Kwa bahati mbaya dhana hii
potofu bado ipo miongoni mwetu. yamejengeka mawazo kuwa menopause ni
kipindi kigumu kinachoweza kumfanya mama awe kichaa, na hata kufikia hatua
ya kumdunda mwenza wake!
Kwa kuwa mabadiliko
yanayosababisha hali hii ni mengi na mapana, nitajadili mabadiliko yanayoletwa
na hali hii na jinsi ya kuyakabili.
Kwa akina mama mama wengi,
hedhi inaanza katika umri wa takribani miaka 14 na kukoma katika umri
nilioutaja mwanzo. Katika hali ya kawaida, kuona au kutoona hedhi
kunasababishwa na kuwepo au kutokuwepo kwa mzunguko wenye uwiano mzuri wa homoni
nne kuu; mbili zikiwa
zinatengenezwa na tezi za kutengeza mayai ya uzazi na
ambazo ni kuu katika maisha ya uzazi wa mwanamke: estrojeni na projesteroni
na zingine mbili toka kwenye
ubongo.
Homoni hizi ndizo
zinasababisha kukua na hatimaye aghalabu yai moja kupevuka na kutoka katika
tezi moja kati ya mbili alizonazo mama kila mwezi. Kama yai hili
litakutana na mbegu ya kiume, basi mama atatunga mimba na tangu hapo hedhi
inakoma mpaka baada ya kujifungua.
Kama itakuwa vinginevyo,
utando wa ndani ya mfuko wa
uzazi wa mama ambao ulikuwa umeandaliwa na
mabadiliko ndani ya mwili wa mama kuitunza mimba kwa sababu ya homoni
hizi, unatoa damu tunayoiita hedhi. Mara nyingi mzunguko huu unajirudia kila
mwezi mpaka mama
anapofikia menopause.
Ikitokea kuwa mfumo wa
kutengeneza homoni hizi au uwiano wake katika mwili una shida au vyote
viwili, hedhi
ya mama inakuja kwa mpangilio usio mzuri. Aghalabu hili ni jambo
la kawaida katika miaka ya mwanzo ya hedhi (miaka minne hadi sita ya mwanzo wa
hedhi) na miaka miwili hadi
minane kabla ya menopause.
Matatizo yanayotokea mama
anapokaribia menopause yanasababishwa na mambo makuu manne. Mosi, ni
ukweli kwamba homoni mbili muhimu katika mpangilio wa kuona
hedhi kila
mwezi kwa mpangilio zinaanza kutengnezwa katika mfumo usiotabirika sana na tezi
za mama.
Hali hii inasababisha hedhi
kutotabirika; yaweza kuja mara kwa mara au baada ya muda mrefu na kwa baadhi ya
akina mama inaambatana na damu nyingi isiyo kawaida yao.
Pili, ni mabadiliko
yanayoambatana na vichomi joto (hot flushes) kichwani, shingoni na
kifuani ambavyo aghalabu huambatana na hisia ya joto jingi mwilini na kutoka
jasho
jingi hasa wakati wa usiku. Kwa kawaida hali hii inachukua sekunde au
dakika chache ingawa kwa nadra yaweza kuchukua saa moja hivi na inatokea na
kujirudia mara kwa
mara.
Hali hii inaweza kuleta
usumbufu mkubwa na hali ya wasiwasi katika maisha ya kila siku ya mama.
Tatu, ambalo nalo
linasababishwa na upungufu wa homoni nilizozitaja ni baadhi ya viungo
vya mama kuanza
kuonyesha hali ya uzee kama vile viungo kulegea kinyume na hapo
mwanzo. Mabadiliko haya hutokea katika viungo mbalimbali vikiwemo vya uzazi. Ni
wakati huu ambapo ngozi
ya mama inaanza kulegea, mama kuwashwa sehemu za siri
na kupata matatizo mbalimbali katika mfumo wa mkojo kama vile kusikia maumivu
anapokojoa na baadhi hata kushindwa kuuzuia mkojo wanapopata hisia za kukojoa.
Mwisho ni matatizo ya kiafya yanayoweza
kutokea miaka mingi baada ya hedhi kukoma kwa sababu ya ukosefu wa homoni
ya oestrogeni kama mifupa ya mama kupoteza uimara wake na magonjwa
yanayohusiana na mzunguko wa damu na moyo.
Ingawa mwanzoni kulikuwa na
dhana kuwa akina mama wengi wa Kiafrika hawapati matatizo mengi yanayohusiana
na mifupa kupoteza uimara baada ya kufikia menopause, ushahidi wa
karibuni unaonyesha kuwa yawezekana magonjwa haya si nadra kama ilivyofikiriwa.
Pengine sababu kubwa
iliyojenga dhana hii ni kukosekana kwa akina mama wengi wa Kiafrika wanaoishi
kufikia umri wa miongo saba au zaidi. Ni wakati huu ambao akina mama
wanaweza
kuvunjika mifupa kirahisi na kama huduma za matibabu sio nzuri, hali hii
inaweza kusababisha vifo.
