Tuesday 17 June 2014

FAHAMU SARATANI YA TEZI DUME (PROSTATE CANCER)





Ugonjwa huu ni chanzo kikuu cha vifo vinavyosababishwa na saratani kwa wanaume wenye umri wa miaka 70 na kuendelea, hata hivyo, satarani ya tezi dume kwa sasa inawapata sana wanaume kuanzia miaka 25.
Kwa ufahamisho tu ni kwamba  neno saratani ni jina la ugonjwa ambalo hutokea wakati chembechembe za uhai au seli katika sehemu fulani ya mwili zinapoanza kukua bila kufuata utaratibu wa mfumo wa mwili na kutengeneza vijiuvimbe vidogo vidogo.
Kwa kawaida seli huwa zinajigawa, kupevuka na baadaye kufa kwa kufuata taratibu za mfumo wa mwili. Lakini seli za saratani hazifuati mfumo huo, badala ya kufa, zenyewe huishi muda mrefu kuliko chembe chembe za kawaida na wakati huohuo huendelea kutengeneza seli nyingine na kuwa uvimbe wa saratani au tumour.
Tezi dume linapatikana katika mwili wa mamalia dume tu na pale seli katika kiungo hicho zinapoanza kukua bila kufuata utaratibu wa mfumo wa mwili hapo ndipo mtu huyo hupata saratani ya tezi dume.
 Ugonjwa huu pia hujulikana kama saratani ya kipofu huwapata wanaume tu na hasa wenye umri wa takriban miaka 50 na kuendelea.
Saratani hii imethibitika kushika nafasi ya pili, ukiachia mbali saratani ya mapafu kwa kusababisha vifo vya wanaume wenye umri wa takriban miaka 50 na kuendelea.
Kuna vihatarishi vingi vinavyochangia mwanaume kupata saratani ya tezi dume. Vifuatavyo ni baadhi yake: Kwanza kabisa ni umri. Nafasi ya kupata saratani ya tezi dume huongezeka sana hasa ukifikia umri wa karibu miaka 50 na kuendelea.
Nasaba ni kihatarishi kingine ambapo wanaume wenye historia ya tatizo hili kwenye familia zao, yaani wale ambao mmoja wa ndugu zao wamewahi kuugua ugonjwa huu huwa katika hatari ya kupata kansa hiyo kutokana na kurithi jeni za ugonjwa huo.
Suala jingie ni lishe ambapo wanaume wanaopenda kula nyama au (red meat) na walaji wa chakula chenye kiasi kikubwa cha mafuta hasa ya wanyama huwa katika hatari kubwa ya kupata saratani ya tezi dume.
Pia wanaume wasiopenda kufanya mazoezi, wanene na wenye upungufu wa virutubisho vya Vitamin E wako kwenye hatari zaidi ya kupata saratani ya kibofu cha mkojo.
Nao wakulima wanaotumia aina fulani ya mbolea za kemikali, wanaofanya kazi katika viwanda vya kutengeneza matairi na wachimbaji madini, hususan aina ya cadmium hao wamo hatarini kupata saratani hii.
DALILI
Katika hatua zake za awali, dalili za saratani ya tezi dume hazitofautiani na zile za kuvimba kwa tezi dume au BPH. Dalili hizo ni pamoja na, kupata shida wakati wa kuanza kukojoa, kutiririka kwa mkojo baada ya kumaliza kukojoa, kukojoa mkojo wenye mtiririko dhaifu,  kukojoa mara kwa mara hasa nyakati za usiku.
Dalili nyingine ni kujikakamua wakati wa kukojoa na kushindwa kumaliza mkojo wote na kutoa mkojo uliochanganyika na damu. Mwanaume anapoanza kuona na kuhisi baadhi ya dalili hizo anapaswa kuwahi hospitali kupimwa.
Iwapo saratani imesambaa mwilini kiasi cha kuhusisha sehemu nyigine za mwili, mgonjwa anaweza kuwa na maumivu makali ya mifupa katika maeneo ya nyonga, mapajani na kiunoni.
Dalili nyingine ni za kawaida ambazo  zinazoweza kumpata mgonjwa mwingine yeyote wa saratani kama vile kupungua uzito, kuhisi kichefuchefu, uchovu, kizunguzungu na kadhalika.
TIBA
Kabla ya tiba kuna vipimo vitahitajika. Kuna vipimo viwili ambavyo daktari anaweza kumpima mwanaume ikiwa ni hatua ya kwanza ya kugundua ugonjwa huo.
Vipimo hivyo vya kwanza ni “Digital Rectal Exam (DRE)” na cha pili ni “Prostate Specific Antigen (PSA)”. DRE pamoja na PSA huonesha uwepo wa tatizo kwenye tezi dume, lakini vipimo hivi havina uwezo wa kutofautisha iwapo tatizo hilo linamaanisha saratani au uvimbe katika tezi dume.
Hivyo basi, ili kuweza kutofautisha kati ya magonjwa hayo mawili, kipimo kiitwacho Prostate biopsy hufanywa. Baada ya vipimo hivyo kama vitaashiria saratani ya tezi dume basi daktari anaweza kuamuru vipimo vingine ili kuthibitisha uwepo wa ugonjwa huo na vipimo kama vya  transrectal ultrasound au prostatic needle biopsy vinaweza kutumika.
Tukumbuke kuwa kuwahi kugundua saratani mapema kabla ya dalili, kuna faida kubwa kwa muathirika kwani saratani ikigundulika mapema ni rahisi kutibika.
Je, Saratani ya tezi dume inatibika au la jibu ni ndiyo na kuna njia kadhaa za matibabu ya saratani ya tezi dume. Hata hivyo uamuzi wa njia gani itumike unategemea ushauri na maoni ya daktari kulingana na hatua ya ugonjwa ulipofikia na umri wa mgonjwa husika.
Katika hatua za awali za ugonjwa, daktari anaweza kushauri mgonjwa atibiwe kwa kufanyiwa upasuaji na tiba ya mionzi. Hii ni katika hali ambayo kwa wagonjwa wazee, daktari anaweza kushauri mgonjwa kuwa chini ya uangalizi tu bila kufanyiwa upasuaji au bila kupatiwa tiba ya mionzi.
Iwapo saratani imesambaa na kuathiri sehemu nyingine za mwili, matibabu yake yanaweza kujumuisha upasuaji wa kuondoa korodani, matumizi ya dawa za kupunguza kiwango cha homoni ya testosterone katika damu au hormonal therapy, au matumizi ya kemikali za kuua seli za saratani (chemotherapy).
Wasomaji wanapaswa kujua kuwa saratani ya tezi dume ni ugonjwa  wa kawaida kama yalivyo magonjwa mengine na kufanyiwa uchunguzi  na matibabu ya mapema huweza kuokoa maisha ya waathirika wengi wa ugonjwa huo.  

0 comments:

Post a Comment