Saturday 18 October 2014

HALI HALISI KUHUSU UGONJWA WA KANSA TANZANIA.



Saratani  imewekwa katika kundi la magonjwa ya hatari kwa uhai wa watu yanayoundwa na mkusanyiko wa magonjwa 100 duniani, Tanzania ikiwamo.


Mengine ni Ukimwi, kipindupindu na malaria, kwa mujibu wa mabingwa wa matibabu ya saratani ya watoto katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) wanasema ugonjwa huo pia unawakumba
watu wenye umri mkubwa.


Hali ya ugonjwa huo inaelezwa kuwa ni tete, kati ya wagonjwa 40,000 wanaokwenda kutibiwa kwenye hospitali maalumu, asilimia
80 wanafariki dunia.

Ukubwa wa tatizo hilo umesababisha wagonjwa kutibiwa bure katika hospitali chache zilizotengwa, japokuwa hospitali hizo hazina dawa za kutosha.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, jijini Dar es Salaam,  anasema tafiti zinaonyesha kwamba, kati ya wanawake 10, 000 wanaokwenda hospitalini kwa ajili ya matibabu ya saratani ya shingo ya uzazi, wanaobahatika kupona ni 1,000. Anasema aina hiyo ya saratani inaenezwa na aina ya kirusi kwa njia ya kujamiiana kwa zaidi ya asilimia 90 na kwamba wanaoathirika ziadi ni wanawake wenye umri kati ya miaka 20 na 40.

Saratani kwa rika la watoto:

Bingwa wa magonjwa ya watoto katika hospitali hiyo anasema,
saratani inasababishwa na ukuaji wa kasi wa seli usiodhibitika mwilini. Seli hizo huzaliana kwa kasi isiyo ya kawaida huku zikikua bila mpangilio kwa kujirundika eneo moja kwenye maeneo tofauti ya mwili.

Seli hizo zinaonekana kama  hazifi, yaani immortal na kwamba
zinapokuwa zinarundikana eneo moja, hukua na kutengeneza aina tofauti za vivimbe, yaani tumors.


Tabia hiyo ya seli, huibua aina mbali mbali za saratani, kwa mfano vivimbe vikikua shingoni, husababisha saratani ya tezi ya shingo, vinabadilika na kusambaa kulingana na sehemu hiyo ya mwili ilivyo.

Wataalamu wa afya wanasema kuna zaidi ya aina 100 za saratani huku kila aina ikiwa katika kiwango chake cha ukubwa kulingana na jinsi kila moja ilivyokuwa imeathiriwa katika hatua za mwanzo.

Hata hivyo, kwa upande wa saratani  ya damu yaani leukemia, mambo ni tofauti kwani aina hii huzuia  mzunguko wa kawaida wa damu kutokana na seli hizo kujizalisha kwa kiwango kikubwa kisicho
cha kawaida na kisichoweza kudhibitiwa. Vivimbe hivyo huweza kukua na kuathiri kazi za seli hai za mwili ambazo ni seli hai nyeupe, seli hai nyekundu na chembe hai sahani na hivyo kufanya mwili kukosa ulinzi,
hatimaye unashindwa kufanya kazi.


Pia vivimbe hivyo vya saratani (kansa), huathiri mifumo ya uyeyushaji chakula, fahamu  na pia kuzalisha homoni ambazo baadaye huathiri utendaji wa mwili kwa ujumla.
Siyo kansa zote ni za uvimbe, kwani zimegawanyika katika makundi ambayo ni solid tumor, na  liquid/ fluid tumor ambayo mara nyingi huhusisha ile ya damu.

Baadhi ya aina za kansa ambazo zipo katika kundi la solid tumor ni pamoja na zile za kwenye figo, macho, yaani retinoblastoma, ini, misuli, ubongo  na kwenye tezi , ijulikanayo kama lymphoma, kitaalam.

Hizo ndizo zinazoonekana kwa sehemu kubwa katika mazingira mengi nchini huku ile  ya damu ikiongoza kwa  sehemu kubwa.

Hali ya wagonjwa wa saratani MNH:
kwa wastani kwa mwezi hospitalini hapo wanapokea watoto wapya takribani 57 wenye matatizo ya kansa. karibu wagonjwa 250 wanaofika kwenye kliniki ya hospitali hiyo kila mwezi, lakini idadi ya wagonjwa ambao ni watoto wanaofika hospitalini kwa matibabu  ni karibu 1, 000 kwa mwaka.

kwa mfano mwaka uliopita idadi ya watoto wenye matatizo ya kansa waliofika hospitalini hapo kwa ajili ya matibabu ilikuwa takribani 800. Kati ya hao, chini ya 50 wanafika hospitalini kwa ajili ya kufuatilia matibabu,  huku 100 hadi 200 wanakuwa wanaendelea na matibabu.
Changamoto ya dawa:
Changamoto kubwa za hospitali katika kukabiliana na ugonjwa wa kansa kwa watoto hospitalini ni pamoja na uhaba wa dawa.

Mbali na wagonjwa wa saratani kutibiwa bure, lakini dawa hazipo za kutosha. Kuna baadhi ya dawa ambazo hazipo kwenye fungu la kutolewa  bure na wafadhili kwa kuwa ni za gharama kubwa na hivyo kuwalazimu wagonjwa kwenda kujinunulia kwa fedha zao wenyewe.