Ikumbukwe kuwa mifupa ya mama
inajengeka kwa kasi
mara baada ya kuvunja ungo na mara nyingi kasi hii inakoma
kabla ya kufikia umri wa miaka thelathini. Baada ya umri huu, taratibu mifupa
ya mama inaanza kuwa dhaifu
na hali inaendelea kwa kasi baada ya kufikia menopause
mpaka takribani miaka kumi na tano baada ya hapo.
Chakula chenye madini mengi
ya calcium na vitamini D,
mazoezi ya mwili na kuepuka unywaji
pombe wa kupindukia na uvutaji sigara, ni vitu muhimu vinavyosaidia kuifanya
mifupa ya mama kuwa imara.
Bahati nzuri akina mama wengi
wa Kiafrika wana mifupa imara zaidi kuliko akina mama wa nasaba zingine, na
hivyo kuishi maisha yanayosaidia kuifanya mifupa imara zaidi
kunaweza
kuchelewesha madhara mengi yanayotokana na matatizo ya mifupa yanayotokana na
utu uzima.
Vile vile ikumbukwe kuwa
katika hali ya maisha
yanayozingatia afya njema, magonjwa ya moyo na
presha si mengi miongoni mwa akina mama walio katika umri wa
kupata hedhi
kama ilivyo kwa wanaume wa umri sawa, lakini hali hii inabadilika baada ya menopause
ambapo jinsia zote zinakuwa katika uwezekano sawa wa kuugua magonjwa haya.
Kwa bahati mbaya umri wa menopause
na baada ya hapo ni wakati ambao binadamu wengi wanakumbana na matatizo
mbalimbali ya kimaisha na kiafya bila kujali jinsia na wale
wanaoishi miaka
mingi zaidi kama akina mama.
Kwao, hiki ni kipindi cha
kuwapoteza wenzi wao, kukosa huduma mbalimbali za kiafya hasa katika jamii
zisizo na
mfumo imara wa huduma za afya, na pia ni kipindi cha kustaafu kutoka
katika ajira zao au kupungukiwa na nguvu
za kufanya shughuli za awali za kuwaingizia
kipato cha uhakika, na hivyo kulazimika kuishi maisha mapya na
pengine magumu
kuliko awali. Ikitokea mama akapata matatizo ya kiakili wakati huu, ni rahisi
sana kuyahusisha na hali ya mabadiliko yake.
Vilevile ikumbukwe kuwa
magonjwa ya mfadhaiko (depression) mara nyingi yanawapata wanawake
kuliko wanaume, na yakitokea wakati huu si ajabu yakahusishwa
na mabadiliko
yanayompata mama!
Maisha ya mama wakati huu
yanategemea, kwa kiasi kukubwa, jamii iliyomzunguka na matarajio ya jamii hiyo
kwake. Kama jamii husika ina misingi fulani ya maisha, basi, mama
ataifuata. Kwa mfano, kama si kawaida mama kumdunda mume, ni nadra mama kufanya
hivyo kwa sababu
tu amefikia menopause kwa sababau suluhu ya matatizo ya
ndani ya nyumba yatatatuliwa kwa njia na utaratibu wa
jamii husika.
Ni nini cha kufanya katika
umri huu? Vi vyema jamii, mama na wahudumu wa afya waelewe mabadiliko haya na
kumsaidia mama kama inavyostahili. Jamii ielewe kuwa
watu wengi kwa baraka za
Mungu na huduma nzuri za afya wanaweza kuufikia umri huu na kwamba mabadiliko
yanayotokea ni ya kawaida katika maisha ya binadamu.
Zamani katika jamii nyingi za
Kiafrika, huu ulikuwa ni wakati ambao mama alikuwa na wajukuu, na hivyo kuitwa
nyanya na aliweza kupewa majukumu yaliyo wazi na mara
nyingi alisaidiwa katika
shughuli mbalimbali. Bahati mbaya ukaribu huu umeanza kufutika kwa sababu ya
mfumo wa
maisha ya sasa.
Hata hivyo, wahudumu wa afya
katika ngazi zote hawana budi kuelewa hali hii na pale inapowezekana mama
aambiwe mabadiliko yanayotokea mwilini mwake na pengine
kumsaidia amwone
daktari bingwa wa magonjwa ya akina mama aliye karibu kwa ushauri na tiba kama
inahitajika.
Bahati nzuri matatizo mengi
niliyoyataja yanaweza kutibika au kupunguzwa makali yake.
Nasisitiza kuwa ni vyema
wahudumu wa afya wawe na ujasiri wa kuwauliza akina mama hawa mambo mbalimbali
yanayohusiana na mabadiliko yanayowapata na siyo kusubiri mama aeleze kama
anayapata au la.
Yumkini matatizo yanaweza
kuwepo lakini mama akaona aibu akuyasema au kufikiri ndio uzee wenyewe na
kuamua kufa ‘kisabuni’. Kwa mfano, wengi wa mama hawa wanaendela na maisha ya
unyumba na pale yanapotokea
matatizo, hakuna budi wasaidiwe kuweza kufurahia
maisha haya kama watu wengine.
Akina mama hawa ni mama,
nyanya, dada, shemeji na hata jirani zetu, na zaidi ya yote ni Watanzania na
binadamu wenzetu. Hakika, wanahitaji msaada wetu sote.
0 comments:
Post a Comment