NIMEKUWA nikitafuta maneno
sahihi ya Kiswahili yenye maana sawa na maneno mawili ya Kiingereza - menopause
na climacteric, lakini juhudi zangu zinaonekana kutozaa
matunda.
Menopause (hedhi
kukoma mfululizo kwa miezi sita au zaidi), ni hatua ya mwisho ya mabadiliko
yanayotokea kwa
mwanamke; aghalabu kwa sababu ya utu uzima. Hii ni hatua
inayotanguliwa na kipindi cha mpito chenye mabadiliko mengi kutoka katika mfumo
unaotabirika wa kuona hedhi
unaoambatana na tezi za uzazi (ovaries)
kutoa angalau yai moja kila mwezi na kufikia hali ya hedhi isiyo na mpangilio
thabiti ambayo mara nyingi inaambatana na tezi za uzazi
kushindwa kutoa yai na
kuhitimishwa na kukoma kwa hedhi.
Climacteric ni mabadiliko
ya kimwili na kifiziolojia yanayotokea kwa akina mama, kwa sababu ya utu
uzima, yanayoanza pale hedhi ya mama inapoanza kubadilika na
kuwa ya mpangilio
usio thabiti, kupitia katika hali ya hedhi kukoma (menopause) na
kuhitimishwa na mabadiliko yanayotokea baada ya ukomo huu.
Katika hali ya kawaida ya fiziolojia
ya mama, wengi hufikia menopause katika umri wa takriban miaka hamsini
hivi.
Baadhi ya akina mama
wanafikia menopause kwa sababu tofauti kama vile operesheni ya kuondoa
tezi za
kutengeneza mayai, tiba mbalimbali kama vile ya kansa kwa kutumia
mionzi au kwa akina mama wachache, hii inaweza kutokea kwa sababu ya mabadiliko
yasiyotarajiwa ya kufikia hali hii katika umri mdogo bila sababu za wazi.
Takriban asilimia kumi ya
akina mama hufikia menopause kabla ya umri wa miaka arobaini na tano.
Kwa kuwa sababu mbili za mwanzo kati ya tatu nilizozitaja siyo za asili, mama
hana kipindi cha mpito na hivyo hufikia mabadiliko ya
menopause mara
moja.
Ushahidi uliopo unaonyesha
kuwa muda wa binadamu kuishi umeongezeka sehemu nyingi duniani isipokuwa baadhi
ya sehemu za Afrika ya Kusini mwa jangwa la Sahara. Binadamu wanaishi miaka
mingi zaidi sasa kuliko huko
nyuma.
Kwa mfano, inakadiriwa kuwa
miaka 100 kabla ya kuzaliwa Kristo, binadamu aliishi wastani wa miaka 18 tu na
kwa nchi kama Marekani umri huu ulikuwa umeongezeka na kufikia takriban miaka
49 mwanzoni mwa karne iliyopita.
Tangu mwanzoni mwa karne hii,
umri huu umeongezeka na kufikia karibu miaka 80 kwa wanawake na miaka 74 kwa
wanaume. Ikumbukwe kwamba katika nchi nyingi duniani,
wastani wa kuishi wa
wanawake ni mrefu zaidi ya wanaume kwa sababu mbalimbali zilizo nje ya wigo wa
makala hii na kwa sababu hii akina mama wengi wanaweza kuishi na kufikia menopause
sasa kuliko ilivyokuwa huko nyuma.
Takwimu za muda mrefu kama
hizi kwa nchi kama Tanzania ni nadra kupatikana; lakini kitu kilicho wazi ni
kwamba , akina mama wengi nchini mwetu wanaufikia umri huu sasa
kuliko huko
nyuma kwa sababu idadi ya watu imeongezeka na hali ya maisha kuboreka ikiwemo
baadhi ya huduma za afya zinazozuia vifo vingi vya utotoni.
Sensa ya watu na makazi
iliyofanyika mwaka 2002 ilionyesha kuwa takriban asilimia nne ya Watanzania
walikuwa ni akina mama wenye umri wa menopause. Kwa
kutumia takwimu za
sensa hii na umri tarajiwa wa mama kuingia katika menopause, karibu
akina mama nusu milioni
walifikia hali hii mwaka huo.
Vilevile, idadi ya wanawake
wenye umri wa miaka hamsini na zaidi ilizidi ya wanaume, na hivyo kutoa
ushahidi kuwa hata nchini mwetu wastani wa umri wa kuishi wa wanawake
ni zaidi
ya ule wa wanaume.
Zamani, jamii nyingi na hata
madaktari walifikiri kuwa ukomo wa kuona hedhi unatokana na tezi za kutengeneza
mayai kuchoka baada ya miaka mingi ya kazi na kwamba
tezi hizi zilitoa sumu
katika mwili wa mama na hivyo kuathiri viungo mbalimbali ikiwemo ubongo; sumu
ambayo ilisababisha matatizo ya mfadhaiko na hata kichaa.
Ingawa ni kweli kuwa menopause
husababishwa na tezi za kutengeneza mayai kuishiwa nguvu za kutengeza mayai na
virutubisho vinavyohitajika katika mwili wa mama vinavyoitwa homoni,
hali hii haina uhusiano na matatizo ya
akili. itaendelea sehemu ya pili....
0 comments:
Post a Comment