Thursday, 1 May 2014

WASICHANA WAELIMISHWE KUKWEPA MIMBA ZA UTOTONI




Wanafunzi mabinti wanapopata mimba
hulazimika kukatiza masomo na ndoto zao
za kufanikiwa kupitia elimu huzimika.
Mimba za utotoni ni matukio yanayoelekea
kuzoeleka na kuchukuliwa kuwa ni ya
kawaida.

Hakuna mikakati makini ya kudhibiti hali
hiyo zaidi ya utekelezaji wa sheria kwamba
anayepata mimba lazima afukuzwe shule.
Wasichana zaidi ya 55,000 wamekuwa
wakifukuzwa shule kwa sababu ya ujauzito
au nyinginezo katika kipindi cha muongo
mmoja, kwa mujibu wa ripoti mpya kutoka
Kituo cha Haki za Uzazi (the Centre for
Reproductive Health).

Ripoti hiyo iitwayo Forced Out: Mandatory
Pregnancy Testing and The Expulsion of
Pregnant Students In Tanzanian School
ilizinduliwa hivi karibuni jijini Dar es Salaam
na Evelyn Opondo, Mkurugenzi wa Kanda ya
Africa wa Kituo hicho. Uzinduzi huo
ulihudhuriwa na wadau mbalimbali wa
masuala ya afya, afya ya uzazi na waandishi
wa habari
Miongoni mwa hatua ambazo zimekuwa
zinachukuliwa kukabiliana na tatizo hilo ni
wasichana kupimwa ujauzito na kufukuzwa
shule ambayo ni matokeo ya utekelezaji wa
sera inayokiuka Haki za Binadamu.

“Kuwalazimisha wasichana wadogo
kupimwa mimba katika shule za Tanzania ni
ubaguzi na ukiukaji wa haki za binadamu za
taifa na kimataifa- bila ya kujali kama
wasichana hawa ni wajawazito au la,”
alisema Lilian Sepulveda,mkurugenzi wa
Global Legal Program katika kituo cha Haki
ya Uzazi.”Kukiuka haki za wasichana
wajawazito ni ukiukaji mkubwa wa haki za
binadamu,” alisema.

 
 Mambo mengi yamebainishwa katika ripoti
hiyo, ikiwamo mfumo huo unaotumiwa na
maofisa wa shule kuwa ni aibu na
udhalilishaji licha ya kuchukuliwa kuwa
unalenga kuwazuia wasichana kufanya
ngono na kupata mimba.

Wakati hayo yakifanyika, hakuna utaratibu
wa kutoa elimu ya afya ya uzazi au huduma
ambazo zinaweza kutoa kinga kwa
wanafunzi ikiwamo kuwapa taarifa muhimu
ili wasipate mimba bila ya kupanga.
Matumizi ya vidonge vya kupanga uzazi kwa
wanafunzi nchini Tanzania ni kama hayapo
kwa sababu ni asilimia 15- 19 ya wanawake
wenye uwezo wa kufanya mapenzi ndiyo
wanatumia njia za mpango wa uzazi.

“Wasichana hao, wanastahili haki za
binadamu kama ilivyo kwa wakubwa, na
kwa hiyo wanahitaji kuwa na zana
wanazozihitaji ili kuwapa taarifa na kuweza
kuwafanya kuwa na uchaguzi kuhusu afya
ya uzazi,” alisema Dk. Julius Mashamba,
Wakili na Makamu wa tatu wa Kamati ya
Wataalamu wa Afrika wa Haki na Jamii kwa
watoto (the African Committee of Experts on
the Rights and Welfare of Child.)

“Kwa kuwazuia wasichana kupata vidonge
vya uzazi na elimu ya afya ya uzazi, shule ni
kama zinawalazimisha wasichana kubeba
mimba mapema na kuwafanya washindwe
kupata elimu na kushindwa kutimiza ndoto
za maisha yao,” alisema.

Ripoti hiyo Forced Out imebainisha kuwa,
licha ya kuwapo upungufu wa elimu ya afya
ya uzazi na huduma, serikali ya Tanzania
imeshindwa kukabiliana na kiwango
kikubwa cha matokeo ya ngono na ndoa za
mapema nchini- masuala mawili ambayo
yana mchango mkubwa kwa mimba za
utotoni.

Kwa mujibu wa Ripoti ya Taifa ya uchunguzi
ya mwaka 2009 iliyofadhiliwa na Shirika la
Umoja wa Mataifa la Mfuko wa Watoto
(UNICEF), wanawake watatu kati ya 10
wenye umri kati ya miaka 13 na 14 Tanzania
Bara angalau katika tukio moja
wamekabiliwa na ukatili wa kijinsia kabla ya
kufikia umri wa miaka 18 ambao wengi
wao kwa mujibu wa ripoti wamelazimishwa
kufanya ngono.

Miongoni mwa mapendekezo yaliyotolewa
na Kituo hicho ni kuishauri serikali ya
Tanzania kukomesha mara moja kufanya
mambo kinyume cha sheria kuwalazimisha
wasichana kupima mimba shuleni na
kuhakikisha kuwa wasichana wadogo
wanapata fursa ya kuendelea na elimu
wakati na baada ya kupata mimba.

“Kama serikali ya Tanzania inataka kweli
kukabiliana na tatizo kubwa la mimba za
utotoni, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya
Ufundi iandae na kutekeleza sera za
kuwalinda wasichana kutokana na ukatili
wa mapenzi na kuendelea na elimu shuleni”
alisema Evelyn Opondo.

Pia alisema kuwa” shule zinatakiwa kutoa
elimu bora kuhusu ngono na afya ya uzazi
na sheria za Tanzania lazima zifanyiwe
marekebisho ili kuendana na sheria za
kimataifa za haki za binadamu kwa
kupandisha umri wa wasichana kuolewa
hadi miaka 18,”

Ripoti hiyo imeeleza matukio mengi ya
wasichana waliolazimishwa kupimwa
mimba katika shule za msingi au sekondari,
wengi wao walielezea zoezi hilo kuwa ni la
aibu na lenye maumivu na kwa wale
waliofukuzwa shule walielezea kuwa
walinyanyaswa na familia zao, marafiki na
kubwa kuliko yote ni kwamba nafasi zao za
kupata elimu na hali zao za baadaye
zimevurugwa.

0 comments:

Post a Comment