Sunday 11 May 2014

NAMNA YA KUKABILIANA NA TATIZO LA MOYO KUSHINDWA KUFANYA KAZI



Magonjwa ya moyo yameshika kasi hapa nchini kiasi cha kutishia uhai wa watu wengi.
Ripoti ya iliyotolewa na Taasisi ya Afya ya Ifakara  hivi karibuni inaeleza kuwa hospitali na zahanati nyingi hazina vipimo vya moyo. Hali hii inatishia usalama wa afya za watu ambao wanakwenda kwenye zahanati hizi  lakini hawapati tiba sahihi na badala yake wanaambulia kupimwa malaria tu.
 Hata hivyo maradhi haya kwa asilimia  8o yanazuilika kama hatua za mapema zitachukuliwa. Ndiyo maana upo usemi usemao,  kinga ni bora kuliko tiba  hivyo ni vema kuchukua hatua mapema kuliko kusubiri tatizo likukumbe.
 Pale unapoona dalili zisizo za kawaida fika haraka katika huduma za afya kwa ushauri, ikumbukwe kuwa gharama za kutibu magonjwa haya huwa ni kubwa ukilinganisha na magonjwa mengine pia muda wa kukaa hospitalini huwa ni mrefu.
Tatizo la moyo linaweza kuanza na kupotea kwa muda mfupi lakini  usipolitatua mapema huenda likawa sugu hivyo kuhitaji matibabu ya kina na kukugharimu maishani.
Leo tunaendelea makala yetu ya moyo kushindwa kufanya kazi, nitaeleza  kifupi matibabu, uchunguzi na namna yakujikinga.
Matibabu na uchunguzi
Ingawa pia yapo mambo mengi ya kuchunguza yaani maabara na picha nitagusia yale ya yanayohusu picha maalum za mwili.
Uchunguzi wa msingi unahusisha picha ya xray ya kifua kuona ukubwa wa moyo na uwepo wa maji katika mapafu.
Kipimo cha ‘echocardiogram-kipimo hiki huchunguza sehemu za moyo kama vile chemba, vyumba, valvu, mishipa na mfumo wa vimishipa vya fahamu katika moyo.
Kipimo cha electrocardiography-ECG-kuangalia shinikizo la damu, mapigo ya misuli ya moyo, kuoza kwa misuli ya moyo na hali ya kiumeme katika moyo.
Matibabu
 Baada ya daktari wako kukufahamisha kutokana na dalili ulizonazo ndipo atafanya uamuzi ama upewe dawa au usipewe dawa.
Kupumzika muda mrefu ili usiuchoshe moyo  wako wenye tatizo lakini pia mgonjwa anatakiwa alale katika mkao maalum utakaosaidia apumue vizuri yaani mito zaidi ya mwili huwekwa nyumba ya mgongo na kichwa. Kama kuna kitanda maalum robo ya kitanda huinuliwa juu kidogo.
Kutotumia chumvi na kunywa maji kipindi cha ugonjwa. Mambo mengine ya kuzingatia ni kula mlo usio na mafuta mengi ya wanyama, kula mboga na matunda zaidi katika kila mlo na vyakula visivyokobolewa.
Matibabu ya dawa huwa ni maisha yako yote, kama vile unavyomwona punda akivuta toroli kubwa lenye mzigo mzito kwa tabu, ili mnyama huyu aweze kuvuta toroli kwa urahisi inabidi kupunguza mzigo na kuuweka pembeni ili aweze kusonga mbele.
 Mfano huo ndivyo dawa za moyo zinavyofanya kazi ili kuurudisha moyo katika hali ya kawaida na kufanya kazi ya kusukuma damu. Katika huduma za afya wataalam wa moyo watakuelimisha zaidi

juu ya madhara ya dawa na ugonjwa kwa mfano ushauri nasaha wa tatizo linalowapata wagonjwa hawa huwa na upungufu wa nguvu za kiume kwa kipindi cha ugonjwa lakini baada ya kupata nafuu mtu hurudi katika hali yake.
Dawa ni kama vile za kupunguza mrundikano wa maji mwilini, kuifanya misuli ya mwili ikunjuke zaidi na kusukuma damu, dawa za kutanua mishipa ya damu na mwisho ni kutibu tatizo lililosababisha moyo kushindwa kufanya kazi.
Yapo baadhi ya magonjwa ya moyo yanayosababisha moyo kushindwa kufanya kazi  ambayo kwa kawaida huwa hayaponi.
Hivyo dawa nyingi ni zile zakusaidia moyo ufanye kazi vizuri, na dawa hizi unapaswa kutumia kufuatana na maelekezo ya daktari kwani endapo utazidisha kipimo zina madhara na pengine kusababisha moyo kusimama na hatimaye kifo.
Namna ya kujikinga na tatizo hili kiujumla
Fika mapema katika huduma za afya pale unapoona dalili, jenga utamaduni wa kupima mapigo yako ya moyo, sukari ya mwili na kiwango cha lehemu mwilini (cholestrol) hii inasaidia kujua mwenendo wa afya yako.
Lehemu ni mafuta mabaya yanayosababisha kuharibika mishipa inayopeleka damu katika misuli ya moyo.
Kufanya mazoezi mara kwa mara na mapema kabla ya kupata matatizo ya kiafya ni nzuri kwa afya yako.
 Mazoezi yanaufanya mwili utumie mafuta ya ziada yaliyorundikana mwilini na pia kuufanya mwili kuwa na mzunguko mzuri wa damu, angalau mazoezi ya kutembea kwa siku kwa dakika 15-30 yanatosha.
Epuka hasira, shinikizo la kiakili na sonona.Epuka matumizi ya pombe kupita kiasi na tumbaku kwani vitu hivi vina madhara katika moyo na mishipa ya damu.
Ugonjwa wa moyo huweza kumpata mtu yeyote bila kujali umri, na katika siku za karibuni mtindo wa maisha umewafanya watu wengi kupata maradhi haya kutokana na ulaji holela wa mlo usiozingatia afya na kuacha kufanya mazoezi.

0 comments:

Post a Comment