Saturday, 3 May 2014

HII NDIO ELIMU YA MSINGI YA CHAKULA NA LISHE


Umuhimu wa Chakula kwa Binadamu
Chakula na lishe bora ni muhimu kwa binadamu wote. Chakula ni kitu chochote
kinacholiwa na kuupatia mwili virutubishi; ambapo
lishe ni sayansi ya jinsi mwili
unavyokitumia chakula. Lishe inahusisha jinsi mwili unavyosaga na unavyoyeyusha
chakula na hatimaye virutubishi kusharabiwa (kufyonzwa) na kutumika mwilini.
 
 
Faida za chakula kwa binadamu:
 
- Kutengeneza seli za mwili na kurudishia seli zilizokufa au kuharibika
- Ukuaji wa akili na mwili
- Kuupa mwili nguvu, joto na uwezo wa kufanya kazi
- Kuupa mwili kinga dhidi ya maradhi mbalimbali.
 
Ulaji bora ambao unazingatia chakula mchanganyiko na cha kutosha ni muhimu kwa
binadamu wote, na ni muhimu zaidi kwa wagonjwa wakiwemo wale wanaoishi na virusi
vya UKIMWI au UKIMWI.
 
Inasisitizwa kula chakula mchanganyiko na cha kutosha mara zote kwani hakuna
chakula kimoja pekee ambacho kinaweza kumpatia binadamu mahitaji yake yote ya
 
kilishe isipokuwa maziwa ya mama tu kwa mtoto katika kipindi cha miezi sita ya
mwanzo.
 
Ulaji bora ambao unazingatia chakula mchanganyiko na cha kutosha ni muhimu kwa
binadamu wote, na ni muhimu zaidi kwa wagonjwa wakiwemo wale wanaoishi na virusi
vya UKIMWI au UKIMWI.
 
Inasisitizwa kula chakula mchanganyiko na cha kutosha mara zote kwani hakuna
chakula kimoja pekee ambacho kinaweza kumpatia binadamu mahitaji yake yote ya
 
kilishe isipokuwa maziwa ya mama tu kwa mtoto katika kipindi cha miezi sita ya mwanzo.
 
Virutubishi, umuhimu na vyanzo vyake
Virutubishi ni viini vya kikemia vilivyoko kwenye vyakula ambavyo mwili hutumia ili
 
kufanya kazi mbalimbali. Karibu vyakula vyote vina virutubishi zaidi ya kimoja ila kwa
 
kiasi tofauti. Vyakula vingine huwa na virutubishi vya aina fulani kwa wingi zaidi. Kila
 
kirutubishi kina kazi yake katika mwili wa binadamu, na vingi hutegemeana ili kufanya
kazi vizuri mwilini. Zifuatazo ni aina za virutubishi:
·       Kabohaidreti
·       Protini
·       Mafuta
·       Vitamini
·    Madini
Kabohaidreti
 
Hiki ni kirutubishi muhimu kwa kuupa mwili nishati (nguvu) kwa ajili ya kufanya kazi
mbalimbali pamoja na joto. Kabohaidreti ndio inayochukua sehemu kubwa ya mlo.
  Kabohaidreti inajumuisha wanga, sukari na nyuzinyuzi.
 
Vyakula vyenye kabohaidreti
kwa wingi ni pamoja na mahindi, mchele, uwele, ngano, viazi vya aina zote, mihogo, ndizi, sukari na baadhi ya matunda. Nyuzinyuzi ni muhimu sana katika uyeyushwaji wa chakula.
 
Protini
Protini ni muhimu sana kwa ukuaji wa mwili na akili. Protini husaidia mwili
kutengeneza seli mpya, kutengeneza vimeng’enyo mbalimbali na wakati mwingine
protini huupa mwili nishati kwa ajili ya matumizi mbalimbali.
 
Baadhi ya vyanzo vizuri
vya protini ni aina zote za nyama, samaki, aina za mikunde kama choroko, kunde,
maharagwe, soya, karanga, pia maziwa, mayai, dagaa na wadudu wa aina mbalimbali
wanaoliwa kama kumbikumbi, senene, n.k.

Mafuta
Mafuta huhitajika mwilini kwa ajili ya kuupa mwili nguvu na joto pamoja na kusaidia
usharabu wa baadhi ya vitamini. Mafuta pia hulainisha chakula na kukifanya kiwe na
ladha nzuri, na hivyo kumfanya mlaji ale chakula cha kutosha.
 
Mafuta hupatikana kwa
wingi kwenye samli, siagi, baadhi ya nyama, baadhi ya samaki, mbegu zitoazo mafuta
kama ufuta, korosho, mbegu za maboga, karanga, alizeti, mbegu za pamba, kweme,
mawese pamoja na nazi.

 
Vitamini
Vitamini zinahitajika mwilini kwa ajili ya kulinda mwili pamoja na kuufanya mwili
ufanye kazi zake za umetaboli vizuri. Vitamini ziko za aina nyingi na zinapatikana kwa
 
wingi kwenye mboga-mboga, matunda na kwenye vyakula vinavyotokana na wanyama
kama maziwa, aina zote za nyama, mayai, dagaa, samaki, n.k.
 
Madini
Madini kama ilivyo vitamini hulinda mwili na kuufanya ufanye kazi zake za umetaboli
vizuri. Kuna aina nyingi za madini, na baadhi ya vyakula vyenye madini kwa wingi ni
pamoja na vyakula vinavyotokana na wanyama, dagaa, samaki, mboga-mboga na
matunda.
 
