Saturday, 27 September 2014

ATHARI ZA KASWENDE KWA WAJAWAZITO


Kama tulivyoeleza wiki iliyopita ugonjwa wa kaswende husababishwa na bakteria aina ya Treponema Pallidum.
Leo tutazungumzia maambukizi ya kaswende wakati wa ujauzito.
Mjamzito aliyeambukizwa kaswende hupata madhara mengi kama vile kujifungua kiumbe ambacho tayari kimeshakufa na mtoto kuathirika na ugonjwa huu wakati wa kuzaliwa.
Madhara mengine ni mtoto kupata matatizo wakati wa ukuaji wake, degedege na kuongezeka kwa vifo vya watoto wachanga.
Asilimia 30 ya mimba zinazoathiriwa na kaswende huishia watoto kufariki dunia wakati wa kuzaliwa au kupata matatizo ya ukuaji, degedege na kuongezeka vifo vya watoto kwa asilimia 50.
Taasisi ya Kudhibiti Ugonjwa wa Ukimwi nchini (NACP) katika ripoti yake ya utafiti uliofanywa chini ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii nchini hapa imesema maambukizi yote ya kaswende wakati wa ujauzito Tanzania Bara kati ya mwaka 2003 hadi 2004, yaliongezeka kwa wastani wa asilimia 6.7.
Magonjwa ya Ukimwi na kaswende mara nyingi huambatana pamoja.
Pia ugonjwa wa kaswende huongeza uwezekano wa mtu kupata maambukizi ya Ukimwi.
Kaswende inavyoambukizwa 
Ugonjwa huu unaambukizwa kwa njia ya kujamiiana bila kutumia kinga (ngono zembe) dhidi ya mtu mwenye ugonjwa huo.
Njia nyingine ni mwanamke aliyeambukizwa ugonjwa huo wakati wa ujauzito anaweza kumuambukiza mtoto wake.
Pia huambukizwa kupitia michubuko au mipasuko kwenye ngozi wakati wa kufanya ngono zembe.
Unaweza kuambukizwa kaswende wakati unapogusana na mtu mwenye ugonjwa huo, ikiwa wote wawili mna michubuko kwenye sehemu mbalimbali za ngozi.
Siyo rahisi mtu kutambua kama ana michubuko katika ngozi, kwani mingine huwa midogo sana isipokuwa ile inayoweza kuonekana kwa macho.
Dalili za kaswende
Dalili na viashiria vya kaswende hutegemea aina ya ugonjwa wenyewe.
Kuna aina tano za ugonjwa wa kaswende ambazo ni; kaswende ya awali (Primary syphilis), kaswende ya pili (Secondary syphillis), kaswende iliyojificha (Latent  syphilis), kaswende ya baadaye (Tertiary syphilis) na kaswende ya kurithi (Congenital syphilis).
Kaswende ya awali 
Dalili za kaswende ya awali ni kutokea kwa kidonda kidogo cha mviringo katika sehemu ambayo bakteria wameingilia na hutokea kati ya siku 10 hadi miezi mitatu (kwa kawaida kuanzia wiki 2 hadi 6), baada ya mtu kupata maambukizi hayo.
Kidonda hiki kinaweza kutokea kwenye sehemu ya haja kubwa, shingo ya kizazi kwa wanawake, mdomoni, kwenye uume, ulimi, vulva, tupu ya mwanamke na sehemu nyinginezo mwilini.
Tezi ambazo zipo karibu na sehemu iliyotokea kidonda hiki kawaida huwa zinavimba baada ya siku saba hadi 10.
Kidonda hiki hakiambatani na maumivu. Na kwa kuwa kinaweza kutokea katika sehemu zilizojificha kama kwenye shingo ya kizazi, sio rahisi mtu kutambua kama ana aina hii ya kaswende.
Kidonda hiki kinaweza kuwepo kwa muda wa wiki tatu hadi sita kama mtu hatapata matibabu, na hutoweka chenyewe bila tiba au baada ya kupata tiba.
Kaswende ya aina ya pili 
Shirika la Idhaa ya Kiswahili ya Redio Tehran la nchini Iran, linasema robo tatu ya watu ambao hawapati tiba, huishia kuingia kwenye kundi la kaswende ya aina ya pili yaani Secondary syphilis.
Aina hii hutokea wiki 4 hadi 10 baada ya mtu kupata kaswende ya awali. Dalili za aina hii ya kaswende ni vipele ambavyo haviwashi katika viganja vya mikono au nyayo za miguu.
Inaelezwa na wanasayansi kwamba vipele hivi pia vinaweza kutokea mwili mzima au sehemu mbalimbali za mwili, na muathirika huhisi uchovu, kuumwa kichwa, homa, kunyofoka  nywele, vidonda vya koo, kuvimba kwa matezi mwili mzima, maumivu ya mifupa na kupungua uzito.
Kaswende ya aina hii hujitokeza kwa wiki kadhaa, na hutoweka hata bila kupata tiba kwa mtu aliyeathirika.
