Thursday, 1 May 2014

YAFAHAMU MAGONJWA YALIYOKUWA HAYAPEWI KIPAUMBELE NA TIBA ZAKE KIUSAHIHI




Magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele
yapo kwenye jamii ya watu wa kona zote za
Tanzania tena kwa muda mrefu lakini
yalikuwa hayapewi kipaumbele kama ilivyo
kwa ugonjwa wa Malaria na Ukimwi.

Makala hii ilikuwa mahususi kwa mikoa ya
Dar es Salaam na Mwanza
kutokana na mada husika lakini si dhambi
kama wewe wa mkoa tofauti na hiyo
ukipata elimu hii kwa faida yako na familia
inayokutegemea.
Nimeanza kwa kueleza kwamba ni mada
mahsusi kwa mikoa hiyo kutokana na
mpango ulioandaliwa na Serikali wa
kutokomeza magonjwa yaliyokuwa
hayapewi kipaumbele kuanza kuzuiwa na
kutotibika katika mikoa hiyo.
Serikali kupitia uamuzi wa Shirika la Afya
Duniani (WHO) imeanza utekelezaji wa
kutokomeza magonjwa hayo yaliyokuwa
awali hayajapewa kipaumbe ambayo ni
Matende, Ngirimaji, Minyoo ya Tumbo,
Kichocho, Trakoma na Usubi.
Kwa mujibu wa takwimu zilizopo
inakadiriwa watu bilioni moja duniani tayari
wameathiriwa na magonjwa hayo na zaidi
ya watu bilioni mbili wapo hatarini kupata
magonjwa hayo.
Hata hivyo, Tanzania imeonekana kuwa ni
miongoni mwa nchi ambzo zinaweza
kupata maambukizi ya magonjwa hayo na
kila mtu yuko kwenye hatari ya
kuambukizwa moja ya magonjwa hayo
endapo hatazingatia ushauri wa wataalamu
wa afya.
Usubi
Aina hii ya ugonjwa husababishwa na
minyoo iitwayo, Onchocerca Volvulus.
Minyoo hao huenezwa na inzi weusi
wadogo wanaokaa kandokando ya mito
iendayo kasi.
Mtu aliyeathiriwa na ugonjwa huu, hupata
madhara ya ngozi kuwasha na kuwa na
mabakamabaka mithili ya mamba, kenge au
mjusi.
 
Matende na Ngirimaji
Ugonjwa huu husababishwa na minyoo
ijulikanayo kama, Wuchereria Bancrofti
inayosambazwa na mbu. Minyoo hiyo huishi
kwenye mfumo wa maji ya damu na
husababisha mtu kuvimba miguu, mikono,
matiti na sehemu za siri.
 
Kichocho
Ugonjwa huu husababishwa na minyoo
aina ya Schistosoma. Konokono ndiye
mwenezaji wa ugonjwa huo kwa kutoa
vimelea kwenye maji yaliyotuama na
binadamu huambukizwa kwa kugusa mahi
hayo.
Kichocho kikimpata mtu hutoka damu
kwenye haja ndogo (mkono) na haja kubwa
(choo) na usipotibiwa haraka huweza
kusababisha saratani ya tumbo, kibofu cha
mkojo na ini.
 
Minyoo ya tumbo
Aina hii ya minyoo ipo ya aina tatu ambayo
ni ya mviringo, mjeledi na safura. Aina hiyo
ya minyoo huishi ndani ya tumbo na
isipotibiwa mapema mwili kuwa dhaifu,
kupata tatizo la upungufu wa damu, tumbo
kujifunga na kifafa.
Madhara mengine ya ugonjwa huu ni mtoto
kushindwa kuhudhuria shule vizuri na
akiwa mhudhuriaji atakuwa na tatizo la
kuelewa vizuri masomo.
 
Trakoma
Ugonjwa huu nao ni miongoni mwa
magonjwa yaliyokuwa hayapewi
kipaumbele na huu wa trakoma,
husababishwa na bakteria aina ya
Chlamydia Trachomatis wanaosambazwa na
inzi na pia kwa njia ya kugusana kati ya mtu
mwingine na usipotibiwa mapema huweza
kusababisha upofu.

