Thursday 8 May 2014

TATIZO LA MIKONO KUKOSA NGUVU ( CARPAL TUNNEL SYDROME)



Tatizo hili linatamkwa ‘Kapo Tanel Sindrom’, ni hali ambayo mshipa mmojawapo wa fahamu kwenye kiganja cha mkono uitwao ‘median nerve’ unabanwa katika vifupa vya kiganja, mifupa hii inaitwa ‘Kapo boni.’ Vilevile sehemu hiyo kuna misuli ya nyuzinyuzi iitwayo Kapo ligament.
Kubanwa kwa mshipa huu husababisha kidole gumba kikose mawasiliano mazuri na nguvu vivyo hivyo kwa vidole vitatu vya kati.
Kwa hali hii dalili mbalimbali hujitokeza.Tatizo hili hutokea mara tatu zaidi kwa wanawake kuliko wanaume.
Chanzo cha tatizo
Tatizo hili hakuna chanzo maalum ingawa zipo sababu mbalimbali zinazochangia, matumizi ya mara kwa mara ya vidole na kwa muda mrefu hasa kwa wanaofanya kazi za uchapaji kwa kutumia mashine za Typewriter au computer. Watu wanaoshiriki michezo kwa kutumia zaidi vidole na viganja mfano michezo ya tenisi, wenye magonjwa ya mifupa kwa muda mrefu mfano ugonjwa wa baridi yabisi.
Mabadiliko katika mfumo wa homoni mfano kukoma hedhi, ujauzito na matatizo ya goita au uvimbe shingoni. Wenye ugonjwa wa kisukari na watu walioumia mikono au viganja.

Dalili za ugonjwa
Dalili zipo nyingi lakini zinatofautiana kati ya mtu na mtu, ila zipo dalili kuu ambazo kama siyo zote basi mojawapo mtu anaweza kuzipata.
Mikono inakosa nguvu kushika au kunyanyua kitu chochote hata kuandika unashindwa.
Wakati mwingine unahisi maumivu au ganzi mikononi, vilevile unaweza kuhisi vitu vinachomachoma kama sindano kwenye vidole, utahisi vidole kama vimevimba na unashindwa kukamata au kushika hata kitu kidogo.
Vilevile unaweza kuhisi kama vidole vinawaka moto hasa kidole gumba na vidole vya kati.
Usiku unapokuwa umelala hali ndiyo huwa mbaya ambapo maumivu na ganzi katika vidole huongezeka na inakufanya ukose usingizi, unashindwa kula, kunawa hata kuvaa kutokana na vidole na viganja kukosa nguvu.
Ugonjwa huu pia unafanana na magonjwa mengine kwa hiyo ni vema uwahi hospitali kwa uchunguzi wa kina.

Uchunguzi
Ugonjwa huu huwasumbua baadhi ya watu na huanza taratibu hata bila ya mgonjwa kujua tatizo limeanza vipi.
Mikono inapokosa nguvu huanza kutetemeka unapotaka kushika kitu au kuandika, yaani unahisi vidole na kiganja vinakuwa vizito.
Tatizo hutokea zaidi kwa wanawake na mojawapo ya sababu kama tulizoziona hapo mwanzo.

Uchunguzi huzingatia historia ya mgonjwa 
na kazi anazofanya, vipimo mojawapo ni kuangalia hali ya mkono na vipimo vingine ambavyo daktari ataona vinafaa hasa kuchunguza kama ana magonjwa mengine au matatizo yanayosababisha kama tuliyoona hapo awali.
Matibabu na ushauri
Tiba ya tatizo hili hufanyika baada ya uchunguzi wa kina hospitali, daktari wako ndiye atakayeamua aina ya tiba utakayopata kwa kuzingatia umri wako, hali halisi ya afya yako, historia yako hasa kama kuna aina nyingine ya magonjwa uliyonayo, ukubwa wa ugonjwa na mambo mengine yahusuyo tiba utajadiliana na daktari wako.
Matibabu yanayoweza kutolewa ni kama vile kudhibiti mienendo ya kiganja na vidole ‘Splinting of the hand’, dawa ambazo zinaweza kuwa sindano au vidonge, upasuaji wa kurekebisha tatizo au badilisha matumizi ya vifaa mfano aina ya ‘keyboard’ ya computer.

Tiba ya upasuaji
Ni operesheni ndogo inayofanyika katika kiganja kwa kuondoa nyama zinazolalia na kugandamiza mshipa wa fahamu. Baada ya hapo utapewa ushauri mwingine.

Ushauri
Hakuna njia maalum ya kujikinga ili usipatwe na tatizo hili ila zipo njia kadhaa zinazoweza kukusaidia usipatwe na tatizo au kupunguza nguvu unapobofya mashine au computer mfano mashine za risiti, ‘cash register, mashine za kupiga chapa, ni vema kutumia ‘keyboard’ laini ambazo utakuwa unagusa taratibu.

0 comments:

Post a Comment