KUMBUKA
 
Vyakula huwa na kirutubishi zaidi ya kimoja, hivyo vyakula vinavyotajwa
kwenye kirutubishi fulani humaanisha vyakula hivyo vina
kirutubishi hicho kwa wingi.
 
Makundi ya vyakula na mlo kamili
Pamoja na kuzungumzia virutubishi mbalimbali, ni muhimu kukumbuka kwamba mtu
anapokula hafikirii virutubishi bali chakula. Hivyo ni muhimu katika kujifunza ulaji
 
bora, kutumia makundi ya vyakula badala ya aina za virutubishi. Pia ni muhimu
kukumbuka kwamba vyakula vingi vina virutubishi zaidi ya kimoja, na pia kiasi hutofautiana.

Kwa afya na lishe bora, inashauriwa kula mlo kamili (chakula mchanganyiko). Mlo
kamili hutokana na vyakula ambavyo vimewekwa pamoja kwa namna ambayo vikiliwa
 
pamoja huupatia mwili virutubishi vyote muhimu kwa afya bora. Hutayarishwa
kutokana na mchanganyiko wa angalau chakula kimoja kutoka katika kila kundi, katika
makundi yafuatayo:
 
Vyakula vya nafaka, mizizi na ndizi:
Vyakula hivi ndivyo vinavyochukua sehemu kubwa ya mlo na kwa kawaida ndiyo
vyakula vikuu. Vyakula katika kundi hili ni pamoja na mahindi, mchele, mtama, ulezi,
 
ngano, uwele, viazi vikuu, viazi vitamu, mihogo, magimbi, viazi mviringo na ndizi.
 
• Vyakula vya mikunde na vyenye asili ya wanyama:
Vyakula vilivyoko katika kundi hili ni pamoja na maharagwe, njegere, kunde, karanga,
soya, njugu mawe, dengu, choroko na fiwi. Vile vyenye asili ya wanyama ni pamoja na
 
nyama, samaki, dagaa, maziwa, mayai, jibini, maini, figo, senene, nzige, kumbikumbi na
wadudu wengine wanaoliwa.
 
• Mboga-mboga:
Kundi hili linajumuisha aina zote za mboga za majani zinazoliwa, zile zinazolimwa na
zinazoota zenyewe. Mboga-mboga ni pamoja na mchicha, majani ya maboga, kisamvu,
 
majani ya kunde, matembele, spinachi, mnafu, mchunga, pia aina nyingine za mboga
 
kama karoti, pilipili hoho, biringanya, matango, maboga, nyanya chungu na bamia,
bitiruti, kabichi na figiri.

 
Matunda:
Kundi hili linajumuisha matunda ya aina zote kama mapapai, maembe, mapera,
malimau, mapesheni, mananasi, peasi, machungwa, machenza, zambarau, mafenesi,
 
mastafeli, mabungo, pichesi, topetope. Aidha “matunda pori” yana ubora sawa na
 
matunda mengine. Matunda hayo ni kama ubuyu, ukwaju, embe ng’ong’o, mikoche,
n.k.

 
• Mafuta na sukari:
Mafuta na sukari ni muhimu ingawa vinahitajika kwa kiasi kidogo mwilini. Mafuta
 
yanaweza kupatikana kutoka kwenye mimea kama mbegu za alizeti, ufuta, karanga,
 
mawese, mbegu za pamba n.k na kutoka kwa wanyama kama siagi, samli na nyama ya
mafuta. Sukari inapatikana kwenye sukari, miwa, asali na vyakula ambavyo
vinatengenezwa kwa sukari nyingi kama jamu.
 
 
Kumbuka;
  Maji
 
Maji kwa kawaida hayahesabiwi kama kundi la chakula, lakini yana umuhimu mkubwa katika afya na lishe ya binadamu.
 
Inapaswa kunywa maji ya kutosha, angalau lita moja na nusu (glasi nane) kwa siku au hata zaidi. Inashauriwa kunywa maji zaidi wakati wa joto kali ili kuzuia upungufu wa maji mwilini.
 
Vilevile unaweza kuongeza maji mwilini kwa kunywa vinywaji kama supu, madafu, juisi za matunda
mbalimbali.

Mtu anatakiwa kula mchanganyiko wa vyakula kwenye mlo mmoja kwa sababu
hakuna chakula kimoja chenye virutubishi vyote muhimu kwa ajili ya lishe na afya
 
bora. Vilevile baadhi ya virutubishi hutegemeana ili kuweza kufanikisha kazi zake
mwilini. Kwa mfano madini ya chuma yanayopatikana kwenye vyakula vya mimea
 
kama mboga-mboga za kijani husharabiwa vizuri mwilini kama kuna vitamini C
ambayo hupatikana kwa wingi kwenye matunda. Mfano mwingine ni zile vitamini
kama A, D, E, K ambazo usharabu na utumikaji wake mwilini hutegemea kuwepo
 
kwa mafuta. Vilevile nishati huweza kutumika vizuri mwilini iwapo kuna aina za vitamini B kwenye vyakula.
 
HIVYO;
Kwa mtu yeyote ni muhimu kula mlo ulio kamili angalau mara mbili au tatu kwa siku
na asusa (vitafunwa) kati ya mlo mmoja na mwingine.
 
KUMBUKA
Katika jamii zetu, matumizi ya mboga-mboga na matunda yamesahaulika
sana. Inabidi kusisitiza umuhimu wa kuhakikisha kwamba mboga-mboga na matunda vinakuwa sehemu ya mlo.

0 comments:

Post a Comment