Sunday, 4 May 2014

UFAHAMU KUHUSU FISTULA




Miongoni mwa magonjwa ambayo yamekuwa yakisumbuwa akinamama wengi katika jamii ni pamoja na fistula.Kitaalamu fistula ni tundu linatokea wakati mwanamke anapojifungua katika misuli kati ya uke na kibofu cha mkojo au kati ya uke na njia ya haja kubwa au vyote viwili.

Fistula inapojitokeza,mtoto kwa kawida huzaliwa mfu.Mara mama huanza kujisikia kutokwa na mkojo mara kwa mara,hali hiyo hujulikana kitaalamu kama Vesco-Vaginal Fistula (VVF) wakati hali ya kutoka kinyesi kupitia kwenye uke inajulikana kama Rectal Vaginal Fistula (RVF)
.

Katika nchi zinazoendelea sababu ya fistula ni kutokana na uzazi pingamizi unaohusiana na hali ambayo nyonga ya mama ni ndogo na hivyo kushindwa kuruhusu kichwa cha mtoto kupita salama.
WHO inasema chanzo kikubwa cha Fistula ni ufinyu wa njia ya uzazi wakati wa kuji fungua.Taarifa za madaktari zinasema matatizo ya fistula yanaongezeka, na hapa Tanzania kiwango kinafikia kinamama 1,200 kwa mwaka.

Fistula siyo tatizo pekee miongoni mwa kinamama wanaojifungua wakiwa na umri mdogo,bali pia kwa akina mama wenye umri zaidi ya miaka 40,na mara nyingi familia maskini zinaathirika zaidi kutokana na ukosefu wa lishe bora,huduma za afya na taarifa muhimu za afya.
Katika mazingira yenye kuwa na huduma za dharura za uzazi,hususani watoaji wa huduma za upasuaji wa kutoa mtoto,wanaweza kudhibiti matukio mengi ya uzazi pingamizi.Wakati ambapo huduma ya upasuaji ya kumtoa mtoto haipatikani au haitolewi kwa wakati unaofaa,msukumo wa kichwa cha mtoto unaweza kusababisha misuli ya uke ishindwe kufanya kazi na hivyo kujiachia na matokeo yake ni mama kupata fistula,au tundu kwenye misuli.Karibu kwa kila tukio la fistula,uzazi pingamizi pia unasababisha kifo cha mtoto aliyeko bado tumboni.

Kwa mujibu wa takwimu za shirika la Afya Duniani (WHO),kuna wanawake wanokadiriwa kufikia milioni 4 wanaoishi na matatizo ya fistula na wengine 50,000 hadi 100,000 hupata matatizo hayo kila mwaka.
Ni jambo la kusikitisha kuona kwamba kinamama wenye matatizo ya fistula wanabaguliwa,kudharauliwa na hata kulaumiwa na jamii  kutokana na harufu mbaya inayotoka kwenye mkojo na kinyesi chao.

Mwanamke mwenye fistula hawezi kumudu kuzuia mkojo au kinyesi kutoka kwenye mwili wake kutokana na kuwepo kwa mwingiliano usio wa kawaida kati ya sehemu hizo wazi,na kusababisha haja kubwa na ndogo kuvujia kwenye uke.

Wanawake wenye fistula wanaweza kuugua magonjwa kadhaa ikiwa ni pamoja na kushindwa kudhibiti utoaji wa mkojo au kinyesi,maambukizi ya kibofu cha mkojo,vidonda kwenye uke.Pia kadri ya wanawake watano,mmoja anaugua ugonjwa wa ulemavu “ulemavu wa kanyagio” unaosababisha kuharibika kwa mishipa katika mguu mmoja au yote na kusababisha ulemavu wa kutembea.

Kupatwa na fistula haimaanishi ndiyo kuteseka maisha yote,fistula inaweza kutibiwa kwa upasuaji,hata ikiwa miezi au miaka kadhaa baada ya kutokea na dalili nyingi au zote zinaweza kuondolewa na mama kurejea katika hali yake ya kawaida.kwa kulinganisha na mahitaji, huduma za matibabu ya fistula hazitoshi ikilinganishwa na idadi ya wataalamu ambao ni wachache.

Ili kuzuia fistula,upatikanaji wa huduma ya afya ni muhimu.kunahitajika mchanganyiko wa huduma bora kabla ya kujifungua ikiwa ni pamoja na uchunguzi,kuwepo na wakunga wenye ujuzi wakati wa kujifungua,na kutolewa kwa matibabu ya haraka inapotokea dharura na huduma bora baada ya kujifungua,yote haya yanaweza kuokoa maisha ya akina mama na kuzuia ulemavu wa aina nyingi ikiwa ni pamoja na fistula.

0 comments:

Post a Comment