Mfano, sindano moja ya dawa kwa siku ni Sh.100, 000 na katika matibabu yake mgonjwa hutakiwa kudungwa sindano 24 ili kukamilisha dozi na kumfanya alipie jumla ya Sh.2, 400, 000.
Hizo ndizo wanazotakiwa kulipia. Kwa mujibu wa Madaktari bingwa, ukubwa wa gharama ya dawa hizo umesababisha wananchi wengi wa kawaida kushindwa kulipia matibabu.


Mbali na kutobainisha  takwimu sahihi za wagonjwa wanaobahatika kupona,  uchunguzi wa maradhi unaotakiwa kuendelea huchukua muda mrefu.

Muda wa matibabu kwa watoto wenye matatizo ya kansa hutofautiana
kulingana na jinsia, kwa mtoto wa kike huchukua muda wa miaka miwili na wa kiume miaka mitatu, kansa ya damu ndiyo inayotumia muda mrefu kutibika.

Hawezi kujua kwa haraka ni kiasi gani cha wagonjwa wa kansa wanaokuja hospitalini walioponywa kabisa, hii ni kwa sababu watoto wengi wanaoendelea kutibiwa huwa kwenye mchakato wa uchunguzi wa miaka kumi ili waweze kujiridhisha iwapo ugonjwa huo unaweza
kutibika, kujirudia au la. Matibabu mengine ya kansa huweza kuanzia muda wa miezi sita na kuendelea kulingana na hali ya ugonjwa kwa mgonjwa.

Tatizo la dawa bado ni kubwa Mahospitalini kwani kati ya aina nne za dawa ambazo wanapaswa kupewa kwa ajili ya kukamilisha dozi ya mgonjwa wa saratani, Wengi wao wanapewa aina mbili tu. Mbali na hizo, kuna dawa maalumu kwa ajili ya saratani kwa watoto na magonjwa mengine, kwani wengine hupoteza maisha yao kutokana na baadhi ya magonjwa kama vile Malaria na Neumonia.

Changamoto nyingine ni uhaba  wa watoa huduma, hata wale wachache waliopo hawana utaalamu wa kutosha kuhusu saratani ya watoto, kwa mujibu wa Dk  Namala katika hospital ya MHN.

Wodi za saratani:
MNH inakabiliwa na changamoto nyingine ambayo ni idadi kubwa ya wagonjwa kuliko uwezo wa wodi zilizopo. Kwa mujibu wa Madaktari, siku zingine wanakuwa na wagonjwa wengi kuliko vitanda kutokana na uhaba wa wodi na hivyo kusababisha baadhi yao kulazwa sakafuni.

Kwa siku wanaweza kupokea wagonjwa takribani 74 hadi 90 kwa vitanda 21 na kuwafanya wao kuwa katika wakati mgumu. Kibaya zaidi, mbali na changamoto hiyo, kwa sasa wanatarajia kuwahamisha wagonjwa kutoka katika wodi iliyokuwa na uwezo wa kuchukua vitanda 74 na kuwapeleka kwenye ile yanye uwezo wa vitanda 47. Anasema vituo kwa ajili ya wagonjwa wa saratani nchini havitoshelezi kwani mbali na kuwapo hospitali zingine, lakini maalumu kwa watoto ni MNH pekee.
Baadhi ya hospitali chache zinazotegemewa kwa ajili ya matibabu ya kansa (siyo watoto) ni pamoja na KCMC, Taasisi ya Saratani ya Ocean Road na Hospitali ya Rufaa ya Mbeya. Uhaba wa hospitali za huduma hizo, unasababisha wananchi wengi, hasa wa kawaida kupoteza maisha, wengi wao wakiwa ni wale wanaokwenda kwenye hospitali hizo wakiwa watu wazima, wanafariki dunia.

Kwa mfano kati ya wagonjwa 40, 000 wanaofika kwenye vituo hivyo kwa ajili ya matibabu, asilimia 80 wanafariki dunia kutokana na kuchelewa kupata huduma ya matibabu.

Wale wenye uwezo wa kwenda nje ya nchi kwa ajili ya matibabu, kwa mtu mzima hulazimika kugharimia Sh. milioni 15.Sambamba na hilo, wanawake wamekuwa ndiyo waathirika wakubwa kwa ugonjwa huo ambao hauchagui jinsia wala rika.

Kwa mfano, takwimu zinaonyesha kwamba, kati ya wanawake wagonjwa 10,000 wanaokwenda hospitali kwa ajili ya matibabu ya saratani ya shingo ya kizazi, ni 1, 000 tu ndiyo wanaobahatika kupona kwa mwaka.

Bajeti haikidhi Kuhusu bajeti, Dk. Namala, anasema, hospitali hiyo haina fungu la moja kwa moja, bajeti ikija kwanza hupitia wizarani,
nayo hugawiwa kwa vituo kulingana na maeneo, na mchakato unaofanyika ni ule wa kuagiza dawa kutoka Bohari ya Dawa ya Taifa (MSD).

Bila hatua za kuboresha huduma ya tiba ya saratani, hasa kwa upande wa gharama za matibabu, idadi ya wananchi wanaopoteza maisha kwa ugonjwa huo itaendelea kuongezeka kila mwaka badala ya kupungua” Anasema Dk.  Namala.

0 comments:

Post a Comment