Ni ajabu, wala si jambo
la kawaida kwa wanawake walio wengi kujikuta katika matamanio, kiasi cha
kujikuta wakilazimika kushiriki tendo la ndoa.
Hata hivyo, homoni
kadhaa zilizoko katika miili ya wengine zinawachochea kujitumbukiza kwenye
tendo hilo.
Utafiti wa baadhi ya
wanasayansi umeonyesha kuwa baadhi yao wana kiwango kikubwa cha vichocheo mwili
kinachoweza kushawishika kuwa na mpenzi wa nje au kumchoka haraka mwenza wake
baada ya kuishi naye kwa kipindi fulani.
Wanasayansi hao
wamefanya uchunguzi na kugundua kuwa, wanawake wenye kiwango kikubwa cha
vichocheo (homoni) aina ya oestradiol, wana mwamko mkubwa wa kushiriki tendo la
ndoa kuliko wanawake wenzao wenye kiwango kidogo cha vichocheo hivyo.
Vichocheo hivi aina ya
oestradiol (oestrogen) ni vile vinavyotumika katika kuzalisha mayai ya
uzazi wa mwanamke.
Pia, vichocheo hivyo ni vile ambavyo humpa mwanamke mwamko
wa tendo la ndoa.
Wanasayansi wa Chuo
Kikuu cha Saikolojia nchini Uingereza walifanya utafiti kuhusu uhusiano uliopo
kati ya vichocheo na tabia za watu na kubaini kuwa kiwango cha vichocheo
huweza kuelezea tabia ya mwanamke ikiwamo kumsababisha kuwa na tamaa za mwili
zaidi tofauti na wanawake wengine.
Wanasayansi hao, Dk
Kristina Durante na Norm Li walitoa ushahidi wa utafiti wao kuwa mfumo wa
kisaikolojia unachangia kwa kiasi kikubwa katika mwamko wa tendo la ndoa na
tabia kwa wanawake.
Wanawake 52 wenye
umri wa kati ya miaka 17 na 30, wote wanafunzi wa vyuo vikuu walishiriki katika
utafiti huo na kuambiwa wasitumie njia yeyote ya uzazi wa mpango kwa
sababu njia hizo huongeza vichocheo mwilini.
Kwa upande wao, watafiti
walipima kiwango cha homoni hizo kwa wanawake wote na walipewa maswali ya
kujibu yaliyohusu mienendo yao ya kimapenzi, kutosheka na wenzao pamoja na
uwezo wa kuvumilia kutofanya tendo la ndoa kwa kipindi fulani.
Pia, washiriki hao
walitakiwa kujibu maswali maalumu ambayo yanapima uwezekano wa washiriki hao
kuwasaliti wenzao wao.
Mwishowe, watafiti hao
walibaini kuwa, wanawake wenye kiwango kikubwa cha vichocheo vya oestradiol
wanapenda utani, wanapenda kupigana busu na ni rahisi kupata mwenza mpya wa
kudumu wakati wowote.
“Matokeo yetu yalibaini
kuwa, wanawake wenye kiwango kikubwa cha rutuba za uzazi hawatosheki na mwenza
mmoja hasa waliyeishi naye kwa muda mrefu. Wana uwezo wa kutafuta mwenza
mwingine anayewatosheleza,” alieleza Dk Durante.
Hata hivyo, daktari huyo
alisema kuwa, wanawake wa aina hiyo hawapendi kushiriki tendo la ndoa ovyo au
kuwa na wapenzi wa muda mfupi, bali wanaweza kuwa na wenza wawili wa kudumu ili
mradi wamtosheleze.
Almasi Nyangasa, Daktari
Bingwa wa magonjwa na upasuaji wa moyo anasema, vichocheo vya mwanamke
vinabadilika kulingana na mzunguko wake wa mwezi.
“Wanawake wana
vichocheo vya aina nyingi. Viwango vya vichocheo hivyo hubadilika
kulingana na mzunguko wake” anasema
Anaizungumzia homoni ya
oestradiol na kusema kuwa homoni hiyo inatakiwa kuwa katika kiwango cha
kawaida, ikizidi au ikipungua basi mwanamke anaweza kuwa na tabia zisizo za
kawaida.
