Si wengi wetu wanaofahamu umuhimu wa kula samaki mara kwa mara na jinsi
kitoweo hiki kilivyo na umuhimu wa kipekee katika afya ya binadamu
Samaki ni kitoweo ambacho kinatajwa
na hata kupendwa na wengi, binadamu au wanyama.
Kitoweo hiki kinaelezwa kuwa na
mafuta yenye kiambata aina ya Omega 3 yanayomfanya binadamu kuwa na uwezo
mkubwa wa kufikiri, kutunza kumbukumbu na kuishi kwa muda mrefu.
Vyakula vyote vinavyozalishwa majini
huwa na kiambata aina ya Omega 3 yenye mafuta yanayotakiwa kwa mwili wa
binadamu yatokanayo na samaki, yana mbegu maalumu zinazomsaidia binadamu katika
ukuaji ambazo pia ni maalumu kwa faida ya mfumo wa ubongo na neva.
Tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa
watu wanaoishi maeneo ya pembezoni mwa bahari, maziwa, mito mikubwa wamekuwa na
uwezo mkubwa wa kufikiri, akili nyingi na wamekuwa wakiishi kwa muda mrefu
kutokana na kutokuzeeka mapema.
Kwa upande wa Tanzania, watu
waliozaliwa na kuishi maeneo ya pembezoni mwa bahari, maziwa, mito ikiwemo
kisiwa kama cha Ukerewe na maeneo mengine karibu na maziwa Victoria, Nyasa,
Rukwa hata visiwani Zanzibar wamebainika kuwa ni watu wenye akili nyingi na
wanaishi kwa muda mrefu ukilinganisha na maeneo mengine ya nchi kitakwimu.
Mkurugenzi wa Kituo cha Huduma ya
Ushauri Nasaha, Lishe na Afya, Counselnuth, Mary Materu anadhibitisha kuwapo na
virutubisho vingi vinavyopatikana katika kitoweo hiki cha samaki iwapo wataliwa
kwa wakati mwafaka mara tu baada ya kuvuliwa.
“Samaki wana kiambata aina ya Omega
3 ambayo husaidia katika ukuaji wa binadamu na kujenga ubongo wake vizuri,
ndiyo maana watu wanaoishi katika maeneo yaliyozungukwa na maji mengi
‘bahari, mito au maziwa’ ni watu wenye akili nyingi na watambuzi hata
kama hajaenda shule na akienda shule hufanya vyema sana darasani kama ni mtoto,
angalia watu wanaotoka ukerewe au sehemu nyinginezo,” anasema Materu.
Kinamama wajawazito kwa upande wao
wamekuwa wakipewa ushauri kutumia kitoweo hicho wawapo wajawazito na kuepuka
nyama nyekundu ambayo hata hivyo ni muhimu kwa mama mjamzito kutumia ili
kuongeza damu haraka kwa mjamzito.
“Wajawazito wanapaswa kula samaki
kwa wingi ili kukuza ubongo wa mtoto, pia ni lazima wale nyama nyekundu ili
kuongeza damu kwa uharaka mwilini ila tunawashauri isizidi nusu kilo kwa siku
saba,” na kufafanua umuhimu wa Omega 3 kwa wajawazito.
“Omega 3 humsaidia mtoto kukuza
ubongo, kutengeneza retina kwenye mboni ya macho na kutengeneza mfumo wa neva.
Pia, humsaidia mama kuzuia matatizo
kama kifafa cha mimba na sonono baada ya kujifungua. Njia kuu ya mtoto kupata
Omega 3 ni kutokana na vyakula anavyokula mama yake.
Kama mama atashindwa kupata vyakula
vya kutosha vyenye Omega 3, basi mtoto atachukua ile iliyoko mwilini mwa mama
ambayo mara nyingi iko kwenye ubongo wa mama.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya
Wanawake na Afya ya Uzazi kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH),
Dk Cyril Masawe anasema samaki wana umuhimu katika afya ya mama na mtoto
na iwapo mama hatapata Omega 3 ya kutosha anaongeza hatari ya kupata postpartum
depression, ‘mtoto mwenye uzito mdogo’, uchungu wa mapema (preterm labour),
‘mtoto kuzaliwa kabla ya muda’, au kulazimika kuzaa kwa upasuaji.
“Watoto ambao wamepata Omega 3 ya
kutosha wameonyesha kuwa na umakini mkubwa na upeo mzuri kuliko watoto wengine.
Pia, hukua kwa haraka zaidi kuliko yule ambaye hakupata kiambata hicho na huwa
mtunzaji mzuri wa kumbukumbu. Hupunguza matatizo ya kitabia, na kwa watu wazima
hupunguza uwezekano wa kupata saratani ya matiti na saratani nyinginezo.
