Thursday, 1 May 2014

IFAHAMU TEKNOLOJIA MPYA YA KUBAINI CHANZO CHA KIFO


 
WAKATI mageuzi yakiendelea kwenye
ulimwengu wa sayansi na teknolojia,
wataalamu hawajalifumbia macho tatizo
la utata wa baadhi ya vifo.

Waliobobea katika eneo hilo la
kuchunguza maiti ili kubaini
kilichomsababishia mhusika mauti, sasa
wamekuja na mbinu mpya, ambapo si
lazima tena kumpasua marehemu kama
ilivyozoeleka. Kwa misingi hiyo, wale
watu wenye ‘nyoyo ndogo’ waliokuwa
wanajihisi vibaya marehemu wao
kupasuliwa, wengine kwa imani
kwamba kuna kitu kinatolewa huko,
sasa watapata pumziko walau kwa
upande huo.
Njia mpya sasa ni kuuangaza mwili kwa
mwanga wa kompyuta, wenyewe
wakiita CT Scanner, ili kuchunguza
kilichosababisha kifo. Njia hii inatumika
pia kubaini viungo vya mwili
vilivyovunjika, kuteguka au hata ikiwa
mtu ana aina fulani ya ugonjwa ambao
mashine husika inaweza kuubaini.
Pamoja na picha hiyo kupigwa maeneo
yanayotakiwa katika mwili wa
marehemu, tishu au ogani kwenye
shingo huchomwa kidogo tu ili
kufanikisha ufuatiliaji wa mishipa, na
kukamilisha uchunguzi huo.
Teknolojia
hiyo ya kisasa zaidi, wataalamu
wanasema, imeshafanywa mara kadhaa
na matokeo yake yamekuwa ya uhakika
kwa asilimia 80 kwenye kung’amua
chanzo cha kifo.
Hiyo ni hatua kubwa na muhimu
kwenye eneo hilo kwa madaktari, kwa
sababu itaondoa adha iliyokuwa
imezoeleka siku na miaka iliyopita, ya
kupasua mwili wa mhusika ili viungo
nyeti, si vya siri, vipate kukaguliwa na
hatimaye wataalamu wabaini
kilichosababisha kifo.
Uvumbuzi huo umefanywa na Chuo
Kikuu cha Leicester, kilichopo jijini
Leicester, Leicestershire nchini
Uingereza. Kiongozi wa wataalamu hao
ni Profesa Guy Rutty. Kwa ugunduzi huo,
ni wazi kwamba, walau kwa wakati ujao
katika hata nchi zote itakuwa rahisi
kupata uamuzi unaokubalika kuhusu
nani alifia wapi na kipi chanzo cha kifo
chake na huenda utata unaokumba vifo
vingi sasa ukafutika.
Utamaduni katika nchi nyingi, zikiwamo
Marekani na Uingereza, umekuwa ni
kwamba baada ya vifo polisi ndio
wanachunguza sababu zake, na hata
pakiwa na utata, korti husimamia, huku
ofisa anayechunguza vifo na kutoa vyeti
vyake (coroner) akisubiri tu kutoa taarifa
yake kama kubandika stempu kwenye
bahasha au kupiga muhuri kugusa
stempu na bahasha yake.
Ugunduzi huo bila shaka utabadili
taratibu, na si ajabu hata sheria na
kanuni zikabadilishwa, ili kuokoa muda
na kuondoa kutofautiana kati ya watu
kwenye masuala hayo yamekuwa
yakichukua muda mrefu na kuwaacha
ndugu katika majonzi kwa kufuatilia
mambo ya mpendwa wao, huku
ikijulikana wazi kwamba hatarejea
kwenye dunia hii, hata iweje.
Tayari Profesa Rutty ametunukiwa tuzo
na mamlaka husika, kwa sababu ya kazi
yake hiyo, aliyoianza muda mrefu
uliopita, akiipa jina ya ‘Operesheni
Tochi’. Wataalamu wanasema kwamba,
teknolojia hiyo mpya itatumika kwa
ufasaha katika kuchunguza sababu ya
vifo vya kawaida na vile visivyo vya
kawaida, iwe kwa mtu mmoja au hata
kwa wengi wanaokufa kwa wakati
mmoja.
Tena, teknolojia hii itakuwa habari
njema kwa watu walio kwenye makundi
ya kiimani, ambayo kwa miaka kadhaa
sasa, wamekuwa wakipinga upasuaji
wa wafu ili kubaini sababu ya vifo vyao.
Profesa Rutty na wasaidizi wake katika
mradi huo tayari wamechapisha mada
ya kazi yao kwenye jarida la kimataifa la
masuala ya afya liitwalo ‘International
Journal of Legal Medicine’.
Humo wameeleza teknolojia waliyotumia
kufikia mafanikio hayo na protokali
iliyofuatwa tangu kwa mtafiti mmoja
huru hadi mwisho, chini ya Taasisi ya
Taifa ya Utafiti wa Afya (NIHR) ya
Uingereza. Profesa Rutty aliye kwenye
kitengo cha utafiti wa saratani chuoni
