Tuesday 16 December 2014

UGONJWA WA KWENYE MFUMO WA UZAZI WA MWANAMKE (PELVIC INFLAMATORY DISEASES)



MAAMBUKIZI ugonjwa wa kwenye mfumo wa uzazi wa mwanamke (Pelvic Inflamatory Diseases)  ambao pia hujulikana kama shingo ya uzazi (kitaalamu huitwa cervix) ambayo hujulikana kwa jina la cervicitis hutesa sana wanawake wengi wenye umri mbalimbali.
Maambukizi hayo husambaa hadi kwenye mfuko wa uzazi (endometrium) ambayo kitaalamu huitwa endometritis na mirija ya uzazi (fallopian tubes) hali ijulikanayo kitabibu kama salpingitis.
Ugonjwa huu husababishwa na vimelea vya jamii ya Neisseria Gonorrhoeae pamoja na Chlamydia Trachomatis ndivyo vinavyosababisha ugonjwa huu kwa akina mama na wataalamu huuita Pelvic Inflamatory Diseases (PID) yanayotokea kwenye mfumo wa uzazi wa mwanamke.
Kuna njia kadhaa ambazo mwanamke anaweza kuambukizwa ugonjwa huu, njia hizo ni pamoja na kufanya ngono isiyo salama, maambukizi ya njia ya uzazi hasa baada ya kujifungua.
Wanawake wanaotoa mimba kwa njia zisizo salama, wana uwezekano wa kupata maambukizi au wale ambao mimba hutoka (miscarriage) au wakipewa damu iliyo na vimelea vya maambukizi.
Dalili za ugonjwa huu
Dalili za ugonjwa huu wa PID ni nyingi kama vile mwanamke kuhisi maumivu ya tumbo hasa maeneo ya chini ya kitovu, kupata maumivu ya mgongo au mwanamke kutokwa na uchafu wenye harufu sehemu za siri.
Kuna dalili nyingine kama vile kuhisi maumivu wakati wa kukojoa au wakati wa tendo la ndoa. Kutoka damu bila mpangilio wakati wa hedhi na mgonjwa kuwa na homa na kuhisi kichefuchefu au kutapika.
Mwanamke aliyeambukizwa maradhi haya ya maambukizi, anaweza kufanya vipimo  kwa kuchunguza mkojo ili kufahamu kama mgonjwa ana mimba.
 Mkojo huchunguzwa na darubini ili kutambua aina za vimelea vinavyomletea mgonjwa maambukizi.
Kuna kipimo kiitwacho kitaalamu Full Blood Picture hutumika ili kujua aina mbalimbali za chembe za damu zilivyoathiriwa na maambukizi hayo au kama kuna mwingiliano na magonjwa mengine yaliyojificha.
Daktari anaweza kujua kama mgonjwa ana maradhi haya kwa kuchukua utando unaozunguka shingo ya uzazi na kuuotesha kwa ajili ya utambuzi wa aina za vimelea viletavyo maambukizi hayo. Kipimo hiki huitwa cervical culture.
Mgonjwa pia anaweza kufanya vipimo vingine ili kujua kama ana maambukizi ya magonjwa yatokanayo na kujamiiana, kama vile virusi vya ukimwi na kisonono. Mgonjwa pia anaweza kufanyiwa ultrasound ya nyonga ili kuangalia kama kuna athari yoyote katika mfumo wake wa uzazi.
Matibabu
Mara mgonjwa anapogunduliwa kuwa ana magonjwa hayo, atatibiwa na dawa za jamii ya antibayotiki ili kuua vimelea vya ugonjwa.
Dawa za maradhi haya zipo nyingi kama vile Cefoxitin pamoja na Doxycycline, Cefotetan na Doxycycline; Clindamycin pamoja na Gentamycin; Ampicillin nakadhalika. Tunashauri kuwa dawa hizi zinunuliwe kwa kushauriwa na daktari.
Ushauri
Kuna njia kadhaa zinazoshauriwa kuzuia maambukizi katika mfumo wa uzazi kama vile kufanya ngono salama kwa kutumia kondomu au kujizuia kabisa kufanya ngono, kuwahi kuwaona wataalamu wa afya mara dalili za ugonjwa huu zinapoanza kujitokeza na kupimwa vipimo vya maambukizi ya magonjwa yanayosambazwa kwa njia ya ngono (STI).

0 comments:

Post a Comment