Monday 7 July 2014

JUISI YA MAJANI YA PAPAI: KIBOKO YA DENGUE




Ugonjwa wa Homa ya Dengue (dengi) umeibuka nchini katika siku za hivi karibuni na kuwa tishio. Ripoti za awali kuhusu Dengi kwa mwaka huu, ziliibuka kwa kishindo baada ya kuwakumba hadi wasanii maarufu. Ni ugonjwa ambao umekuwepo kwa miaka mingi na huwa unajirudia mara kwa mara, lakini kwa mwaka huu umekuja kwa kishindo zaidi.
Ugonjwa huu husumbua sana katika nchi za Asia zenye watu wengi, hasa nchini Malyasia ambako imeelezwa na Shirika la Afya Duniani kuwa hadi kufikia Machi 22, mwaka huu, watu waliokumbwa na ugonjwa huo walikuwa zaidi ya 23,000 na vifo 58, likiwa ni ongezeko la asilimia 314, ukilinganisha na mwaka jana!

Aidha, imeelezwa katika taarifa hiyo ya WHO kuwa inakadiriwa watu kati ya milioni 50 – 100 huambukizwa Dengi duniani kila mwaka, hivyo utaona kwamba ni ugonjwa unaosumbua dunia kila mara. Chanzo ni mazingira machafu yanayozalisha mbu wanaouma mchana.
TIBA MBADALA
Kama ilivyo kwa magonjwa mengi yanayomkabili binadamu, Dengi nao inayo tiba mbadala ambayo inaaminika kuwasaidia na kuwatibu watu wengi wanaopatwa na ugonjwa huu, ambao unaelezwa kuwa ukikupata hutakiwi kutumia dawa bila ushauri wa daktari.
MAJANI YA MPAPAI

Kwa mujibu wa utafiti uliofanyika nchi za Malysia na India, ambako ugonjwa huu unawasumbua sana kila mwaka, juisi itokanayo na majani ya mpapai huweza kutibu na kumpa nafuu mgonjwa wa Dengi kwa haraka zaidi.
JINSI YA KUANDAA JUISI
Ili kupata juisi ya majani ya mti wa mpapai kwa ajili ya homa ya Dengi, kata matawi mabichi yaliyokomaa ya mpapai kiasi cha matawi mawili au matatu, kutegemeana na kiwango cha juisi unachokitaka kupata.
Kuna njia mbili unayoweza kuitumia kutengeneza hiyo juisi.

Ya kwanza ni njia ya asili. Ukishakata matawi yako mawili, kata yale majani tu na uyasage kwenye jiwe au uyatwange kwenye kinu hadi yawe laini (usisage pamoja na matawi, chukua na saga majani peke yake).
Njia ya pili, unaweza kutumia mashine za kisasa za kutengeneza juisi, kama vile Blender au Juicer kwa kuweka majani na kisha kuyasaga hadi kulainika na kuwa tayari kutoa juisi.

Baada ya hapo, ukiyakamua kwa mkono majani hayo yatatoa juisi ambayo utaikamulia kwenye chombo safi kwa kiwango utakacho.
DOZI YAKE
Baada ya kupata juisi, inashauriwa kuinywa kutwa mara tatu kwa siku mbili hadi tatu, kijiko kimoja kikubwa cha chakula kwa mtu mzima na kijiko kimoja kidogo cha chai kwa mtoto.

Juisi ya majani ya mpapai ni chungu sana, hata hivyo inashauriwa kuinywa hivyo bila kuchanganya na kitu chochote. Iwapo utashindwa, haswa kwa watoto wadogo, unaweza kuichanganya na vijiko vichache vya asali ili kupata ladha tamu kiasi.
ZINGATIA
Inayotibu siyo juisi ya papai, bali ni juisi ya MAJANI YA MTI WA MPAPAI. Muda wa kutumia juisi hii kama tiba ni siku mbili hadi tatu, iwapo utaona hupati nafuu yoyote, unashauriwa kupata ushauri wa daktari na ni vyema ukatumia tiba mbadala yoyote baada ya kupata uhakika na unachoumwa.

MWISHO, wagonjwa wa Dengi hupata nafuu haraka kwa kunywa juisi halisi za matunda mbalimbali, hasa juisi ya machungwa.
Kwa kawaida, homa ya Dengi inapotokea huweza kudhibitiwa na mgonjwa akapona bila kutumia dawa iwapo mwili una kinga ya kutosha, kinga ya mwili ya asili hupatikana kwa kuzingatia ulaji wa matunda na mboga za majani kwa wingi kila siku.

0 comments:

Post a Comment