Monday 3 November 2014

JINSI YA KUJIKINGA NA KUONDOA HARUFU MBAYA MDOMONI!


WATU wengi husumbuliwa na tatizo la kunuka mdomo bila hata kujijua hivyo kuwa kero kwa wenzao na wakati mwingine hujishushia hadhi mbele ya jamii. Mara nyingi ugonjwa wa kunuka mdomo (Halitosis) husababishwa na uchafu wa kinywa na ulaji wa vyakula usiosahihi lakini ni tatizo linalotibika.
Ni rahisi kulizuia na kuliondoa tatizo la kunuka mdomo iwapo utaamua kufuata kanuni za usafi wa kinywa na unywaji wa maji kwa kufuata kwa makini muongozo ufuatao:
KUPIGA MSWAKI
Kitu cha kwanza kufanya ni kupiga mswaki kwa ukamilifu kila uamkapo asubuhi. Wakati wa kupiga mswaki, utatakiwa siyo tu kusugua meno, bali pia ulimi, sehemu ya katikati hadi karibu na koromeo kwa kusugua vizuri.
Vile vile kila uamkapo baada ya kulala mchana au jioni, hakikisha unapiga mswaki, kwani bakteria wa kinywani, hutawala kinywa kila ulalapo. Mara baada ya kupiga mswaki na kusugua ulimi sawaswa, hakikisha unasukutua vizuri kwa maji, kwani hapa ndipo baadhi ya watu hukosea kwa kupiga mswaki bila kusukutua kwa maji.
KUNYWA MAJI MENGI
Maji ni muhimu sana karibu kila eneo la mwili wa binadamu. Unywaji wa maji ya kutosha kila siku utakusaidia kudhibiti na hatimaye kuondoa tatizo la kunuka mdomo. Unywaji wa maji mengi ni muhimu, hasa kwa wale watu wenye ugonjwa wa kukauka midomo (xerostomia).
Mara nyingi harufu itokayo mdomoni, hutokea tumboni na siyo kinywaji peke yake kama unavyoweza kudhani. Hivyo, kama tumbo litakuwa chafu, hata kama utasafisha kinywa vizuri bado harufu mbaya inaweza kuendelea kutoka.
Harufu mbaya ya tumboni hutokea pale tumbo linapokuwa chafu kutokana na kutopata choo kwa muda mrefu. Miongoni mwa mambo yanayochangia kukosekana kwa choo kwa muda mrefu ni pamoja na tabia ya kutokunywa maji ya kutosha kwa siku, hivyo hakikisha unakunywa maji, kiasi kisichopungua 

lita moja na nusu hadi mbili au zaidi, kutegemeana na kazi unazozifanya.
Ukiwa na tatizo la kukaukiwa maji mwilini kila mara, mwili hujaribu kutumia njia zake za kiasili kupunguza uzalishaji wa mate ili kuhifadhi maji kwa ajiili ya matumizi mengine, kitendo hicho huchangia kunukisha mdomo kwa sababu ndani ya mate huwa kuna kinga muhimu dhidi ya baktetria wanaonukisha kinywa.
Kwa upande mwingine, ili kuzuia kinywa kunuka pale mdomo unapokuwa umekaukiwa na mate, ni vizuri kutafuna vitu kama bazooka au ‘chewing gum‘ yoyote ili kuzalisha mate ambayo huhitajika katika kudhibiti bakteria.
Mwisho, hakikisha unasukutua sawaswa baada ya kula chakula chochote, hata kama ni juisi isipokuwa unapokunywa maji tu ya kawaida. Bila shaka, ukizingatia haya, tatizo ulilonalo la kunuka mdomo litataoweka na kubaki historia.

1 comments: