Monday, 19 May 2014

MAPARACHICHI NA MAPAPAI: WAFALME WA MATUNDA -2






Ukipita maduka ya Uzunguni utakuta vyakula mbalimbali vinauzwa toka Afrika. Matunda haya yanayothaminiwa sana Majuu, huuzwa bei aghali sana.
Hapa London ambapo kila aina ya chakula ulimwenguni hupatikana bei za matunda ziko hivi, kiwastan:
1. Kichani kimoja cha ndizi kisukari (mara nyingi toka visiwa vya Ngazija au Mauritius) ni £2-£3. Kama shilingi 6-7,000. Ona chini ilivyo mbaya ukilinganisha na zinazopatikana Arusha, Mbeya au Kilimanjaro…
Ndizi Kisukari-pic by F Macha
2. Parachichi – hupimwa kufuatana na uzito. Kuna vijiparichichi vidogo vyeusi ambavyo vimejazana katika maduka makubwa makubwa (supamaketi) vijiparachichi koko- si vizuri hata kidogo- halafu aghali- mara nyingi si vitamu au vimeharibika ndani. Maparachichi makubwa makubwa toka Afrika nan chi za joto (tropics) hupatikana maduka ya pembe za chaki, kwa Wahindi au sokoni. Bei yake moja kiwastani ni £1.50- £2 kuendelea. Takriban 5,000.
Maparachichi Mawili-by F Macha
3. Maembe kiwastani ni kama maparachichi – ila miaka ya karibuni yameanza kupungua bei na hupatikana kirahisi (kufuatana na msimu). Maembe haya( kama mananasi ) hutoka Ivory Coast, Costa Rica na Brazil.
4. Papai-pia hupimwa kwa uzito. Makubwa hayapatikani kabisa katika supamaketi za Kizungu. Ukilitaka uende mitaa tunaoishi wageni, ya wafanyakazi , Wahindi na Waturuki. Haya yanatoka Brazil – bei yake ni £5 (Shilingi 12,000) kuendelea.
Tikiti Maji-1
5. Tikiti Maji- haya yako aina nne. Ya kijani nje, rangi ya chungwa ndani “Cantaloupe” yenye vitamin kibao huzwa wastani wa £1; ilhali manjano (toka Brazil) na kijani nje(toka Hispania ) wastani £2; aghali kuzidi yote ni tikiti maji lenyewe- kijani nje, jekundu ndani (“water-melon”);
£2.50 (Shs 6,000) kuendelea. Faida zake ki-afya hazisemeki.
6. Cherries na Strawberries. Matunda ya Kizungu. Kabla sijaja Majuu sikufaham Cherries, lakini Strawberry hupatikana maduka ya Kizungu Afrika.
Cherries
Mcheri…tunda lenye faida nyingi ikiwemo kusaidia maradhi ya Jongo.
Cherry ambalo hupendwa sana na ndege, lina faida nyingi sana miongoni kusaidia kupambana na maradhi yanayosakama damu au mzungunguko wa maji mwilini kama Jongo. Jongo ni ugonjwa unatokana na aidha kurithi, kunywa sana pombe, nyama nyekundu, mayai, kutofanya mazoezi. Hujionyesha kwa maumivu makali katika goti moja au kidole gumba cha mguu. Cherry safi sana. Vichache katika kasha huanzia £2 (Shilingi 5,000).
Strawberry- Stroberi kiwastani huwa aghali. Msimu yanapopungua bei ni wakati wa baridi (Desemba-Machi) yanaposhuka toka shilingi 7,000 hadi 5,000. Bei hizi hufuatana na wapi unaishi, maduka makubw ana madogo , nk
Kawaida sehemu tunazoishi Watanzania , kama mitaa ya Mashariki ya London kuna unafuu wa bei za vyakula na matunda shauri wakazi wengi hapa pia ni Wahindi wenye maduka ya bei nafuu kuliko ya yale makubwa makubwa ya Kizungu.
Apricot
7. Matunda yote yenye mbegu dani (Berries) kama Cranberries, Blue Berries, Blackberries- siku hizi hupatikana katika juisi zinazotengenezwa bila sukari nyingi. Nadhani tatizo kubwa la nchi Afrika ni kutengeneza juisi za matunda zilizojaa maji na sukari zaidi kuliko matunda. Huu ni udanganyifu na uroho wa wafanyabiashara wetu. Shirikisho la Ulaya limekuwa makini miaka ya karibuni kuzuia tabia hiyo Uzunguni na kuweka mikakati mikali.
Strawberries
Stroberi (Strawberry) – tunda linalopatikana zadi Uzunguni- ambalo lina Vitamin C kwa wingi.
Kifupi haya ndiyo matunda ya aghali rahisi hapa London.
