Saturday, 27 September 2014

AFYA: SUMU HUATHIRI WAUME,WATOTO WA WANAWAKE WANAOTUMIA MIKOROGO




“Tunafanya kampeni ya kupambana na vipodozi vyenye sumu kwa sababu tatizo ni kubwa nchini.“Hadi sasa asilimia 52 ya Watanzania hutumia mkorogo. matokeo yake wengi wameathirika na wanashindwa kuacha.” Euphrasia Shayo

KWA UFUPI


  • Kuna watu ambao hujitoa mhanga kwa vipodozi vilivyopigwa marufuku ilimradi wanaamini wakivitumia wanapendeza zaidi mbele ya macho ya watu na kupendwa.



Nuru Masoud, mkazi wa Kinondoni jijini Dar es Salaam, amekuwa akijishughulisha na biashara za vipodozi vya asili, maarufu kama mkorogo.
Hata hivyo, biashara hiyo aliisitisha mwaka 2013 baada ya kupata madhara makubwa ya ngozi ambayo yaliambukiza pia familia yake.
“Nilianza kuwashwa ngozi mfululizo, nikadhani nimeathirika na Ukimwi,” anasema akikumbuka jinsi ugonjwa huo ulivyomtesa.
“Niliamua kwenda Hospitali ya Muhimbili kwa daktari wa ngozi ambaye alichukua kipande cha ngozi yangu na kwenda kuipima na kubaini tatizo ni mkorogo.”
Nuru anasema alipewa dawa aina ya scaboma ambayo ilimsaidia na inaendelea kumsaidia hadi sasa. Kwa sasa ameachana na biashara hiyo na badala yake anatoa ushuhuda wa madhara ya dawa hizi.
Akizungumzia biashara hiyo, Nuru anasema licha ya kusitisha biashara iliyokuwa ikimpa fedha za kujikimu kimaisha, sasa amekuwa balozi wa kueleza madhara ya mkorogo kwa jamii.
Alianza biashara hiyo mwaka 1998 baada ya kufanya majaribio ya kupaka losheni hizo na kuona zinampendeza na watu wanazipenda na hivyo akawa anachanganya na kuuza.
“Kwa kipimo kimoja nilikuwa nauza kati ya Sh25,000 hadi 30,000 na ningeweza kupata hadi Sh400,000 kwa mwezi,” anasema.
Hata hivyo, mwaka 2013, mambo yalianza kwenda vibaya baada ya kujikuta akiwashwa ngozi na kuharibika ikawa kavu, yenye mikunjo na kubadilika rangi.
Licha ya Serikali kupambana na utengenezaji na matumizi ya vipodozi vyenye sumu, imeelezwa kuwa zaidi ya nusu ya Watanzania hutumia vipodozi hivyo kwa lengo la kuongeza urembo.
Utafiti uliofanywa na Taasisi ya Evirocare ya Dar es Salaam mwaka 2013 umeonyesha bado tatizo hilo ni kubwa.
Utafiti huo ulifanyika kwa kuhusisha mkoa mmoja katika kanda sita nchini. Mikoa hiyo ni Dar es Salaam ukiwakilisha Kanda ya Mashariki, Mbeya (Kanda ya Nyanda za Juu Kusini), Tanga (Kanda ya Kaskazini) na Dodoma (Kanda ya Kati).

Katika utafiti huo ambao watu 785,000 walihojiwa, asilimia 46.77 (asilimia 66 kati yao ni wanawake) walikiri kumiliki maduka ya vipodozi huku asilimia 27.38 walikuwa waajiriwa kwenye maduka hayo.

Utafiti huo pia umeonyesha kuwa maduka mengi ya vipodozi yako kwenye wilaya za Tanga (maduka 28), Ilala–Dar es Salaam maduka 27, Dodoma 23, Mbeya 22 na Kondoa maduka 20.

“Wilaya za Kinondoni na Temeke za Dar es Salaam zina maduka mengi lakini hazikuweza kuifikia wilaya ya Kondoa. Uwepo wa maduka mengi humaanisha kuwa hata watumiaji pia ni wengi japo ubora wa vipodozi katika mgawanyo na upatikanaji unatofautiana kati ya mtumiaji mmoja hadi mwingine,” inasema sehemu ya utafiti huo.

Kuhusu uelewa wa watumiaji ilionekana kuwa asilimia 57.4 wanatumia kujipodoa uso, asilimia 30 wanaona kama kitu cha kujipaka mwilini na asilimia 12.6 wanaona kuwa inaimarisha mwonekano wa ngozi.