 
Malale
Huu husababishwa na vimelea aina ya
protozoa aitwaye, Trypanosoma. Hasa
ugonjwa huu huenezwa na Mbung’o na
husababisha udhoofu wa viungo vya mwili,
kichwa kuuma, kuvimba tezi za shingo,
kupungua uzito, kuchanganyikiwa, kulala
mara kwa mara hasa mchana na kukosa
usingizi.

Tauni
Ugonjwa huu husababishwa na bakteria
aina ya Yersinia Pestis na husambazwa na
viroboto vya panya.
Dalili za ugonjwa huo ni homa kali, maumivu
ya mitoki na mwili kuchoka.
 
Kichaa cha Mbwa
Ugonjwa huu husambazwa na virusi na
binadamu huambukizwa na kuumwa na
mbwa au wanyama wengine kama Mbweha
na Paka.
Hata hivyo, binadamu anaweza kupata kwa
kugusa mate ya mnyama mwenye ugonjwa
huo.
Mgonjwa wa kichaa cha mbwa anaweza
kupata dalili ya homa, kichwa kuuma, mwili
kuchoka, kushtuka, kuchanganyikiwa,
kupoteza fahamu, kuogopa maji, upepo na
wakati mwingine kushindwa kutembea.
Homa ya Papasi
Huu husababishwa na bakteria aina ya
Borrelia na huenezwa na Papasi.
Mgonjwa aliyeathiriwa na Papasi huonesha
dalili za homa kali, kichwa kuuma, mwili
kuchoka na kutapika.
Zipo njia za kuzuia kupata magonjwa hayo
ambazo ni kutumia dawa za kutibu dalili,
kusafisha uso na mwili kwa ujumla, kuweka
mazingira katika hali ya usafi wakati wote,
kutooga kwenye maji ya mto ambayo
hayatembei na kujikinga kuumwa na inzi,
mbung’o na mbu.
Ipo mikakati ya kudhibiti magonjwa hayo,
kwa Serikali kugawa dawa za kutibu na
kukinga maambukizi ya magojwa hayo na
dawa hizo hutolewa kila mwisho wa mwaka
mara moja kwa mwaka katika mikoa na
wilaya zote nchini zilizoathirika.
Mpango huu wa kugawa dawa za kinga tiba
utaanza kutolewa,
katika Mkoa wa Dar es Salaam na
Mwanza na dawa hizo zitatolewa bure
katika vituo vitakavyopendekezwa na
Serikali.
Kwa Mkoa wa Dar es Salaam utaratibu wa
unywaji dawa utawahusu watu wote wenye
umri wa kuanzia miaka mitato hadi wenye
umri wa uzee.
Hata hivyo magonjwa yatakayokuwa
yanatolewa dawa ni Ngiri maji na matende
kwa, Dar es Salaam kwa kumeza dawa aina
ya Albendazole na Mectizan na umezaji huo
utafanyika kwenye ndazi ya jamii na watoto
wenye umri wa kwenda shule watameza
dawa aina ya Praziquantel kwa ajili ya
kukinga kichocho.
Mkoa wa Mwanza utaratibu wa umezaji
dawa utahusu ugonjwa wa kichocho hivyo
watu wa mkoa huo watameza dawa aina ya
Praziquantel. Umezaji wa dawa hizo
utafanyika kwenye shule za msingi
walioandikishwa na wasioandikishwa
watapata huduma hiyo shuleni.
Ugonjwa wa kichocho umeenea karibu nchi
nzima na tatizo hilo liko katika kiwango cha
asilimia kati ya 12.7 hadi 87.6.
Utafiti umebaini kwamba ugonjwa huu
umeenea zaidi katika watu wa mikoa ya
Kanda ya Kaskazini, Kanda ya Kati na Nyanda
za Juu Kusini.
Ugonjwa wa mabusha na matende
umebainika kuenea nchi nzima lakini tatizo
kubwa liko katika sehemu za pwani ambapo
ukubwa wa tatizo hilo ni asilimia 1 hadi 69.

0 comments:

Post a Comment