Bei rahisi ni ndizi mbivu (toka visiwa vya Carribbean – na zingatia Matoke ya Uganda ni aghali sana- kichani kimoja kinaanzia shilingi elfu saba!), matufaha (matunda rasmi ya Kizungu), machungwa na machenza, Kiwi (yale matunda ya kijani toka New Zealand), zabibu, mapea (pears ), mapera, nk
Sasa tuongelee faida za matunda nliyoyachagua kwa leo yaani Mapapai na Maparachichi.
Ni muhimu kuzingatia kwamba matunda yanatakiwa kuliwa yakiwa katika kitengo kimoja- yaani chachu (“acid”), asidi au alkali (“alkaline”). Matunda hayo ya chachu ni maembe, mananasi, machungwa, zabibu, Kiwi, nk; ambapo alkali ni matikiti maji, ndizi mbivu, tufaha, mapea, Strawberry nk.
Acids-Mango Oranges Kiwi
Matunda chachu (“asidi”) yanatakiwa yaliwe pamoja…
Mapapai na Maparachichi yanaangukia katika mkondo wa “alkali” na moja ya matunda yaliyowekwa katika Vyakula Vyenye Nguvu kuliko vyote (Superfoods) . Matunda hayo ni Machungwa , Kiwi, Papai, Parachichi. Vyakula hivi via faida sana mwilini.
Alkalines-Apples Pears Ndizi-FMacha
Mfano wa matunda yenye “alkali” yanayotakiwa kuliwa pamoja.
Faida zake ni zifuatazo.
1. Kinga maradhi na kinga magonjwa (Anti-Oxidant) ambazo husaidia kukinga na kupambana na takataka zinazotolewa na mwili au zinazotoka katika mazingira machafu.
2. Vitamin C. Vitamin hii ni muhimu sana mwilini. Ukosefu wa Vitamin C husababisha uchovu, kukosa usingizi, uvivu, kutokuwa na hamu ya kula. Kwa siku mtu mzima unatakiwa upate gramu 40 za Vitamin C. Kwa wavuta sigara zidisha mara mbili. Ukila matunda yenye Vitamin C unapata kinga ya majeraha mwilini (vidonda pona haraka), huboresha wajihi, haiba na “nafsi” ya ngozi, mifupa, meno na mzunguko mzima wa damu mwilini- hivyo kusaidia usingizi ( na kwa watoto kusaidia kukua vizuri).
Papai-1-pic by F Macha
3. Papai lina “papain” inayosaidia kuukinga mwili na kulainisha tumbo- ndiyo maana kama umevimbiwa au huendi haja kubwa sawasawa (“constipation”) ukila papai husaidia sana.
4. Mapapai na Maparachichi yana “Beta Carotene”(itokanayo na Vitamin A) inayopatikana pia katika nyanya, karote, maembe, mchicha (ambao haukupikwa hadi ukanyong’onyea), mbegu mbegu (mbichi si za kukaanga au kuwekwa chumvi- hadi zikakongoroka) kama hizi pichani chini karanga, mlozi, korosho, nk.
Mseto wa Mbegu Mbichi
Faida zake ni pamoja na kusaidia mizunguko ya umajimaji na damu mwilini, ngozi na nywele (safi sana kwa kina dada wanaojipenda), kupunguza mafuta katika damu (cholestoral) na “presha” – mambo yanayoua sana watu weusi duniani leo. Ukiwa upungufu wa “Beta Karotene” macho hayaoni vizuri, unaugua upesi upesi hasa maradhi ya mapafu (mafua, kikohozi,nk). Kwa wanawake waja wazito ni rahisi kupoteza watoto au kuzaa watoto ambao hawako sawasawa.
5. Maparachichi yanayo mafuta asilia. Mafuta haya ni mazuri SANA kuliko yale tunayoyapata katika nyama au vitu vilivyokaangwa, maana yanausaidia na haya haribu mwili. Makisio yake ni kalori 400 kwa parachichi moja. Hiyo ni nguvu kubwa sana. Ndiyo maana Parachichi (na Papai) huhesabiwa kama mfalme wa matunda.
Papai na Parachichi -nje
Lazima izingatiwe kuwa chakula, mmea au tunda lolote lenye rangi nzito iliyokolea kama parachichi huwa na faida MARIDHAWA mwilini.
Hivyo, kuanzia leo kama hukua ukithamini matunda haya mawili- kayatafute. Kuna watu wazima wanaosema eti matunda ni chakula cha watoto. Wanakosea. Mtu mzima anahitaji kuendelea kuukarabati mwili wake. Kwetu Afrika ni ya bei nafuu- wapo wengi wanaofika Ulaya na Marekani wanashindwa kuyala shauri bei yake si mchezo. Halafu wala si matamu kama ya nyumbani Afrika…
MATUNDA OYEE!

0 comments:

Post a Comment