Saturday, 28 June 2014

SABABU 7 KUU MUHIMU ZA MWANAMKE KUTOPATA UJAUZITO



Moja ya matatizo yaliyoko katika
jamii zetu na yamesababisha
wanandoa wengi au wanawake
wengi kukosa furaha, ni kukosa
uwezo wa kupata ujauzito kwa
mwanamke.

Sote tunafahamu kuwa, swala la
mwanamke kupata ujauzito
linahusisha pande zote mbili,
yaani upande wa mwanamke na
pia upande wa mwanamme, wote
wawili wanapokuwa katika afya
nzuri ndipo ujauzito unaweza
kupatikana kwa mwanamke.

Miongoni mwa sababu
zinazoweza kumfanya
mwanamke ashindwe kupata
ujauzito ni kama zifuatazo:

1. Matatizo katika homoni, 
hii ni
kutokana na kwamba, mzunguko
(Menstrual cycle) katika mwili wa
mwanamke hutawaliwa na hizi
kemikali asilia ndani ya mwili
ambapo mabadiliko madogo
yakitokea katika uzalishaji wa
hizi homoni au homoni
kuzalishwa katika wakati ambao
siyo muafaka huweza kupelekea
mwanamke akashindwa kupata
ujauzito, pia tatizo la kuwa na
uzito wa mwili mdogo sana au
mkubwa sana pia huathiri hali
nzima ya homoni na kupelekea
kushindwa kupata ujauzito.

2. Umri,
Kwa wanawake uwezo wa
kupata ujauzito unapungua kwa
kadri umri unavyoongezeka, hii
inatokana na kupungua kwa
uzalishaji wa homoni husika
wakati umri unavyoongezeka.
Kuanzia miaka 35 na kuendelea
huwa kunakuwa na tatizo la
kushindwa kupata ujauzito kwa
wanawake wengi.

3. Kuziba kwa mirija (fallopian
tubes),
Hii husababisha mbegu za
kiume (sperms) zishindwe
kulifikia yai na kulirutubisha ili
ujauzito utokee. Kuziba kwa
mirija huweza kusababishwa na
magonjwa yanayoambukizwa
kwa njia ya kujamiiana, matatizo
katika kizazi au upasuaji. Mara
nyingi wanawake ambao mirija
yao imeziba, hawahisi dalili
zozote..

4. Ute ute katika kizazi (mucus
problems),
Ute unaopatikana
katika kizazi cha mwanamke
huwa na sifa ya kuruhusu mbegu
za kiume ziweze kusafiri kwa
urahisi na kulifikia yai ili
kulirutubisha. Kwa baadhi ya
wanawake ute huu unakuwa na
uzito na kemikali ambazo ni
vigumu kwa mbegu za kiume
kuweza kupita, na wakati
mwingine mwili wa mwanamke
huzalisha sumu ambazo huziua
mbegu za kiume, haya yote
husababisha kukutana kwa yai
na mbegu za kiume kusitokee na
hivyo ujauzito kutopatikana.

5. Uvimbe katika kizazi (fibroids),
hii huchangia asilimia tatu (3%)
katika mwanamke kutopata
ujauzito. Uvimbe huu ambao
hutokea katika kuta za mji wa
mimba, kwa namna moja au
nyingine huweza kuzuia yai
lililorutubishwa lisikae sehemu
yake na hivyo kuathiri kizazi.

6. Matibabu ya kansa,
Kwa kutegemeana na aina ya
matibabu, aina ya dawa au njia
ya mionzi, hizi huweza
kumuathiri mwanamke na
kumsababishia kushindwa kupata
ujauzito.

7. Ukomavu katika kizazi,
Kwa baadhi ya wanawake wanayo
matatizo ambayo kizazi chao
huwa hakijakomaa vizuri au
katika kuzaliwa kwao walizaliwa
na tatizo hili ambalo, kizazi
hakiko sawa (abnormally
developed uterus).

USHAURI
Asilimia kubwa ya matatizo ya
mwanamke kushindwa kupata
ujauzito yanayo tiba, kama unalo
tatizo katika kupata ujauzito
usikate tamaa, onana na
wataalamu wa afya ili uweze
kujua chanzo cha tatizo lako na
kupatiwa msaada unaostahili.

0 comments:

Post a Comment