Kumekuwa na ongezeko kubwa la magonjwa ya mfumo wa
mkojo (UTI) na uzazi kwa wanawake, hii inasababishwa na sababu nyingi ikiwemo
ya kukosa uelewa sahihi wa kanuni za afya na usafi wa mwili pamoja na mazingira
yanayomzunguka mwanamke. Mada za usafi wa mwanamke ni pana sana siwezi kumaliza
kusema kila kitu, hivyo leo nitajikita zaidi katika matumizi sahihi ya pedi na
mambo ya kuzingatia kabla ya kunua pedi.
Wadada wengi wamekuwa wakitumia pedi na kuziacha
zikizagaa mitaani hali inayofanya nijiulize kama tu ameshindwa kujua sehemu
sahihi ya kuhifahi au kutupa pedi aliyotumia yeye mwenyewe, Je anauelewa upi
katika matumizi sahihi ya pedi hizo kabla hajazitumia?
Somo la leo nitajikita katika njia sahihi ya
kuchagua na kutumia pedi, makosa yanayofanywa katika matumizi ya pedi na
ushauri juu ya matumizi sahihi ya pedi na vitambaa kwa wale wanaovitumia.
Yafuatayo
ni makosa yanayofanywa katika uchaguzi na matumizi ya pedi kwa wanawake:
1. Kutonawa mikono kabla na baada ya kutumia pedi.
Mikono hushika sehemu mbalimbali hivyo kuna uwezekano ikawa na
vimelea vinavyosababisha magonjwa kwa hiyo kushika pedi bila kunawa mikono kwa
sabuni kunaweza kuhamisha vimelea hivyo kutoka mikononi na kwenda kwenye pedi
inayotegemewa kuvaliwa.
2. Kutunza pedi bafuni au chuoni. Wadada wengi
hupendelea kutunza pedi zao chooni/bafuni. Vyumba vingi vya choo/bafu havina
mwanga wa kutosha na kuwa na unyevunyevu hali inayoweka mazingira mazuri ya
ukuaji wa vimelea vya magonjwa kama bacteria na kitendo cha kutunza pedi katika
sehemu hizo kunaweza kusababisha kuhama kwa vimelea hao kutoka bafuni/chuoni
kwenda kwenye pedi isiyovaliwa na kupelekea pedi hizo kuwa
na vimelea vya magonjwa na mwanamke anakuwa katika hatari za
kupata maambukizi.
3. Kutoangalia muda wa matumizi wa pedi
kabla ya kutumia au baada ya kuzihifadhi kwa muda mrefu hali inayopunguza
kiwango cha ufanisi cha pedi sababu ya kuisha kwa muda wake wa matumizi.
4. Kununua pedi zinazouzwa kiholela kwa njia ya
utangazaji na za bei rahisi (promotion) ambazo baadhi zimeonekana kutengenezwa
kwa malighafi zilizo chini ya kiwango au kukaa kwa muda mrefu hivyo kuuzwa kwa
bei rahisi ili zitoke na kutumika haraka kabla ya kuisha muda wake.
5. Kutumia pedi ambazo zipo katika majaribio
maalum. Kama tunavyojua kuna kila aina za pedi mpya katika soko kwa kadri siku
zinavyozidi kwenda na baadhi ya pedi huingizwa sokoni kinyemela pasipo tafiti
za kutosha na bila hata kuthibishwa na mamlaka husika.
6. Kutumia pedi kwa muda mrefu. Wanawake wengi
hususani katika nchi zinazoendelea huwa hawamudu kutumia pedi moja kwa
muda wa masaa mawili kama inavyoshauriwa na wataalamu hivyo kujikuta katika
hatari ya kupata magonjwa ya mfumo wa mkujo na njia za uzazi .
7. Kupendelea pedi zenye uwezo mkubwa wa
kufyonza unyevunyevu ili ivaliwe muda mrefu pia ni tatizo sababu kwa kadri muda
wa kuvaa pedi moja unapozidi kuongezeka na hatari za maambukizi ya magonjwa pia
inazidi kuongozeka.
Wanawake
wanashauriwa kufanya yafuatayo ili kuhakikisha usalama wa afya zao :
1. Kunawa mikono vizuri kwa sabuni kabla ya
kugusa pedi ambayo unatarajia kuivaa na baada ya kuvaa kunawa tena mikono
vizuri.
2. Kutohifadhi pedi bafuni au chuoni au sehemu yote
yenye unyevunyevu na isiyo na mwanga wa kutosha ili kutotengeneza mazingira ya
kukua kwa vimelea vya magonjwa ndani ya pedi.
3. Kuangalia kwa makini muda wa matumizi ya pedi
kabla ya kununua au baada ya kutunza pedi kwa muda muda mrefu ili kuepuka
kutumia pedi zilizopita muda wake wa matumizi.
4. Kuepuka kununua pedi zinazouzwa kiholela na
zisizothibitishwa na TBS na mamlaka nyingine zenye dhamana ya kuangalia ubora
wa pedi hizo. Mwanamke anatakiwa kuangalia nembo ya uthibitisho wa
mamlaka hizo na kujiridhisha kuhusiana na usalama wa pedi hizo kabla hajanunua.
5. Kubadilisha pedi kila baada ya masaa
mawili, kama tunavyojua damu ni moja wapo ya chakula kizuri sana kwa vimelea
vya magonjwa kama bacteria, unyevunyevu unaosababishwa na kuvaa pedi kwa
muda mrefu pia unapelekea ustawi wa bacteria hao na joto ambalo lipo
katika maumbile ya ndani ya mwanamke vikiungana kwa pamoja vinatengeneza
mazingira mazuri ya ukuaji wa bacteria , hivyo wanawake wanashauriwa kutovaa
pedi hizo kwa muda usiozidi masaa mawili ili kuepuka mazingira hayo.
6. Kuchagua aina sahihi inayokutosha ina
kuepuka pedi zinazobana sana kupita kiwango sababu zinaweza pia kukufanya usiwe
huru na kutengeneza joto la ziada na michubuko katika maumbile ya
mwanamke,hivyo mwanadada unashauriwa kutumia pedi itakayokukaa vizuri(isilegee
sana wala kuachia sana)
7. Kwa wadada wanaotumia vitambaa badala ya pedi ni
muhimu pia kuzingatia kanuni za kiafya na usafi kabla na baada ya kutumia
vitambaa hivyo kama vile kuchagua kitambaa angavu ,kukiloweka na kukifua
vizuri, kuanika kwenye sehemu yenye mwanga wa jua wa kutosha na upepo wa
kutosha pasipo na unyevunyevu ,kupiga pasi kabla ujakihifadhi na kabla ya
kutumia ili kuuwa vimelea vya magonjwa na kuvitunza sehemu nzuri ambayo haina
unyevunyevu, penye hewa na mwanga wa kutosha na mwisho ni
kubadilisha kitambaa hicho kila baada ya masaa mawili pamoja
na kunawa mikono vizuri kabla na baada ya matumizi ya vitambaa hivyo.
0 comments:
Post a Comment