Repoti mpya ya Shirika la Chakula la Umoja wa Mataifa (FAO),
limetoa taarifa hivi karibuni ikiwahimiza watu duniani kula wadudu kwa
wingi kwani ni miongoni mwa vyakula bora, kutokana na kuwa na kiasi
kingi cha virutubisho bora vya mwili.
Wadudu ni chanzo kikubwa cha protini, mafuta mazuri kiafya, madini na
kamba lishe. Aidha, wadudu wameelezwa kuwa ni rafiki wa mazingira na ni
rahisi kuwafuga au kuwakamata.
Inakadiriwa na shirika hilo kuwa
kiasi cha watu bilioni 2 duniani wanatumia wadudu kama sehemu ya milo
yao ya kila siku. Imeshauriwa watu kupendelea kula wadudu kutokana na
ukweli kwamba protini inayopatikana kwenye wadudu hao ni bora zaidi
kuliko ile inayopatikana kwenye nyama ya kuku, ng’ombe, nguruwe na
samaki.
Mbali ya wadudu kuwa ni chanzo kikuu cha protini na mafuta
mazuri kama ya samaki (fish oil), lakini pia ni chanzo kizuri cha madini
ya kashiamu (calcium), chuma (iron), seleniamu (selenium), zinki (zinc)
na Vitamini B.
Kumbikumbi.
WADUDU WA TANZANIA
Kuna aina zaidi ya elfu tisa ya wadudu
wanaoliwa sehemu mbalimbali duniani. Lakini kwa nchini Tanzania, kuna
aina kuu mbili za wadudu ambao wanajulikana na kutumiwa kama sehemu ya
kitoweo katika familia nyingi nchini, hasa vijijini.
Aina hizo mbili
maarufu nchini Tanzania ni Senene na Kumbikumbi, ambao hupatikana kwa
wingi zaidi nyakati za masika sehemu za vijijini. Senene na Kumbikumbi
ni miongoni mwa vyakula vyenye faida nyingi mwilini na ni vitamu pia.
Kutokana na kuwa na faida nyingi za kiafya mwilini, ndiyo maana
wamekuwa wakiliwa tangu enzi na enzi na mababu zetu. Ingawa idadi kubwa
ya wadudu hao wanaoliwa hupatikana kwa kuwakamata kwenye makazi yao
porini, lakini katika siku za hivi karibuni, mifumo ya kisasa ya
kuwakamata wadudu hao imebuniwa na hivyo kurahisisha ukusanyaji kwa
idadi kubwa na kwa mara moja.
Kwa kuona umuhimu na faida za kiafya
zinazoweza kupatikana kwa kula wadudu, Shirika la Chakula la Umoja wa
Mataifa limetoa wito kwa nchi zote duniani kufuga wadudu hao kwa wingi
kibiashara, shirika linaamini nchi nyingi zikitilia mkazo suala hili,
zinaweza kupunguza tatizo la njaa kwa kiasi kikubwa na wakati huo huo
kuboresha afya za watu wengi.
Bila shaka hii ni habari njema na ya
kutia moyo kwa watu ambao tayari wanafuga na kuvuna Senene kibiashara,
kama ambavyo tunavyoona wakiuzwa baadhi ya sehemu za mijini. Nitoe wito
kwa watu wengine ambao hawajawahi kuonja Senene au Kumbikumbi kufanya
hivyo, kwani siyo tu wana faida kiafya mwilini, bali ni watamu sana. (so
delicious)!
0 comments:
Post a Comment