Saturday, 3 May 2014

LIPSTIKI, LIPSHINE ZENYE MADINI YA SUMU NI HATARI KWA AFYA YAKO

Wanawake hupenda kuonekana nadhifu siku zote na katika kufanya hivyo wanatumia vitu mbalimbali vikiwamo rangi za aina mbalimbali ambazo baadhi yake hupakwa katika miili yao ikiwamo midomo.

Rangi na mafuta ya midomo ambayo hutumiwa zaidi na wanawake yanaelezwa kuwa na sumu ambayo huweza kusababisha saratani ya mapafu, kushindwa kwa figo kufanya kazi na hata maumivu ya tumbo.
Utafiti uliochapishwa  Januari mwaka huu na Jarida la Sayansi ya Mazingira nchini Uingereza (JES) umebaini kuwa  matumizi ya muda mrefu ya rangi za midomo na ‘lipglosses’ yanaweza kusababisha maradhi kadhaa kutokana na kuwa na kiwango cha madini ya aluminiam, cadmium na risasi (lead).
Kemikali zinazopatikana zaidi katika rangi za midomo zinatajwa kuwa ni cadmium, chromium, titanium, lead na manganizi.



Ingawa bidhaa hasa zenye wingi wa madini hayo hazijawekwa wazi,wanasayansi hao wanasema kuwa ni zile zinazotumiwa au kupendwa zaidi na kinamama.
Imebainika kuwa kupaka ‘lipshine’ au ‘lipstick’ mara tatu na zaidi kwa siku kunaweza kusababisha maradhi hayo na ilishauriwa kuwa matumizi yake yasiwe ya muda mrefu.
Mkuu wa utafiti huu, Katharine Hammond, mwanasayansi wa mazingira na afya katika Chuo Kikuu cha California, 
Marekani   anasema nia ya utafiti huo ni kutaka kupima kiwango cha madini hayo ambacho mtumiaji wa lipstiki huweza kukimeza na kiwango kinachokubalika.
“Kiafya,  mtumiaji hatakiwi kunywa au kumeza zaidi ya asilimia 20 ya metali za lead au cadmonium hata katika maji tu ya kunywa,” anasema Hammond
Utafiti wa Hammond unaeleza kuwa bidhaa hizo zina kiwango kikubwa cha aluminium, cadmium, chromium na manganizi kilichozidi asilimia 20.
Hali ikoje nchini
Afisa Uhusiano wa Mamlaka ya Chakula na Madawa(TFDA) Gaudensia Simwanza anasema  madini ya Lead na Titanium yapo kwenye orodha ya mchanganyiko uliozuiwa.
“Lakini madini ya titanium dioxide ndiyo yanaruhusiwa na siyo titanium zote” anasema Simwanza
Anasema madini ya ‘Lead Acetate’ yasiyozidi asilimia 0.6 yanaruhusiwa katika rangi za nywele tu(Hair Dye).
“ Madini haya ni moja ya sehemu ya vipodozi ndiyo  imeangaliwa na kuelekeza kuwa si salama katika matumizi ya lipstiki:” anasema Simwanza
Daktari katika kitengo cha uchunguzi wa magonjwa cha Hospitali ya Taifa Muhimbili, Innocent Mosha anasema kwa kawaida madini ya Lead yanaathiri figo kwa kiasi kikubwa.
Mosha anasema kiasi kidogo tu cha madini hayo kikimezwa kwa muda mrefu, mtumiaji huana kuona dalili zisizo za kawaida katika mwili.
“Sijawahi kusikia utafiti wa hapa nchini uliowahi kuchunguza lipstiki au lipgloss, lakini kama ni kweli vipodozi hivyo vina madini hayo, badi ni ya hatari,” anasema Dk Mosha.
Wataalamu wa afya wanasema kuwa matumizi ya kudumu   ya Cadmium midomoni  yana uhusiano wa karibu na  uharibifu wa figo na mifupa.
Watafiti hao walisema mwanamke anapopaka urembo huo, madini yaliyotumika kuutengeneza huingia tumboni kidogokidogo na baada ya muda husababisha maradhi hayo.
Elizabeth Salter Green, Mkurugenzi wa Kampeni ya Bidhaa za Kemikali anasema kuna haja ya kuwa waangalifu katika 