Leicester, anasema kwamba utafiti huo
utasaidia sana na kubadili jinsi ya
kushughulikia maiti katika kipindi
kijacho.
Kwamba uchunguzi wa maiti si kitu cha
kawaida sana au kinachofuatiliwa kwa
karibu na watu wengi, na pia wapo
ambao wamekuwa wakichukia watu
wao, kwa maana ya ndugu, rafiki au
wana dini au itikadi moja kupasuliwa
baada ya kufariki dunia.
“Kabla ya utafiti huu, pasipo kutumia
angiografia, vifo vitokanavyo au
kuhusishwa na matatizo ya moyo
havikuweza kuchunguzwa na kupatiwa
sababu kwa uhakika kwa njia ya utafiti
(Post mortem) kwa CT Scan, kwa hiyo
tulihitaji kutafiti na kubaini mfumo
ambao ungetuwezesha kufanya hivyo,”
anasema, huku akifurahia kufanikiwa
kupata mfumo wenyewe.
Profesa Rutty alishirikiana na Profesa
Bruno Morgan na wengine kwenye
kitengo cha radiolojia, na wakabuni na
kufanikisha mfumo wa kumchoma
marehemu kidogo tu shingoni wakati
wa kuchukua picha hiyo kwa kompyuta
(scanning).
“Kuchoma huko husaidia kufuatilia moja
kwa moja mishipa ya moyo, ni teknolojia
isiyo ghali, rahisi kuifanya na yaweza
kutumiwa kwa aliyefariki dunia kwa kifo
cha kawaida na kisicho cha kawaida,
cha mtu mmoja au cha watu wengi,”
inasema taarifa ya Chuo Kikuu cha
Leicester kwa vyombo vya habari.
“Tulikuwa kitengo cha kwanza duniani,
kwa kutumia elimu yetu, kupendekeza
matumizi ya angiografia kama njia ya
kuepukana na aina zilizopitwa na wakati
za kutafiti chanzo cha vifo, na pia ni wa
kwanza kuweka bayana maendeleo
yake... makundi mengine yamefanya
angiografia ya mwili mzima ambayo
huchukua muda mrefu, ni ghali na si
rahisi kutekelezwa kwenye uchunguzi
wa kila siku katika Uingereza,” Profesa
Rutty anajigamba.
Mada nzima ya utafiti iliyowasilishwa na
kuchapwa, inaonesha matokeo ya
majaribio 24, huku timu nyngine ya
Chuo Kikuu ikipewa jukumu la kupitia
mengine 200, ili kupitia teknolojia
tuliyotumia na kujenga msingi mkubwa
zaidi wa ushahidi. Matokeo ya utafiti
huu hayakupokewa kimya kimya,
yalikuja na mwangwi kutoka kwa
wataalamu na wasio wataalamu
kadhalika.
Mmojawapo ni kutoka nchini Marekani.
Huko, Mohit Joshi, akiwa Washington,
makao ya serikali, akiliandikia jarida
liitwalo ‘International Journal of Legal
Medicine’, anasema wanasayansi wa
Uingereza wamegundua teknolojia
kubwa, lakini itakayotumiwa kirahisi.
Kwamba teknolojia hiyo ni mapinduzi
makubwa kwenye utafiti wa vifo na
itapunguza gharama za awali
zilizoingiwa na watu na taasisi
mbalimbali kubaini sababu za vifo.
Joshi, pia, anagusia kwamba ugunduzi
huo utatoa faraja kwa vikundi vya imani
visivyopenda maiti kupasuliwa.
Ilitarajiwa kwamba, England na Wales
zingepunguza haraka idadi ya utafiti wa
vifo kwa kutumia njia ya zamani, kwa
asilimia 60. Profesa Derrick Pounder
anasema kwamba kiwango cha utafiti
wa maiti 110,000 coroner kwa kila maiti
500,000 ni kikubwa, kwa hiyo kwa
kutumia teknolojia hiyo mpya itakuwa
rahisi.
Akiandika kwenye jarida la ‘Royal Society
of Medicine’, anasema kwamba katika
Scotland ni asilimia sita, ikilinganishwa
na 22 ya England na Wales. Hata hivyo,
Profesa Pounder anayetoka Chuo Kikuu
cha Dundee, anashangaa sababu ya
watu wengi kiasi hicho wanataka
kuchunguza sababu za vifo.
Haoni kwa nini, hufika mahali serikali
ikaingilia mambo ya kifamilia na kuagiza
uchunguzi wa maiti wengi kubaini
sababu za vifo vyao. “Japokuwa utafiti
wa ndani ni zana muhimu kwenye
uchunguzi wa kisasa wa sababu za vifo,
si sahihi kila kifo kukifanyia uchunguzi
kiasi hicho. maiti wachunguzwe pia
kwa kuangaliwa nje, ni gharama nafuu.
Kuwe na uwiano kati ya uchunguzi
unaoagizwa na serikali na ule wa ndugu
au wadau,” anasema.

0 comments:

Post a Comment