Vipodozi vinavyouzwa zaidi

Walipoulizwa kuhusu vipodozi vinavyouzwa zaidi, watu 118 walisema ni losheni, 44 walisema mafuta ya nywele, 38 vipodozi vinavyobadilisha nywele, 37 mafuta ya mwili, 26 walisema krimu na 19 walisema manukato.

Wakati matumizi ya losheni yakiwa juu kwa watu wengi hivyo kuwaweka hatarini watumiaji hao, uchanganyaji wa manukato nao unaelezwa kuwa na athari zaidi kwani huweza kuumba kemikali nyingine kutokana na zile zilizochanganywa jambo linaloweza kuzalisha usugu wa matibabu.

“Matumizi ya losheni pia yanaiweka ngozi kwenye nafasi kubwa ya kuathirika na kemikali hasa kama mtumiaji atapaka vipodozi vilivyopigwa marufuku vya Carolite na Extra light.”

Waliopo hatarini zaidi

Kati ya idadi ya watu wanaotumia kwa wingi vipodozi sumu, imeonekana kuwa asilimia 67.6 ni wanawake.

“Kwa wanawake kutumia zaidi vipodozi hivyo, inamaanisha kuwa wengi wako kwenye hatari ya kuathirika.

“Kwa mfano kuna rangi za midomo, kama mwanamke atambusu au kugusana mara kwa mara na mwanaume, wote wawili wataathirika,” unaeleza utafiti huo.

“Watoto wanaoathirika zaidi ni wale wanaonyonyeshwa na wanawake wanaotumia mkorogo.”

Wengi hawajui madhara yake

Walipoulizwa kuhusu aina ya kemikali zilizomo kwenye vipodozi wanavyotumia, asilimia 62.4 ya watu 263 walisema hawajui huku asilimia 34 wakisema wanajua.

Unasema pia nusu ya wauzaji walisema hawajui kemikali zitumiwazo katika vipodozi wanavyouza, achilia mbali madhara yatokanayo na vipodozi, hivyo kipaumbele chao ni kupata faida kuliko afya za watumiaji.

Akizungumzia utafiti huo, meneja mradi wa kupambana na vipodozi vyenye sumu, Euphrasia Shayo anasema hali ni mbaya kwa Tanzania ndiyo maana Envirocare wameanzisha kampeni ya kupambana na vipodozi hivyo.

“Tunafanya kampeni ya kupambana na vipodozi vyenye sumu kwa sababu tatizo ni kubwa nchini. Hadi sasa asilimia 52 ya Watanzania hutumia kati ya Sh35,000 hadi 50,000 kwa mwezi kununua mkorogo. matokeo yake wengi wameathirika na wanashindwa kuacha,” anasema Euphrasia na kuongeza:

“Kichocheo kikubwa ni wanaume ambao huwashawishi wanawake watumie ili wawapende. Tunatoa elimu kwa wanawake kujiamini na uzuri walionao na kutumia vipodozi visivyo na sumu.”

Madhara ya vipodozi

Akizungumzia madhara ya vipodozi hivyo, Shayo anasema kwa kiasi kikubwa cha mikorogo husababisha saratani ya ngozi na kupunguza nguvu za kiume.

Madhara haya pia huwaathiri wale ambao wenzi wao wanatumia vipodozi vyenye viambata vya sumu.

“Kwa mtu aliyeathirika na matumizi ya mkorogo inabidi atumie dawa kwa miaka mitatu mfululizo huku akipewa ushauri wa kitaalamu.

Siyo rahisi kuacha kwani kwa siku mtu hutumia hadi dawa tisa, hivyo itabidi kuacha moja baada ya nyingine, vinginevyo ataharibika kabisa mwili wake,” anasema.

Ofisa Habari wa Taasisi ya Chakula na Dawa (TFDA), Gaudencia Simwanza anasema wamekuwa wakishirikiana na wadau kama Envirocare kupambana na tatizo la matumizi ya vipodozi vyenye sumu.

Anasema TFDA vile viel, imekuwa ikifuatilia na kukamata vipodozi vyenye sumu vinavyoingizwa nchini mbali na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu athari zake.

Ametaja baadhi ya viambata vya sumu vinavyotumika katika miongopni mwa vipodozi walivyovipiga marufuku ni pamoja na Bithionol, Hexachlorophene, zebaki, Vinylchloride, Zirconium, Halogenated salicylanilides (di-,tri-metabromsalan na tetrachlorosalicynilide), Chloroquinone na viambata vyake, Steroid, Chlofluorocarbon za kupuliza na Methyelene chloride.

0 comments:

Post a Comment