Omega 3 inahitajika kwa kila
binadamu ili kuendelea kuutunza ubongo na kujiepusha na magonjwa yanayotokana
na kukosa madini haya.
“Ni vizuri kupata Omega 3 ya kutosha
kupitia mlo wa kila siku. Wakati wa ujauzito mwanamke anashauriwa kupata angalau
gramu 250 kila siku na katika kipindi cha mwisho (miezi mitatu ya mwisho) kwa
sababu katika kipindi hiki mtoto hutumia asilimia 70 ya Omega 3 kujenga ubongo
wake na mfumo wake wa neva.
Wataalamu hao wanaelezea vyanzo
vinavyoleta madini hayo kuwa vinapatikana katika samaki na mafuta ya samaki
hasa samaki wenye mafuta mengi kama vibua (mackerel), sato, salmon, sangara,
dagaa, herring na jodari.
Vyakula vingine vyenye Omega 3
Vyanzo mbalimbali vya habari duniani
vimewahi kuripoti kuwa wapo samaki ambao si wazuri sana kuwatumia kwani wana
sumu aina ya mercury kwa sababu ya machafuko ya kimazingira, hivyo unaweza pia
ukapata Omega 3 kutoka kwenye mayai, mkate, juisi, mboga za majani, canola,
alizeti, mafuta ya samaki na vyakula jamii ya mbegu.
Kama utapenda kumeza vidonge vya
Omega 3 uhakikishe kwamba havijatengenezwa na maini ya samaki kwani hizi zina
asilimia kubwa ya retinol Vitamin A, ambayo imegundulika kusababisha madhara
kwa watoto.
Omega 3 iliyotengenezwa kutoka kwa
nyama ya samaki na siyo maini ni bora zaidi. Kama huna uhakika ni bora kununua
vidonge maalumu vya Omega 3 vilivyotengenezwa kwa ajili ya wajawazito.
Inaelezwa na wataalamu kuwa mafuta ya samaki yanaweza kuchanganywa katika
vyakula vya mboga mboga ikiwemo za majani na hata katika kachumbari.
Tafiti za kimataifa
Mwaka 2012, wanasayansi kutoka
Marekani walifanya utafiti kwa watu 17,478 walio na umri chini ya miaka 64,
wanaoishi maeneo ya pembezoni mwa bahari na maziwa duniani ambao wamekuwa
wakila vyakula vya samaki na vyakula vinginevyo vinavyopatikana ndani ya maji.
Utafiti huo uliofanyika kwa miaka
minne, uligundua kuwa watu wanaoishi kwa kutegemea vyakula vya kwenye maji
huishi kwa muda mrefu na huwa na kumbukumbu nzuri na uwezo mkubwa wa kufikiri.
Hata hivyo iligundulika kuwa watu
wanaoishi kwa kutegemea samaki huepuka kupata magonjwa ya akili kwa asilimia
19.
Watafiti hao wanaeleza kuwa samaki
hula mimea iliyopo ndani ya maji yenye virutubisho ambavyo husababisha binadamu
atakayekula samaki huyo kupata virutubisho adimu kutoka kwa samaki huyo.
Hata hivyo, wanatanabaisha kuwa
virutubisho hivyo ni sumu ikiwa binadamu atakula pasipo kupitia kwa samaki.
Kiongozi wa utafiti huo, Dk Georgios
Tsivgoulis kutoka Chuo Kikuu cha Alabama, Marekani anasema “Watu wanaokula
vyakula vya samaki ni vigumu kupata matatizo ya akili na huwa na akili nyingi
zinazoambatana na kuishi kwa muda mrefu, hata hivyo mimea mbalimbali inayoota
pembezoni mwa bahari na maziwa ina virutubisho bora kwa afya ya binadamu,”
alisema Tsivgoulis.
Anasema samaki ni chakula
kinachofanya kazi kwa wepesi zaidi mwilini na kusaidia katika kuhifadhi kazi za
utambuzi katika maisha ya binadamu, hata hivyo huwa na virutubisho maalumu
ambavyo humfanya binadamu aishi kwa muda mrefu.
Wengine waligundua kwamba ulaji wa
mlo unaopatikana pembezoni mwa bahari wakiwamo samaki, husaidia kuondoa tatizo
la ugonjwa wa moyo, kupooza na kupunguza idadi ya wagonjwa wanaokufa kwa
shinikizo la damu.
Inaaelezwa kuwa watu wenye idadi
kubwa ya kiambata aina ya Omega 3 Omega 3 wana uwezekano wa kuishi kwa muda
mrefu ukilinganisha na watu wenye upungufu wa madini hayo ambayo hutokana na
samaki au mafuta ya samaki.
0 comments:
Post a Comment