Saturday, 28 June 2014

SIRI YA KUONDOA MARADHI YA KOLESTRO MWILINI




KWA kuzingatia kwamba wenye lehemu nyingi mwilini (Bad High Cholestol) huwa katika hatari zaidi ya kupatwa na magonjwa ya moyo, ikiwemo kupooza (stroke), suala la kuhakikisha mwili wako unakuwa na kiwango cha mafuta kinachotakiwa ni la lazima.
Siri ya kujiepusha na magonjwa hayo iko kwenye chakula, hususan mboga na matunda, ambayo nimeyaorodhesha katika makala haya ya leo, kama ifuatavyo:

CHAI YA KIJANI (GREEN TEA)
Ingawa hata chai nyeusi nayo inavyo virutubisho vyenye uwezo wa kupunguza kolestro mwilini, lakini chai ya kijani ndiyo yenye nguvu zaidi. Chai ya kijani huwa haipitii mchakato wa moto ambao hupunguza nguvu nyingi za virutubisho kama ilivyo kwa chai nyeusi.

Kwa mujibu wa watafiti, kwa kuwa chai ya kijani haipitii mchakato wa moto, hubaki na kiwango kingi cha kirutubisho chenye uwezo wa kushusha lehemu mwilini, kirutubisho hicho kinajulikana kama Catechins.
MAHARAGE (Beans)
Utashangaa lakini ndiyo ukweli wenyewe! Maharage haya haya ambayo baadhi huwa hawapendi kabisa kuyala na hata wanapoyala huonekana kama ni kwa sababu ya shida.

Aina zote za maharage zimeonekana kuwa na kiwango kingi cha kamba lishe (fibre) ambayo husaidia kuondoa kolestro na sumu zingine mwilini wakati wa kwenda haja kubwa. Hivyo maharage nayo ni sehemu ya chakula muhimu kwa moyo wa binadamu.

KARANGA (Nuts)
Kama ulikuwa siyo mpenzi sana wa kula karanga, korosho na jamii nyingine za karanga, basi unatakiwa kujiangalia upya, kwani vitafunwa hivi vina virutubisho vya kutosha vya kuzuia na kuondoa mafuta mabaya mwilini. Kiasi cha kiganja kimoja cha karanga kwa siku kinatosha, hasa karanga mbichi.

PARACHICHI (Avacado)
Ingawa kwa kawaida yanaonekana kama yana mafuta, lakini maparachichi yana kirutubisho aina ya Oleic Acid, ambacho siyo tu huondoa mafuta mabaya mwilini (LDL), bali huyaboresha mafuta mazuri yanayotakiwa mwilini.

Si hayo tu, maparachichi yana kamba lishe za kutosha ambazo husaidia usagaji wa chakula na uimarishaji wa kiwango cha kolestro mwilini.

PEASI (Pears)
Kama msemo maarufu wa Kiingereza usemao, An Apple a Day, keeps the doctor away (Epo moja kwa siku, humuweka daktari mbali), kwa peasi ni zaidi ya epo. Mapeasi yana uwezo mkubwa sana wa kushusha kolestro mwilini kushinda hata epo. Ili kupata faida zake zote, inashauriwa kulila peasi pamoja na maganda yake.

Halikadhalika matunda mengine kama vile machungwa, ndizi mbivu na nyanya za mboga, vina uwezo mkubwa wa kushusha na kuondoa mafuta mabaya (bad cholestrol) mwilini ambayo ndiyo huwa chanzo cha matatizo makubwa ya moyo na kiharusi.

Kama unajali afya yako, hakikisha unakula matunda hayo kila siku au kila msimu ili kujilinda dhidi ya magonjwa ya moyo na athari zake. Kwa lolote, usisite kuwasiliana nasi kwa namba zilizopo hapo juu.

0 comments:

Post a Comment