Friday 20 May 2016

UTAFITI WA-TANZANIA WENGI WANAUMWA NA MARADHI YA BAWASIRI




WA-TANZANIA WENGI WANAUMWA NA MARADHI YA BAWASIRI


UGONJWA BAWASIRI

Ni ugonjwa usiofahamika na hata baadhi ya wanaougua huwa hawachukui hatua

Bawasiri ni tatizo linalosababishwa na kuvimba, kutuna na kutokeza nje kwa mishipa ya damu iliyoko katika njia ya haja kubwa.

Tatizo hili mara nyingi huambatana na damu kuganda ndani ya mishipa ya vena iliyoko katika njia ya haja kubwa. Katika baadhi ya maeneo katika ukanda wa Nyanda za Juu Kusini, bawasiri hujulikana kwa jina la makila.

Baadhi ya dalili za ugonjwa wa bawasiri ni kinyesi kunuka harufu ya damu wakati wa kujisaidia, hisia za maumivu wakati wa kujisaidia haja kubwa, kijiuvimbe katika eneo la tundu la haja kubwa, muwasho wa ngozi katika tundu la njia ya haja kubwa na kujitokeza kwa kinyama (bawasiri) wakati wa kujisaidia haja kubwa.

Dalili nyingine ni kutokwa na matone ya damu mpya au nyeusi wakati wa kujisaidia haja kubwa.

Hata hivyo, utafiti ulioongozwa na Dk S. Riss wa Chuo Kikuu cha Tiba cha Vienna nchini Austria na kuchapishwa mwaka 2012 katika Jarida la Afya la Kimataifa kuhusu Matatizo ya Utumbo, toleo la 27(2), ulibainisha kuwa idadi kubwa ya watu wanaougua maradhi haya hasa yanapokuwa katika hatua ya daraja la kwanza ama bawasiri ya ndani. Wakati huu hawapati usumbufu wala maumivu yoyote.

Ingawa ni vigumu kupata takwimu sahihi za tatizo hili hapa nchini kutokana na watu wengi kutibiwa na wataalamu wa tiba za jadi au kushindwa kwenda kutibiwa hospitalini kwa sababu ya kuona aibu, takwimu kadhaa zinaonyesha kuwa kutokana na mtindo wa maisha na kile kinachoitwa ustaarabu wa kisasa, tatizo hili huwaathiri Watanzania wengi, hasa watu wazima.

Wataalamu wa takwimu za makadirio wa Taasisi ya Right Diagnosis, kwa kutumia takwimu za nchi nyingine duniani, wanakadiria kuwa Tanzania inaweza kuwa na wagonjwa wa bawasiri wapatao milioni 1.4.

Baadhi ya wachunguzi wa maswala ya takwimu za afya wanakadiria kuwa, karibu asilimia 50 ya idadi ya watu wazima wenye umri wa miaka 50 na kuendelea, wanakabiliwa na tatizo hili au wamewahi kupata maradhi haya katika kipindi fulani cha uhai wao.

Matokeo ya utafiti wa Dk R.J. Davies uliochapishwa mwaka 2006 katika jarida la Clinical Evidence toleo la 15 na ulibainisha kuwa watu milioni 10 wa jinsi zote nchini Marekani, walikuwa na maradhi ya bawasiri.

Chanzo cha bawasiri

Kimsingi tatizo la bawasiri pamoja na mambo mengine, hutokana na mtindo wa maisha usiofaa. Bawasiri huwapata mara kwa mara watu wasiopendelea kula matunda, mboga za majani pamoja na vyakula vyenye nyuzi lishe kwa vingi. Watu wengine wanaopata tatizo hili ni wale wanaopendelea kula maandazi, kaukau, bisukuti, vyakula vilivyokobolewa kama ugali wa sembe, chips zenye mafuta mengi pamoja na vinywaji vyenye kafeini kwa wingi.

Tabia nyingine inayochangia kutokea kwa tatizo hili kwa kiwango kikubwa ni kutokunywa maji ya kutosha. Matokeo yake watu wenye mtindo huu wa maisha, hupata kinyesi kigumu na kutumia nguvu nyingi wakati wa kujisaidia haja kubwa. Jambo ambao huongeza hatari ya kupata maradhi ya bawasiri.

Wakati wataalamu wa afya wanapendekeza kunywa maji mengi kiasi cha mililita 50 kwa kila kilo moja ya uzito wa mwili kwa siku au bilauri (glass) 12 kwa siku, sawa na mililita 185 kwa kila saa kwa muda wa saa 16 ambazo mtu anakuwa macho, ni vigumu kwa Watanzania wengi kunywa maji kiasi hicho. Wengi hawafikishi hata bilauli nne kwa siku.

Tabia nyingine hatarishi ni matumizi ya kiasi kikubwa cha pombe. Watu wanaokunywa kiasi kikubwa cha pombe zaidi ya chupa moja ya bia pamoja na kutumia kiasi kikubwa cha chumvi, wanakabiliwa na hatari ya kupoteza maji mengi kutoka mwilini kwa njia ya mkojo na kujiweka katika hatari ya kupata ukavu wa kinyesi.

Wale wasiofanya mazoezi mepesi ya mwili kila siku, angalau kwa dakika 20 kama vile kutembea au kukimbia taratibu, nao wanakabiliwa na hatari ya kupata maradhi ya bawasiri.

Hii ni kutokana na ukweli wa kisayansi kuwa misuli yao katika njia ya haja kubwa (puru) huwa dhaifu na kuruhusu mishipa kuvimba, kutuna na kutokeza nje kwa urahisi wakati wanapotumia nguvu nyingi kusukuma kinyesi kikavu ili kitoke nje wakati wa kujisaidia haja kubwa.

Nani wako hatarini?

Bawasiri pia huwapata zaidi wajawazito, watu wenye unene kupita kiasi, wale wanaofanya mazoezi mazito ya kunyanyua vitu vyenye uzito mkubwa kupita kiasi na wale wanaofanya mambo yanayoongeza shinikizo katika utumbo mpana kama vile kujisaidia haja kubwa ukiwa umekaa, kuharisha kwa muda wa siku nyingi pamoja na kukaa muda mrefu mahali pamoja.

Matatizo yanayoweza kujitokeza kutokana na bawasiri ni pamoja na upungufu wa damu mwilini, kujifunga kwa bawasiri, uambukizo wa bakteria katika misuli inayozunguka njia ya haja kubwa, matundu ya fistula na kushuka kwa misuli ya njia ya haja kubwa.

Ni vizuri kuonana na daktari mara unapohisi au kuona dalili za bawasiri ili kupata tiba stahiki na sahihi kabla ya kupata madhara zaidi. Kumbuka huu ni ugonjwa kama magonjwa mengine na hakuna haja ya kuona aibu na kushindwa kumweleza mtaalamu wa afya kuhusu bawasiri.

Kupima afya mara kwa mara kutasaidia kugundua tatizo kama ya bawasiri mapema na kuchukua hatua mapema. Matibabu ya mape ni njia rahisi ya matibabu kabla ya kusababisha madhara makubwa.

Kama wahenga wasemavyo, kinga ni bora kuliko kuponya. Ili kujikinga dhidi ya maradhi haya, inashauriwa kuboresha mtindo wa maisha ya kila siku kwa kufanya mazoezi mepesi, kula mlo kamili na kuepuka vinywaji na vyakula vyenye sukari nyingi na vileo.

1 comments:

  1. Thanks for this. I really like what you've posted here and wish you the best of luck with this blog and thanks for sharing. Loose Leaf Tea

    ReplyDelete