Utafiti wa hivi karibuni uliofanywa nchini Marekani umeonesha kuwa suala la unene wa kupita kiasi (obesity), limekuwa tatizo kubwa duniani kuliko hata tatizo la njaa.
Takwimu zilizopo zinaonesha kuwa mwaka 1950, idadi ya watu waliokuwa wakikabiliwa na njaa duniani ilikuwa milioni 700. Kwa miaka hiyo, watu milioni 100 tu ndiyo walioathiriwa na matatizo ya unene wa kupita kiasi. Yaani watu milioni 700 walikuwa wanasumbuliwa na njaa na watu milioni 100 walisumbuliwa na unene.
Lakini kwa kipindi cha miongo sita tangu miaka ya hamsini, hali imebadilika. Kwa takwimu za mwaka 2010, watu milioni 800 wanasumbuliwa na tatizo la njaa (hunger), likiwa ni ongezeko la watu milioni 100 tangu wakati huo.
Lakini kwa upande wa pili, hadi kufikia mwaka 2010 watu milioni 500 wanasumbuliwa na tatizo la unene, likiwa ni ongezeko la watu milioni 400 ukilinganisha na ongezeko la watu milioni 100 wa njaa katika kipindi hicho. Nchini Marekani kuna ongezeko la asilimia 350 la watu wenye unene wa kupita kiasi ndani ya kipindi cha miaka michache tu iliyopita.
Kutokana na hali inavyojionesha, inakadiriwa kuwa ifikapo mwaka 2030, zaidi ya watu bilioni moja duniani kote watakuwa na tatizo la unene wa kupindukia na baadhi ya nchi duniani zina hali mbaya zaidi kwa sasa.
Kutokana na matatizo ya unene wa kupindukia, watu milioni 100 nchini India na Mexico wanahofiwa kupatwa na ugonjwa wa kisukari hivi sasa. Katika nchini hizo inaelezwa kuwa magonjwa yatokanayo na unene ndiyo yanayotawala na Mexico ni miongoni mwa nchi zinazotumia kwa wingi vinywaji baridi kama soda.
Tatizo la unene siyo tu ni la nchi zilizoendelea, kama Marekani, Uingereza, Austarlia, bali ni la nchi zinazoendelea pia, ikiwemo Tanzania. Chanzo cha matatizo ya unene wa kupindukia ni vyakula vya kusindika, kupenda kula kila wakati bila kufanya mazoezi, mtu yeyote mwenye tabia ya kupenda kula vyakula vya kusindika (proccessed food), suala la kunenepeana haliepukiki.
Kwenye miaka ya 50, vyakula na vinywaji vya kutenegeneza (artificial) vilikuwa vichache au havikuwepo kabisa, tofauti na miaka ya sasa ambapo vyakula vinavyoliwa kwa wingi na idadi kubwa ya watu, mijini na vijijini ni vyakula vya kusindika, vyenye sukari, mafuta mengi na vyenye kemikali zinazowekwa kwa ajii ya kuvihifadhi visiharibike.
Inaelezwa kuwa ongezeko la unene wa kupindukia katika nchi zinazoendelea kama Tanzania, lina uhusiano mkubwa na ongezeko la mauzo ya vinywaji baridi kama soda na juisi zinazotengenezwa kwa kutumia kemikali zenye ladha mbalimbali za matunda, huku watumiaji wakihadaika na utamu wa sukari nyingi uliyomo.
Mara nyingi kuongezeka kwa uzito wa mwili uhusiana na hatari ya kupatwa na magonjwa sugu, yakiwemo presha na kisukari. Tunashauriwa kuepukana na imani potofu kuwa mtu mwenye afya njema ni yule aliyenenepa, vijana pamoja na watoto wanene ndiyo wako katika hatari zaidi ya kupatwa na magonjwa hatari kuliko watu wazima. Tujihadhari na unene!
0 comments:
Post a Comment