Friday 1 August 2014

TATIZO LA KUTOPATA UJAUZITO


TUNAPOSEMA tatizo la kutopata ujauzito ina maana mume na mke au watu walio katika uhusiano wa kutafuta ujauzito ndani ya mwaka mmoja lakini wameshindwa. Inaweza ikawa zaidi ya mwaka mmoja lakini wastani kiwango cha chini ni mwaka mmoja.
Ni tatizo kubwa katika jamii kwani kila mmoja anataka afikie malengo ya kuwa na familia.  Mwanamke na mwanaume wote wanahusika katika tatizo hili, mara nyingi imeonekana ni tatizo la mwanamke.
CHANZO CHA TATIZO
Kutokushika ujauzito kwa muda mrefu ni ugumba au ‘infertility’. Mwanamke au mwanaume anaweza kuwa mgumba. Ugumba umegawanyika katika maeneo makuu mawili, kwanza ni ‘Primary Infertility’ ambapo mtu hana historia ya kuwa na mimba wala mwanaume hana historia ya kumpa mwanamke mimba.
Ugumba wa aina ya pili ni ‘Secondary infertility’ ambapo mwanamke anayo historia ya kuwahi kupata ujauzito, haijalishi kama alizaa au mimba ilitoka na mwanaume anayo historia ya kumpa mwanamke mimba pia haijalishi kama mtoto alizaliwa au mimba ilitoka.
TATIZO KWA MWANAUME
Tatizo la kutoweza kumpa mimba mwanamke linaweza kusababishwa na mwanaume kukosa nguvu za kiume hivyo kushindwa kufanya tendo la ndoa, hali hii ya kukosa nguvu inaweza kusababishwa na matatizo mbalimbali kwani yenyewe siyo ugonjwa.
Kwa hiyo kitu cha msingi siyo kuongeza nguvu bali ni kufanya uchunguzi kuona tatizo ni nini na kulipatia ufumbuzi.
Tatizo lingine kwa mwanaume ni kutotoa mbegu za kiume au kutoa mbegu zisizo na ubora. Hii ni baada ya kupimwa kipimo cha mbegu za kiume, mbegu zinaweza zisizalishwe au zikazalishwa pasipo na ubora unaostahili kurutubisha yai la mwanamke.
Matatizo mbalimbali yanaweza kuathiri uzalishaji wa mbegu za kiume kama uvutaji wa sigara, unywaji wa pombe kali, maumivu ya korodani na utumiaji wa madawa ya kulevya kama mirungi na bangi.
Mazingira ya joto kali katika korodani pia huathiri uzalishaji. Tatizo hili na lile la upungufu wa nguvu za kiume tutakuja kuyaona kwa undani katika matoleo yajayo.
Kutokufahamu mzunguko wa hedhi wa mwanamke na kipindi gani unaweza kumpa mimba pia ni changamoto katika tatizo hili kwa upande wa mwanaume.
UFUMBUZI KWA MWANAUME
Wanaume wengi huwa wagumu kufanya uchunguzi kuona kama wana tatizo au la, siyo kila unapoweza kufanya tendo la ndoa na kutoa manii kwamba huna tatizo, unaweza kutoa mbegu zisizo na ubora. 
Vilevile kuwa na historia ya kumpa mwanamke mimba au kuwa na mtoto au watoto siyo kigezo cha kutokuwa na tatizo. Unaweza kuwa na historia hiyo nzuri lakini tatizo likaja kutokea baadaye.
Kwa hiyo unashauriwa na mwanaume ufanyiwe uchunguzi kuona kama una tatizo au hakuna. 
Uchunguzi kwa mwanaume ni kupimwa manii na vipimo vingine vitafanyika kadiri daktari atakavyoona inafaa.
Tiba ipo endapo itathibitika tatizo ni uzalishaji au nguvu za kufanya tendo la ndoa. Kama tatizo ni ufahamu wa siku zipi za kushika mimba pia itaeleweshwa. Ni vema uwahi hospitali.
TATIZO KWA MWANAMKE
Kama ilivyo kwa mwanaume, mwanamke pia anahitaji uchunguzi wa kina, kwani tatizo linaweza kusababishwa na mambo mengi.
Matatizo yanaweza kuanzia ukeni yakapanda ndani au yakaanzia humohumo ndani.


