Saturday, 17 May 2014

KUNA AINA 7 ZA UGONJWA WA KUSAHAU


1. Kusahau kwa muda mfupi (Transience)
Hii ni hali ya kusahau habari au matukio fulani yaliyopita.  Tatizo hilo humfanya mtu asahau habari  ambayo ameipata muda mfupi.  Hata hivyo, habari ambayo mtu atakuwa haihitaji kuitumia mara kwa mara ni rahisi kuisahau.  
Japokuwa hali ya kusahau mambo kwa muda mfupi inaweza kuonekana 

kama ni dalili ya udhaifu wa kumbukumbu, wanasayansi wa masuala ya akili huiona hali hiyo kuwa ni ya manufaa kwani huisafisha akili kwa kuondoa kumbukumbu ambazo hazitumiki na kuingiza kumbukumbu mpya na zenye manufaa.

2. Usahaulifu wa kutotilia maanani mambo (Absentmindedness)

Aina hii ya usahaulifu hutokea iwapo mtu hatilii maanani jambo fulani.  Mfano, unaweza kusahau ulipoweka kalamu yako kwa sababu hukuweka maanani mahali ulipoiweka.  Inawezekana ulikuwa unafikiria kitu kingine wakati unafanya hivyo,  au huenda ulikuwa hufikirii chochote ila akili yako haikuchukua kumbukumbu ya tendo ulilolifanya.  Usahaulifu huu pia ni pamoja na kusahau kufanya jambo fulani katika muda wake, kama vile kutumia dawa au kwenda kutimiza ahadi.

 3. Kutokumbuka mara moja (Blocking)
Mtu anaweza kukuuliza swali ambalo unalifahamu kabisa, lakini ukashindwa kulijibu mara moja kwa kutolikumbuka.  Huu huenda ni aina kubwa zaidi ya usahaulifu ambapo akili hushindwa kuifikia kumbukumbu mara moja.
Wanasayansi huamini kwamba usahaulifu huu ni kawaida kulingana na umri wa mtu unavyozidi kuongezeka .

Pia, usahaulifu huu huchangia kwa kiasi kikubwa kwa watu wenye umri mkubwa katika matatizo ya kukumbuka majina ya watu na vitu vingine.  Hata hivyo, utafiti umeonesha kwamba watu huweza kunasa nusu ya kumbukumbu zao katika kipindi cha dakika moja. 

4. Kumbukumbu potofu (Misattribution)
Kumbukumbu potofu hutokea wakati mtu anapokumbuka sehemu ya jambo kwa usahihi, lakini akakosea maelezo kadhaa kama vile wakati, mahali, au mtu husika.  Usahaulifu mwingine wa aina hii ni pale unapoamini kwamba dhana uliyokuwa nayo ni halisi wakati ukweli ni kwamba ilitokana na kusoma 

mahali  au kuisikia kwa watu wengine, lakini ukawa umesahau ukweli huo.
Aina hii ya usahaulifu iko zaidi katika wizi usiokusudiwa wa kazi za sanaa  ambapo mwandishi, kwa mfano, anaandika habari fulani akidhani ni ya kwake kumbe aliisoma mahali fulani.

Kuhusiana na matatizo mengine ya kupoteza kumbukumbu, kumbukumbu potofu huendana na umri.  Mtu anapozidi kuzeeka anakuwa anaingiza habari chache zaidi kwenye akili yake, kwani akili yake inakuwa haina uwezo wa kudaka habari kwa haraka.

5. Kudaka habari potofu (Suggestibility)
Kudaka habari potofu pia kunaathiri mfumo wa kumbukumbu, ambapo mtu huiweka habari hiyo katika akili yake akifahamu kwamba ni jambo la kweli wakati siyo kama alivyoliona wakati likitokea. Alidanganyika.

 6. Kumbukumbu iliyojenga dhana tayari (Bias)
Kumbukumbu ya mtu ambayo tayari imejenga dhana fulani inayotokana na mambo aliyoyaona, imani fulani, mambo ambayo ameyapa mwenyewe kipaumbele, itamletea matatizo.
Dhana ambayo tayari unayo kichwani ni dhahiri itaathiri mawazo yako, hivyo kila ukitaka kukumbuka jambo fulani mawazo yako na dhana zako ni lazima yatatawaliwa na habari ambayo unaikumbuka.
Lakini, pamoja na hali hii, wanasayansi hawajafanya utafiti mkubwa kuhusu dhana aliyo nayo mtu na jinsi inavyoweza kuathiri kumbukumbu zake, pia hawajafahamu vyema iwapo hali hiyo huenda sambamba na umri.

7. Kumbukumbu mbaya (Persistence)
Watu wengi husumbuliwa na tatizo la kusahau mambo kila wakati  lakini katika matukio mengine, kuna watu ambao huteseka kwa kuwa na kumbukumbu mbaya ambazo hutaka kuzisahau, lakini wanashindwa.

Kuendelea kwa kumbukumbu mbaya na zenye matukio yasiyopendeza au yenye kuleta hisia mbaya ni moja ya matatizo ya kumbukumbu.
Baadhi ya kumbukumbu hizi huonesha matukio ya kutisha na mengine  ambayo huwa ni ya kufikirika na hivyo  kuleta hisia mbaya.

Kumbukumbu hizi kwa watu wengi hutokana na matatizo ambayo waliyapata kama vile kudhalilishwa kijinsia au matukio waliyoyapata wakiwa vitani.

0 comments:

Post a Comment