Friday, 22 August 2014

MAUMIVU YA TUMBO YA MARA KWA MARA KWA WANAWAKE

Wanawake wanaosumbuliwa na maumivu ya tumbo chini ya kitovu mara kwa mara hupata athari nyingi baadaye endapo kama hawatagundua chanzo cha maumivu hayo.
Katika tumbo la mwanamke kuna mfumo wa kawaida wa tumbo ambao ni tumbo la chakula na mfuko wa haja kubwa, kuna kibofu cha mkojo na mfumo wa mkojo.


Pia kuna mfumo wa uzazi ambao ndiyo tunaozungumzia leo kwa undani.
Mfumo wa chakula una matatizo yake mengi ambayo huambatana na kichefuchefu na kufunga choo, mfumo wa mkojo nao una shida nyingi tu ambazo ni maambukizi au ‘UTI’ au Yutiai ambayo huambatana pia na maumivu katika njia ya mkojo.

Matatizo ya mfumo wa uzazi huambatana na dalili mbili, mojawapo ni ile ya kutokwa na uchafu ukeni.
Chanzo cha tatizo

Maumivu ya mara kwa mara ya tumbo kwa wanawake yanahusiana zaidi na mfumo wa uzazi. Maumivu haya yanaweza kuwa maambukizi katika mfumo wa uzazi ambayo huathiri kuta za ndani za uzazi, maambukizi yanasambaa hadi katika mirija ya uzazi hali iitwayo ‘Salpingitis’ na huweza kusababisha mirija kujaa maji ‘Hydrosalpinx ’ au kujaa usaha ‘Pyosalpinx’.
Maambukizi pia husambaa hadi katika vifuko vya mayai ‘Oophoritis’.
Maambukizi pia huwa ukeni na kitaalamu huitwa ‘Vaginitis’ na hushambulia kuta za uke, yakifika katika mlango wa shingo ya kizazi huitwa ‘Cervicitis’.
Pamoja na kushambulia ndani ya uke na shingo ya kizazi, pia hushambulia nje kabisa ya uke ambapo mwanamke hulalamika muwasho nje ya uke kwenye midomo au mashavu ya uke na hata kutokwa vipele.
Dalili za tatizo


Mwanamke mwenye tatizo ukeni hulalamika muwasho ukeni na kutokwa na uchafu ambao mara nyingi huwa na harufu kama shombo la samaki. Pia hulalamika maumivu wakati wa tendo la ndoa.
Mwanamke ambaye maambukizi yamefika katika mlango wa shingo ya kizazi hupatwa na maumivu wakati wa tendo la ndoa na wakati mwingine hutokwa na damu wakati wa kujisafisha huona damu kidogo au kama hakuna damu atahisi mdomo wa kizazi umevimba na kushika kitu kama kigololi ndani ya uke.
Mwanamke pia hulalamika kama kuna kitu kinasukumwa wakati wa tendo la ndoa.
Maumivu ndani ya kizazi hasa katika kuta za ndani hupatwa na maumivu baada ya tendo la ndoa, vilevile hupatwa na maumivu chini ya tumbo muda wote yaani kila siku na kumnyima raha. Maumivu wakati wa hedhi na kutokwa na damu nzito nyeusi na wakati mwingine hutoa harufu.
Maumivu yakiwa katika mirija ya uzazi husambaa chini ya tumbo kulia na kushoto, maumivu pia huwa ya muda mrefu na hali hii humfanya mgonjwa apate haja kubwa kwa shida.
Maambukizi katika vifuko vya mayai husababisha siku za hedhi zivurugike na ziwe hazina mpangilio maalum, huathiri upevushaji na uzalishaji wa mayai hivyo kushindwa kupata ujauzito.
Maambukizi nje ya kizazi humfanya mwanamke aumwe tumbo lote na kupata hali iitwayo ‘Perionitis’, hupata homa za mara kwa mara na mwili kuwa mnyonge.
Maumivu ya muda mrefu hudhoofisha afya ya mwanamke, hukosa hamu ya kula na kupoteza raha ya tendo la ndoa na uzazi husumbua.
Maambukizi hushambulia kwa njia ya kupitia ukeni, mfano magonjwa ya ngono, kuharibika au kutoa mimba na hata kwa kufanyiwa upasuaji wa tumbo pia huathiri mfumo wa uzazi.
Vyanzo vingine vinavyoathiri mfumo wa uzazi na kusababisha maumivu ya chini ya tumbo mara kwa mara ni matatizo katika mfumo wa homoni au vichocheo, uvimbe katika kizazi, mirija na vifuko vya mayai.
Athari za tatizo
Maambukizi sugu katika mfumo wa uzazi huathiri mzunguko wa hedhi, uzalishaji mayai ya uzazi, kuziba mirija ya uzazi, kupoteza hamu na uwezo wa kufanya tendo la ndoa.
Kwa ujumla mwanamke mwenye tatizo hili anaweza kupoteza uwezo wa kuzaa na kuwa mgumba.
Matatizo haya hutokea zaidi kwa mwanamke aliye katika umri wa kuzaa.
Uchunguzi
Matatizo haya hufanyiwa uchunguzi katika kliniki za magonjwa ya kinamama. Vipimo mbalimbali vitafanyika kadiri daktari atakavyoona inafaa. 
Matibabu
Tiba inaweza kuwa dawa, upasuaji au yoyote ambayo daktari ataona inafaa kutegemea aina na ukubwa wa tatizo.

0 comments:

Post a Comment