leo tuliangalie kwa upande wa wanawake.
Kama ilivyo kwa mwanaume, mwanamke pia anahitaji uchunguzi wa kina, kwani tatizo linaweza kusababishwa na mambo mengi.
Matatizo yanaweza kuanzia ukeni yakapanda ndani au yakaanzia humohumo ndani.
Matatizo ya uzazi kwa mwanamke yamegawanyika katika maeneo tofauti, unaweza kuwa na tatizo katika mirija ya uzazi, mfumo wa homoni au katika kizazi.
Matatizo katika mfumo wa homoni au vichocheo vya mwili husababishwa na mambo mengi ambayo tutakuja kuyaona. Mwanamke mwenye tatizo hili huwa hapevushi au hazalishi mayai.
Daima hulalamika kutoona ute wa uzazi, kuvurugika na kufunga siku za hedhi, kutopata raha au kutojisikia wakati wa tendo la ndoa, maumivu wakati wa tendo na kutokwa na uchafu ukeni na muwasho.
Tatizo la ndani ya kizazi hutokana na athari katika tabaka la ndani la kizazi, uvimbe kwenye kizazi na maambukizi sugu ya kizazi ambapo humfanya mwanamke asumbuliwe na tumbo chini ya kitovu mara kwa mara au maumivu makali anapokuwa katika siku zake.
Mwanamke pia anaweza kupata tatizo la mirija ambayo inaweza kuziba yote miwili au mmoja. Mirija inaweza kujaa maji ‘Hydrosalpinx’ au kujaa usaha, maambukizi sugu au makali katika mirija, matatizo katika vifuko vya mayai, vilevile inaweza kusababisha kutokea kushikamana kati ya kizazi na mirija na viungo jirani.
Kuvurugika kwa mzunguko wa hedhi hutokana na matatizo katika mfumo wa homoni hali ambayo huweza kusababishwa na matumizi ya dawa za homoni kwa kushauriwa na daktari au kwa kutoshauriwa.
Dawa hizi zinaweza kuzuia mimba au zikatumika kwa lengo la matibabu. Kwahiyo ni vema unapokuwa na hali hii umuone daktari mapema.
Wanawake wengine hupatwa na hali hii baada ya kuharibikiwa na mimba au kubadilisha hali ya hewa.
Matatizo katika kizazi na mirija huchangiwa zaidi na maambukizi sugu ya kizazi ambayo husambaa katika mirija na hutokana zaidi na kuharibika mimba, kusafisha kizazi mara kwa mara, magonjwa ya zinaa na uambukizi sugu ukeni.
Maambukizi sugu ya ukeni huambatana na kutokwa na uchafu wenye harufu na muwasho.
Uvimbe kwenye kizazi unaweza kuwa ‘fibroids’ ambazo zinaweza kuzuia au zisizuie kupata ujauzito kutegemea na ukubwa na jinsi zilipokaa.  Uvimbe kwenye mirija na vifuko vya mayai pia inategemea na ukubwa.
Uvimbe huu wa mirija ya mayai na vifuko vyake unaweza kutibiwa kwa dawa au kwa njia ya upasuaji kutegemea na ukubwa na mahali ulipo.
SIKU ZA KUPATA MIMBA
Ni vema mwanamke na mwanaume wote kwa pamoja wakafahamu ni siku zipi za kupata ujauzito ili tendo la ndoa lifanyike kikamilifu.
Huenda mwanamke hana tatizo na mwanaume hana tatizo na jitihada za kutafuta mtoto zinafanyika bila mafanikio kumbe tatizo ni kutofahamu ni siku gani za kupata mimba.
Ili kufahamu vizuri hili, ni vema mzunguko wa hedhi wa mwanamke ufahamike vizuri. Faida ya kujua siku za kupata mimba inasaidia kujua pia siku za kuepuka kupata mimba ili utumie njia ya uzazi wa mpango wa kalenda.
Pia itakusaidia kupanga jinsi ya mtoto unayemtaka kama unataka wa kiume au wa kike.
Katika kufanikisha hili zipo kanuni zake nyingi ambazo tutakuja kuona katika makala ijayo.
Hivyo ni muhimu kufahamu mzunguko wako wa hedhi. Ili mfanikiwe katika hili ni vema wote wawili mkafanya uchunguzi ili kuhakikisha hakuna mwenye tatizo katika suala la uzazi.
Kwa kifupi mzunguko wa hedhi umegawanyika katika maeneo makuu mawili; upo mzunguko wa hedhi unaopevusha mayai na ule usiopevusha mayai. Mwanamke anaweza kuwa na mmojawapo au akawa na yote ikawa inabadilishana kila mwezi.
Mzunguko unaopevusha mayai mwanamke anaweza kupata mimba na ule usiopevusha hawezi kupata.
Kwa hiyo linapokuja suala la kalenda ni vema ukafahamu urefu wa wastani wa mzunguko wako. Tutakuja kuona njia nzuri ya kuhesabu na kutambua mzunguko unaopevusha na ule usiopevusha na siku za kupata mimba pamoja na kupanga jinsia.
USHAURI
Matatizo ya uzazi hufanyiwa uchunguzi na kutibiwa katika kliniki za masuala ya uzazi kwenye hospitali za wilaya na mikoa.
Ni vema uwaone madaktari bingwa kwa matatizo haya ya uzazi. Epuka kutumia madawa bila ya uchunguzi na ushauri wa hospitali.

0 comments:

Post a Comment