Thursday 1 May 2014

MAMBO MUHIMU YA KUZINGATIA UNAPOTAKA KUFANYA MAZOEZI


Mazoezi yana umuhimu mkubwa kwa maisha yako endapo utaweza kuyafanya kwa jinsi ipasavyo. Kujua muda wa kula na kitu cha kula kunaweza kukusaidia kupata matokeo tofauti katika ufanyaji wako wa mazoezi.

Wanasayansi wanasema kuwa ulaji ni mazoezi ni vitu vinavyoenda bega kwa bega. Ni vizuri kuelewa chakula unachokula kinaathiri vipi mazoezi yako.
Baada ya kugundua hilo wataalamu hao waliona si vibaya ikiwa watakuja na mwongozo utakaowasaidia wafanyaji mazoezi kupata matokeo mazuri kwenye programu zao.
Unachotakiwa kuelewa  ni kwamba muda wako wa kufanya mazoezi unaendana na kiasi cha chakula na maji ulichopata.  Hii inawahusu hasa wale wanaotaka kupunguza uzito kwa kutumia mazoezi.
Watu walio katika kundi hili, wamekuwa wakiharibu maana nzima ya mazoezi kwani badala ya kula chakula kinachoweza kuwaongezea nishati katika ufanyaji wa mazoezi, wengi wao huamini kuwa kwa kuacha kula wanaweza kufanikiwa zaidi.
Mara nyingi kitendo cha kaacha kula na kuendelea na mazoezi huchangia kwa kiasi kikubwa kumfanya mtu husika akose nguvu na badala yake kudhoofika na hatimaye hushindwa kufanya mazoezi.
Mambo muhimu ya kuzingatia unapotaka kufanya mazoezi:
1.   -Pata kifungua kinywa sahihi kiafya
Ikiwa unafanya mazoezi asubuhi, unashauriwa kuamka mapema na kupata kifungua kinywa saa mbili kabla ya kuanza mazoezi. Kwani kwa wakati huo nishati yote uliyopata kwenye chakula cha usiku,      itakuwa imetumika usiku hivyo hadi kufikia muda huo, utakuwa una kiwango kidogo sana cha nishati na sukari katika damu pia itakuwa chini.
Ikiwa hutakula kabla ya kufanya mazoezi utajisikia mchovu. Ikiwa utaamua kula kabla ya mazoezi unashauriwa kula chakula chepesi kama vile juisi au hata matunda pamoja na maji ya kutosha. Unashauriwa kula chakula kitakachosaidia kukuongezea sukari katika damu.
Ikiwa wewe si mlaji wa asubuhi sana, jaribu kunywa hata juisi tu kabla ya kufanya mazoezi. Pia ikiwa utaweza kupata kikombe cha kahawa itakuwa ni sawa tu.
2.   -Zingatia kiasi cha chakula
Epuka kula chakula kizito kabla ya kuanza mazoezi kwani kwa kufanya hivyo unaweza kujiweka kwenye hatari ya kuongezeka zaidi badala ya kupungua au kuimarisha mwili wako.
Pia, kula kiasi kidogo cha chakula. Ikiwa utakula chakula kingi unaweza kusikia uvivu kufanya mazoezi na hivyo kuishia kupumzika badala ya kuchangamka kufanya mazoezi.

3.   -Vitafunwa vyenye virutubisho kiafya ni bora zaidi.
Unaposema kula kitafunwa haimaanishi kuwa kila kitafunwa ni sahihi, hapa unapaswa uwepo wa virutubisho muhimu katika kitafunwa husika. Wataalamu wa afya wanashauri ulaji wa matunda zaidi katika hili.
Matunda yanaweza kumweka mfanyaji mazoezi bila kumchosha hata kama atakuwa amekula kiasi kikubwa tofauti na vyakula vingine.
Ikiwa utaweza kupata mlo unaoendana na mazoezi yako, ni wazi kuwa  mazoezi yako yatakuwa yenye tija, kwani utaweza kuona tofauti.

0 comments:

Post a Comment