Friday 22 August 2014

ATHARI ZA MAAMBUKIZI KATIKA VIUNGO VYA UZAZI




Maambukizi kitaalamu huitwa ‘Pelvic Inflammatory Diseases’. Maambukizi haya huwa sugu na huchukua muda mrefu mwanamke kupona endapo atakuwa na tatizo hili.Maambukizi hushambulia kizazi na mirija ya mayai na viungo jirani kama vile kibofu cha mkojo na tumbo.
Chanzo cha maambukizi
Maambukizi haya huwapata wanawake walio katika umri wa miaka 15 hadi 25 ambao tunasema wapo katika umri wa kuzaa.
Vimelea vya ugonjwa huu husambazwa kwa njia ya ngono, pia tatizo hutokea ndani kwa ndani endapo kutakuwa na maambukizi katika kidole tumbo.Vimelea vinavyosababisha maambukizi haya au ugonjwa wa ‘PID’ ni ‘Chlamydia’ au hutamkwa Klamidia ambapo hukabili takriban asilimia hamsini ya matatizo haya.
Vyanzo vingine ni vijidudu vya kisonono au gono.
Pia kuna uwezekano mkubwa mwanamke akapata maambukizi ya vimelea vyote vya aina mbili.
Dalili za ugonjwa
Mgonjwa hulalamika maumivu ya tumbo chini ya kitovu na hushambulia pande zote chini ya kitovu kulia na kushoto, mara chache maumivu huwa upande wa juu wa tumbo yaani juu ya kitovu. Siku za hedhi huvurugika, hutokwa na uchafu ukeni na uchafu huu huwa na harufu mbaya na muwasho, hupata maumivu wakati wa kukojoa, maumivu huwa kwa ndani zaidi na wakati mwingine hufunga kupata haja kubwa.
Mgonjwa hulalamika kupata homa za mara kwa mara na mwili daima unakuwa mchovu.
Athari za ugonjwa
Mwanamke mwenye tatizo hili pamoja na  kuumwa tumbo chini ya kitovu mara kwa mara, athari kubwa anazopata ni kuziba kwa mirija ya uzazi na hivyo kushindwa kupata ujauzito ndani ya mwaka mmoja.
Siku za hedhi huvurugika na maumivu makali wakati wa hedhi na kushindwa kujua siku za kupata ujauzito.
Athari nyingine ni uwezekano wa kupata mimba kwenye mrija ’Ectopic Pregnancy’ kutokana na mrija kuziba nusu.
Uchunguzi
Uchunguzi hufanyika katika hospitali ya mkoa katika kliniki za magonjwa ya akina mama. Vipimo mbalimbali vitafanyika, mfano kipimo cha kuangalia ukeni na kuchukua majimaji ya ukeni na kupimwa maabara, vipimo vingine ni Ultrasound na vingine ambavyo daktari ataona vinafaa.
Ushauri
Ni vema umuone daktari wa kinamama kwa uchunguzi wa kina. Vipimo vya mkojo pia vitafanyika na vingine ambavyo vimeelezwa ili kupata ufumbuzi wa kudumu.
Ni vema kujikinga na kuepuka ngono zembe, epuka kuwa na wapenzi wengi, jiweke katika hali ya usafi wa hali ya juu katika mazingira ya ukeni na haja kubwa. Wahi hospitali kwa uchunguzi na tiba.

0 comments:

Post a Comment