Kwa mfano, mwanamke
anaweza kuwa na mwamko wa kufanya mapenzi au asiwe nao kabisa. Pia,
baadhi wanapata mabadiliko ya miili yao kama chunusi au kuwa na hasira.
“ Hata hivyo, si lazima
mwanamke mwenye kiwango kikubwa cha homoni hii akawa na uwezo mkubwa wa kushika
mimba. Wingi wa homoni hizo zinaweza kumfanya mimba ziharibike au asishike
kabisa” anasema
Dk
Nyangasa anasema tabia za mwanamke hubadilika pindi homoni zake
zinapopita katika mzunguko ambao husababisha yai kupevushwa na ama ashike
mimba au apate hedhi.
“Inawezekana mwanamke
akawa siyo wa kawaida, hivyo akawa na homoni hii kwa kiasi kikubwa hivyo akawa
na mwamko mkubwa wa tendo la ndoa” anasema
Anaongeza kuwa wingi au
uchache wa homoni huweza kuharibu mzunguko wa hedhi kwa mwanamke ambapo anaweza
kupata hedhi siku nyingi zaidi au siku chache.
Naye Dk Meshack
Shimwela, Bingwa wa Magonjwa ya Ndani ya Mwili, anasema homoni
humbadilisha mwanamke kwa hali ya ajabu.
Anatoa mfano kuwa wako
wanawake wenye vinyweleo vingi mikononi na miguuni, wenye sauti za kiume na
wenye miili imara mithili wa wanaume.
Kuhusu mwamko mkubwa wa
kujamiiana, Dk Shimwela anasema wingi wa homoni ukizidi unaweza kumfanya
mwanamke akawa na mwamko mkubwa lakini wapo ambao si wa kawaida.
“Kuna watu ambao si wa
kawaida, lakini hili linahusiana na saikolojia ya mtu pamoja na tabia yake,.”
Anasema.
Hata hivyo anasema,
mwamko wa kujamiiana humkuta kila mwanamke kadri homoni zake zinavyobadilika
lakini baadhi yao homoni zao zinakuwa nyingi na wanapata mwamko ambao si
wa kawaida.
Dk Antoinnete Molekhele
wa Kitengo cha Afya ya Uzazi, Hospitali ya Rosebank, Afrika Kusini anachambua
namna vichocheo vinavyofanya kazi na kusema kuwa, mayai ndiyo yanayozalisha
homoni.
“Mayai yetu
yanatengeneza homoni za oestrogen na progesterone kwa kiasi kikubwa na
kiasi kidogo cha homoni za kiume aina ya testosterone na andorstenedione,”
anasema
Pia, anasema wanawake na
wanaume wana homoni mbili za muhimu ambazo zinatengenezwa na tezi ya
‘pituitary’ ambazo ni FSH na LH.
Anasema kichochezi cha
FSH (Follicle Stimulating Hormones) kinadhibiti utengenezwaji wa mayai na
kichochezi cha LH (au luteinizing horomone) inasimamia utengenezwa wa vichocheo
vya mwamko wa kujamiiana.
“Kichochezi cha LH,
ndicho kinachosimamia kwa kiasi kikubwa mwamko wa kujamiiana na inapozidi
kiwango chake cha kawaida basi inaweza kumuathiri mwanamke,” anasema Dk
Molekhele
Kwa wanawake,
kiwango cha homoni za oestrogen (oestradiol) hupanda taratibu katikati ya
mwezi, kisha huanza kushuka kwa kasi wakati yai linachavushwa na siku ya 14
hushuka kabisa na mwanamke huanza kupata hedhi.
“Wanawake hutofautiana
viwango vya homoni hii na kuwafanya kuwa tofauti linapokuja suala la mwamko.”
Anasema
Anaongeza kuwa, homoni
humuathiri zaidi mwanamke ambaye anaanza kufikia kikomo cha hedhi, kwani wakati
mwingine huweza kupata dalili za ujauzito wakati hana au kupata hasira na
kukosa kujiamini.
0 comments:
Post a Comment