WENGI
wetu tungependa kujua historia ya vidonge vya lishe au lishetiba au
Food Supplement kama inavyojulikana kitaalamu na nani aliyeanzisha
utaratibu huu duniani wa kukigeuza kidonge kuwa chakula.
Kabla
ya mwaka 1934 hakukuwepo lishetiba ya aina yoyote duniani kitu ambacho
kiliwafanya watu wa enzi hizo wapate wakati mgumu lilipokuja suala la
kuboresha afya zao pale palipokuwa na upungufu wa virutubisho mwilini.
Mwaka 1934 mwanasayansi aitwaye Carl Rehnborg alianzisha kampuni ya
Nutrilite kwa ajili ya kutengeneza lishetiba. Kampuni hii imeendelea
hadi leo na kuwa miongoni mwa makampuni makubwa ya kutengeneza
virutubisho duniani. Kampuni hii ndiyo inayotoa udhamini mkubwa kwa
timu ya mpira wa miguu maarufu nchini Italia ya A.C.Milan.
Haikuwa kazi ndogo kwa Rehnborg kufanikiwa kuanzisha kampuni hiyo,
bali yalikuwa ni matunda ya jitihada na tafiti mbalimbali za tangu mwaka
1920 wakati akiishi nchini China akiwa askari jeshi ambapo aligundua
kuwa kulikuwa na uhusiano mkubwa sana kati ya maradhi hasa yale sugu na
vyakula wanavyokula wanadamu.
Kikubwa kilichomshtua ni kuona kuwa jamii ya wakulima ambao walikula
matunda na mboga kwa wingi walikuwa na afya njema huku jamii ya watu
walioishi mijini ambako matumizi ya mafuta, sukari na chumvi ni makubwa,
walikuwa wakisumbuliwa na maradhi sugu mara kwa mara.
Carl alipata wazo la kuchanganya virutubisho alivyohisi kukosekana
katika vyakula walivyokuwa wakila jeshini. Alichanganya dawa za asili,
aina fulani za majani na mboga, chokaa na unga wa misumari (ili kupata
madini ya chuma), pamoja na unga wa mifupa (ili kupata madini ya
Calcium) na baadaye alikula mchanganyiko huo na baadhi ya wanajeshi
wenzake.
Japo ladha ya mchanganyiko huo haikuwa nzuri, lakini waliokula baada
ya muda mfupi walianza kunawiri na afya zao kuimarika tofauti na
waliokula chakula cha jeshi cha kawaida.
Baada ya miaka kadhaa, Car alirejea nchini Marekani na kuanzisha
maabara yake ndogo katika
Kisiwa cha Balboa ambapo baada ya miezi sita
tu akawa ameshafanya majaribio na kugundua lishetiba nyingi sana kwa
kutumia aina nyingi tofauti za mimea na wanyama.
Pia aligundua namna nyingi za kukausha na kuhifadhi bidhaa hizo bila
kuathiri ubora wake wa asili na alizalisha bidhaa za lishetiba kwa wingi
zenye vitamin, madini na tindikali mbalimbali kulingana
na mahitaji ya
mwili wa binadamu. Hadi leo kampuni yake ya Nutrilite ndiyo inaheshimika
sana duniani kama mwanzilishi wa lishetiba chini ya uongozi wa mwanaye
Dr. Sam Rehnborg.
Baadaye, kampuni nyingine nyingi zikaibuka ikiwemo kampuni kubwa
nchini Marekani iitwayo
Herbalife inayomdhamini mchezaji bora duniani
Christiano Ronaldo anayekipiga timu ya Real Madrid ya Hispania, inadaiwa
kuwa afya ya Ronaldo ni imara kutokana na kutumia virutubisho kwenye
mlo wake.
Nchini Tanzania lishetiba ni kitu kigeni kidogo na ndiyo maana siyo
rahisi kuzikuta lishetiba kila duka, hospitali au kwenye maduka ya dawa
pia hata sehemu zinakopatikana ni ghali sana kumudu watu wa kawaida.
Hata hivyo, kupitia safu hii, unaweza kujua aina mbali mbali za
tibalishe na mahali zinakopatikana kwa hapa nchini. Tunawasihi watu
wenye uwezo na ambao kwa njia moja au nyingine wameshindwa kupata na
kutumia matunda na mboga za majani badala yake watumie vidonge vya lishe
kulinda afya zao.
0 comments:
Post a Comment