matumizi ya kemikali zilizopo katika vipodozi hasa kwa wasichana wadogo ambao wapo katika umri wa kuzaa.
Anaongeza: “Lazima wasiwasi uwekwe. Vipimo na tafiti zaidi zifanyike katika vipodozi vyenye kemikali na athari zake’
Watafiti pia walibaini kuwepo kwa  kemikali ya lead kwa asilimia 75 ya bidhaa  za midomo. Nusu ya sampuli hizo 
ilionyesha kuwa lipstiki na ‘lipglosses’ zilikuwa na kemikali ya lead kwa kiwango kikubwa kuliko kile kinachokubaliwa na mamlaka ya chakula na madawa.
Utafiti mwingine ulibaini kuwa mwanamke mrembo ambaye hupaka lipstiki mara 3 kwa siku na kila mpako mmoja hubeba miligramu 10 za madini hayo,  huyo yupo hatarini.
Ilielezwa kuwa kiasi chote hicho humezwa kwa siku moja kila mwanamke anapopaka lipstiki.
Dk Kenneth Spaeth, Mkurugenzi wa Tiba ya Mazingira katika Hospitali ya North Shore, Manhasset anasema  kuwepo kwa madini ya ‘lead’ katika vipodozi kunaweza kuathiri ujauzito au watoto ambao wanachezea vipodozi vya mama zao.
Mwaka 2007, Kampeni ya Vipodozi Salama ya nchini Marekani iligundua madini ya lead kwa asilimia 61 katika vipodozi 33 vya lipstiki.
Mtaalamu wa masuala ya ngozi, Dk Isaack Maro anasema madini ya cadmonium yapo hata katika udongo na baadhi ya vyakula.
Anasema matumizi ya muda mrefu ya madini hayo huweza kusababisha maradhi.
“Cadmonium ni metali nzito ambazo si rahisi kuchujwa katika figo, zikikaa kwa muda mrefu katika figo, huweza kuziathiri” anasema Dk Maro.
Anasema hana uhakika iwapo madini ya lead yapo katika lipstiki kwani ni madini ya hatari sana kiafya.
“Miaka ya nyuma iliwahi kupigwa marufuku kutumika kutengenezea mabomba baada ya kubainika kuwa ni ya hatari” anasema
Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira (UNEP) linasema kuwa Lead ni metali za hali ya juu zenye sumu ambayo huweza kumuathiri binadamu kwa kuikaribia kidogo.
Madini ya lead yanatajwa kuwa na sumu inayoweza kusababisha matatizo ya neva za fahamu, moyo, renal, tumbo na mfumo wa uzazi.
UNEP inaeleza kuwa madini ya cadmium pia yana sumu ambayo inaweza kuathiri figo na mfumo wa mifupa.
Linda Loretz, mtaalamu wa kubaini vimelea vya sumu wa Baraza la Bidhaa za Vipodozi (PPC) alifanya utafiti pia na kusema kuwa hakuna ubishi kuwa liptiki na lipgloss zote humezwa.
Utafiti ulifanyika kwa wanawake 360 nchini Marekani ambao wanatumia lipstiki na ambao huipaka kwa mara mbili na zaidi.
“Kwa nini baada ya muda  lipstiki inafutika mdomoni . Inakwenda wapi? Unafikiri inayeyuka?” anahoji  Mtaalam huyo (Dk Loretz)

        Lipstiki zinatengenezwa kwa kutumia nini?
 
Mtandao wa Wikipedia unaeleza kuwa lipstiki inatengenezwa kwa kutumia ming’aro mbalimbali au waxi. Waxi yenye nguvu ijulikanayo kama Carnauba Wax inatumika kuifanya lipstiki iwe ngumu na isimegukemeguke.
 
Pia mafuta mbalimbali nayo hutumika kama mafuta ya karafuu, madini, cocoa,  lanolini na petroli.

Mtandao wa Wikipedia unaeleza kuwa asilimia 50 ya lipstiki zinazotengenezwa  marekani zinatumia  mafuta ya nguruwe au castor ambayo huipa mng’aro zaidi.

0 comments:

Post a Comment