 9,800 ambao wangepaswa kufa kwasababu ya kutozingatia unyonyeshaji wa maziwa ya mama pekee kwa miezi hiyo sita ya mwanzo.



Wakati huo huo, tafiti nyingine zinaonyesha kuwa watoto walionyonyesha bila kupewa kitu kingine chochote kati ya mwaka 1999 na 2010 iliongezeka kutoka asilimia 27 hadi asilimia 50, pamoja na ongezeko hilo takwimu zinaonyesha kuwa wastani wa kunyonyesha watoto maziwa ya mama pekee nchini Tanzania ni miezi miwili tu.



Takwimu zaidi za tafiti zinabaisha kuwa asilimia 49 ya watoto waliozaliwa wanaanza kunyonyeshwa ndani ya saa 1 tangu kuzaliwa wakati asilimia 94 ya watoto huanza kunyonyeshwa ndani ya siku ya kwanza baada ya kuzaliwa lakini taratibu zinaelekeza kuwa mtoto anapaswa kunyonyeshwa maziwa ya mama ndani ya saa 1 baada ya kuzaliwa.



Asilimia 31 ya watoto waliozaliwa hupewa chakula au vinywaji zaidi ya maziwa ya mama kabla ya muda unaoruhusiwa wa miezi sita wa kuanzisha ulishaji wa vyakula vya nyongeza, kwa kadiri mtoto anavyokuwa, unyonyeshaji unaonyesha kupungua.



“Kwa mfano asilimia 11 ya watoto wenye umri wa tangu kuzaliwa hadi miezi miwili huanzishiwa vyakula vya nyongeza, asilimia 33 kwa umri wa miezi 2 hadi 3 na asilimia 64 kwa umri wa miezi 4 hadi 5,”anasema.



Anafafanua kuwa “changamoto iliyo mbele ya kila mmoja wetu ni kukabiliana na asilimia zilizosalia ili watoto wote wanaozaliwa waweze kunyonyeshwa kwa usahihi, kwa ujumla asilimia 97 ya watoto wa Tanzania wananyonyeshwa maziwa ya mama na asilimia 93 ya watoto hupewa vyakula vya nyongeza katika muda unaostahili kati ya miezi 6 hadi 9,”.



Pamoja na unyonyeshaji kuwa ni jambo lenye umuhimu mkubwa anasema zipo changamoto mbalimbali ambazo mama anayenyonyesha anakabiliwa nazo.



Changamoto hizo ni pamoja na kupambana na taarifa zisizo sahihi, mila na desturi potofu, kuendelea kunyonyesha awapo mbali na mtoto kwa mfano kazini, shambani na kwenye biashara na kunyonyesha wakati wa maafa na majanga.



Anasema changamoto kubwa alionayo mama ni kushinda wasiwasi alionao juu ya uwezo wake wa kumnyonyesha mwanaye kikamilifu. Kujiamini ni suala la msingi katika kuleta mafanikio kwa mwanamke anayenyonyesha.



Halikadhalika, mwanamke anayenyonyesha anahitaji kusikilizwa kwa makini, kupata taarifa muhimu, kupewa stadi  na kusaidiwa kwa vitendo pamoja na kutiwa moyo. Lakini bado ni vigumu kwa jamii nyingi kufanya hivyo.

Mambo kadhaa yanayokwamisha suala zima la unyonyeshaji katika jamii hususani katika nchi zinazoendelea ni kukosekana kwa elimu, rasilimali, miundombinu, upungufu wa chakula na vitu vingine muhimu kama kutoweza kuwafikia au kutokuwepo kwa wahudumu wa afya, makundi ya kuwasaidia akina mama na kutokuwepo kwa fursa za kuongelea masuala ya unyonyeshaji ni baadhi ya changamoto zilizopo.


Kwa mujibu wa Mello anasema zipo athari kubwa za kutonyonyesha watoto maziwa ya mama. Watoto wachanga na wadogo wasionyonyeshwa wana uwezekano mkubwa wa kupata magonjwa ya njia ya hewa na mzio allegies, kuharisha na kupata maambukizi mengine, kupata kiriba tumbo na kisukari.

Aidha, madhara mengine ni kupata pumu na matatizo ya kupumua, saratani za utotoni, kuwa na uwezo mdogo kiakili na maendeleo yasiyo ya kawaida ya ukuaji.

Mbali na mtoto pia mama na jamii nzima huathirika. Athari hizo huelezwa kuwa ni pamoja na kupata saratani ya matiti, kizazi, kisukari, kwa mama asiyenyonyesha, mwanamke kurudia siku zake mapema baada ya kujifungua na hivyo kuwa na uwezekano wa kupata ujauzito na mimba za karibu.


Anasema ili kufanikisha azma ya kumsaidia mama amnyonyeshe mtoto wake vizuri yapo mambo kadhaa yanapaswa kuwepo ili kutoa msaada kwake. Mazingira ya aina hii ni pamoja na mahusiano ndani ya familia na jamii yake.

“Mwanamke anayenyonyesha anapaswa kuwa na mahusiano mazuri na watu wote walio karibu naye ukianzia na baba wa mtoto au ndugu mwingine wa karibu, marafiki, majirani na jamii kwa ujumla,”anasema.

Anasema mahusiano ya karibu na watu hao yana mtia moyo na inamsaidia mama na mtoto kuwa karibu naye, wakati mwingine wanawake hushawishiwa vibaya au vizuri kutokana na kile wanachokisoma, kukiona na kukisikia kupitia vyombo vya habari hivyo anahimiza kuwepo kwa mahusiano mazuri na imara ili yaweze kusaidia kupunguza ushawishi mbaya kwa kutoa msaada unaohitajika.

0 comments:

Post a Comment