Pia inaweza kujirudia rudia katika kipindi cha mwaka mmoja hadi miwili na mtu huingia kwenye kundi la aina ya tatu ya ugonjwa wa kaswende, yaani baada ya miaka miwili.
Kaswende iliyojificha
Aina hii inajulikana kama kaswende ambayo inaweza kuthibitika tu kwa kutumia vipimo vya maabara. Imegawanyika katika makundi mawili. Kundi la kwanza ni kaswende iliyojificha ya awali na kundi la pili ni kaswende iliyojificha ya kuchelewa.
Kaswende iliyojificha ya awali hutokea ndani ya kipindi cha mwaka mmoja baada ya muathirika kuugua
aina ya pili.
Aina hii huwa na dalili zinazojirudia kama za kaswende ya pili.
Kaswende iliyojificha ya kuchelewa hutokea baada ya mwaka mmoja wa kuugua kaswende ya aina ya pili.
Wakati wa kuugua aina hii ya kaswende, muathirika huwa hana dalili wala viashiria vyovyote vile na uwezo wake wa kuambukiza mtu mwingine huwa chini au hawezi kabisa kumuambukiza ugonjwa huu mtu mwingine.
Kaswende ya baadaye
Asilimia 30 ya wagonjwa wa kaswende ambao hawakupata tiba hapo awali huingia kwenye kundi hili na hutokea miaka 15 hadi 30 baada ya maambukizi ya kaswende.
Aina hii inaweza kuathiri viungo kama macho, ubongo, mishipa ya fahamu, viunganishi vya mifupa, uti wa mgongo, moyo na mishipa ya damu.
Kwa ajili hiyo aina hii ya kaswende ni yenye madhara makubwa kwani huweza kusababisha upofu, magonjwa ya moyo, magonjwa ya akili na magonjwa ya mishipa ya fahamu.
Huweza pia kumsababisha mtu kuwa kiziwi na kupungukiwa na kumbukumbu na hata kumsababishia kifo. Pia aina ya ugonjwa huu unaweza kuathiri mfumo wa chakula, mfumo wa kupumua na mfumo wa uzazi.
Kaswende ya kurithi
Aina hii ya ugonjwa huu hutokea wakati wa ujauzito au baada ya mtoto kuzaliwa.
Nusu ya wototo wanaozaliwa huwa hawaonyeshi dalili zozote za ugonjwa huu.
Nusu ya watoto wenye maambukizi ya kaswende hufariki dunia muda mfupi kabla ya kuzaliwa au baada ya kuzaliwa.
Dalili za ugonjwa huu kwa mtoto mchanga zinaweza kutokea baada ya kuzaliwa au wiki mbili hadi miezi mitatu baada ya kuzaliwa.
Dalili hizo ni kutoongezeka uzito au kushindwa kukua, homa, kukasirika haraka, kutochongoka kwa pua yaani pua inakuwa bapa, vipele kwenye viganja vya mikono na kwenye nyayo ambavyo huwa ni vya rangi ya madini ya shaba kwenye uso, viganja vya mikono na nyayo na vipele kwenye mdomo, sehemu za siri na sehemu ya haja kubwa.
Dalili nyingine ni kutokwa na majimaji puani, kuongezeka ukubwa wa ini na bandama, ngozi kuwa ya njano na upungufu wa damu mwilini.
Kwa mujibu wa tafiti za kidunia zilizofanywa na wanasayansi, dalili nyingine ni kutokwa vidonda vya rangi ya kijivu kwenye sehemu ya haja kubwa na kwenye tupu ya mwanamke, ngozi kuwa na mabaka meusi kwenye mdomo, sehemu za siri na sehemu za haja kubwa, maumivu kwenye mikono na miguu na pia kuvimba mifupa.
Dalili za ugonjwa wa kaswende kwa mtoto ni kuathirika meno, maumivu ya mifupa, kupata upofu, kupungua uwezo wa kusikia au mtoto kuwa kiziwi na kuwa na ukungu kwenye mboni za macho.
Matibabu
 Ni bora daktari kufanya uchunguzi wa damu kwani majimaji ya ukeni au uumeni huenda uchunguzi wake usionyeshe viini vya kaswende.
Kaswende ni hatari, kama haitibiwi, inaweza kusababisha utasa au ugumba, na hata kuathiri moyo, mishipa ya damu, ngozi ya mwili, mifupa na hata ubongo na kurukwa na akili.
Hata hivyo, matibabu yake ni rahisi – Zipo dawa aina  ya antibayotiki (zinazoua vijidudu) zinazoweza kutibu kaswende kabisa.
Ushauri
Ili kuzuia kuenea kwa maradhi hayo ni vyema mpenzio nae pia atibiwe.
Lakini pia ni lazima serikali ipeleke elimu na tahadhari kwa jamii namna ya kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huu. Elimu itolewe katika mihadhara na majukwaa ya kisiasa, bungeni, kwenye semina na makongamano na maeneo ya kuabudia.

0 comments:

Post a Comment