Thursday 1 May 2014

VIDONDA VYA TUMBO: NI NINI NA HUSABABISHWA NA NINI HASWA?1



Mfumo wa mmeng'enyo wa chakula ni
mfumo katika mwili unaohusika na
umeng'enyaji wa chakula mpaka kuwa
katika hali inayoweza kusharabiwa na
mwili.

Sehemu kuu zinazohusika katika
umeng'enyaji huo ni kinywa, umio
'Esophagus', mfuko wa tumbo 'Stomach',
ini, mfuko wa nyongo, utumbo
mwembamba 'Duedenum & Ileum',
kongosho, utumbo mpana na puru
'Rectum'.
Mfumo wa mmeng'enyo wa chakula hasa
kuta za umio, tumbo na utumbo
mwembamba hupata mmomonyoko ambao
husababishwa na asidi inayotumika
kumeng'enya chakula inaposhambulia kuta
hizo. Kitaalamu hali hii hutambulika kama
'Peptic ulcers'.
Vidonda vya mfumo wa umeng'anyaji
chakula vikiwa kwenye tumbo tunaita
vidonda vya tumbo 'Gastric ulcer', vikiwa
katika duodenum tunaita 'Duodenal ulcer'
na vikiwa katika esophagus tunaita
'Esophageal ulcer'
VINAVYOSABABISHA VIDONDA VYA TUMBO
Bakteria aina ya Helicobacter pylori 'H.pylori'
& Non-Steroidal Anti Inflammatory Drugs
'NSAIDs' ndio visababishi vikuu.
Bakteria H.pylori wanahusika sana kwa
angalau nne ya tano ya vidonda vya tumbo
'Gastric ulcers' & 95% ya 'Duodenal ulcers'
ambapo NSAIDs husababisha 20% ya
'Gastric ulcers' na 5% ya 'Duodenal ulcers'
Bakteria H.pylori husababisha kupitia
vyakula na maji. Pia hupatikana kwenye
mate ya binadamu hivyo inaweza
kusambazwa mdomo kwa mdomo wakati
mkila denda/kunyonyana midomo.
Bakteria H.pylori huishi kwenye kuta za
utumbo na hutengeneza vimeng'enya
'Enzyme' iitwayo 'Urease' inayopunguza
athari za asidi kwenye utumbo.
Utumbo hutaka kufidia kiasi cha asidi
kinachopotea kwa kutengeneza zaidi na
husababisha kukwangua kuta za utumbo.
Non-Steroidal Anti Inflammantory Drugs
'NSAIDs' ni dawa za kutuliza maumivu ya
kichwa, maumivu ya hedhi, kushusha homa
na kuondoa maumivu madogo madogo
mfano Aspirin, Ibuprofen,Diclofenac &
Meloxicam. Dawa hizi hupunguza uwezo
wa kuta za tumbo na kufanya uwe rahisi
kushambuliwa na asidi za tumboni hivyo
kusababisha vidonda.
Chembe za urithi 'Genetics'. Idadi kubwa ya
watu wenye vidonda vya tumbo wana
ndugu wa karibu wenye vidonda pia, hii
huwafanya wataalamu kufikiria kuwa
chembe za urithi zinahusika pia.
Uvutaji sigara/tumbaku. Wavutaji wa sigara
wako katika hatari ya kupata vidonda vya
tumbo ikilinganishwa na wasiovuta.
Matumizi ya pombe/vilevi. Walevi wako
katika hatari zaidi ya kupata vidonda vya
tumbo ikilinganishwa na wasiotumia vileo/
pombe.
Msongo wa mawazo 'Mental stress'.
Msongo wa mawazo hausababishi vidonda
moja kwa moja ila hufanya hali kuwa
mbaya zaidi kwa wagonjwa.
 
DALILI ZA VIDONDA VYA TUMBO
Hata hivyo ni mara chache sana mtu
kuugua vidonda vya tumbo na kutoonyesha
dalili.
Zifuatazo ni dalili zinazotokea kwa
wagojwa wengi:-
·        Maumivu ya tumbo na huwa makali zaidi
pale asidi inapopita juu ya vidonda.
Maumivu yanaweza anzia kwenye kitovu na
kupanda juu hadi katikati ya kifua
'Epigastric pain'
Maumivu yanaweza kuongezeka
unapokuwa njaa. Pia yanaweza kuwa
makali wakati wa usiku kwenye mida ya
kulala, yanayoweza kupunguzwa kwa kula
chakula kidogo.
·         Kushindwa kumeza vizuri chakula.
·         Chakula kukwama kama kinataka kurudi
mdomoni.
·        Kujisikia vibaya baada ya kula.
·        Kupungua uzito.
·        Kukosa hamu ya kula.
 
DALILI HATARI
·        Kutapika damu.
·        Kupata choo kikubwa cheusi au chenye
damu nzito.
·        Kichefuchefu & kutapika.
 
JINSI VIDONDA HUGUNDULIWA:-
Maelezo ya mgonjwa juu ya dalili alizonazo
humsaidia daktari kuhisi kinachomsumbua
mteka wake ni vidonda vya tumbo.
Ili kuthibitisha vidonda vipimo vifuatavyo
hufanyika :
·        Kupima damu 'Blood test'. Kuangalia
bakteria aina ya H.pylori na kama mgonjwa
amekuwa akitumia antibayotiki au dawa za
vidonda Proton Pump Inhibitors 'PPIs'
mfano Omeprazole vipimo vyake vya damu
vitaonyesha majibu hasi 'Negative'
·        Kupima pumzi 'Breath test'. Mgonjwa
hupewa anywe maji yenye atomi za kaboni
zinazoweza kuvunjika, hii hufanya bakteria
H.pylori kuvunjika na baada ya lisaa
mgonjwa hutoa pumzi kwenye chombo
kilichofunikwa kama mgonjwa
ameambukizwa sampuli ya pumzi
itaonyesha vipande vya kaboni kwenye
kabonidioksaidi.
·        Kupima antijeni kwenye kinyesi 'Stool
antigen test'. Kipimo hiki huangalia kama
kuna bakteria H.pylori kwenye kinyesi.
Vilevule kipimo hiki hutumika kuangalia
ufanisi wa matibabu yaliyotolewa dhidi ya
bakteria.
·        X-ray ya sehemu ya juu ya tumbo 'Upper
gastrointestinal x-ray'. Picha huonyesha
umio 'Esophagus', mfuko wa tumbo
'Stomach' na Dudenum. Mgonjwa humeza
maji yenye 'Barium' ambayo hufanya
vidonda kuonekana kirahisi kwa x-ray.
Kamera ya tumbo 'Endoscopy'. Mrija mrefu
wenye kamera huingia tumboni na daktari
huona vidonda kwenye skrini ya kompyuta
'Monitor'.
 
MATIBABU YA VIDONDA VYA TUMBO
Kama vidonda vitakuwa vimesababishwa
na bakteria H.pylori dawa za kuua na
kuondoa bakteria hutumiwa.
Kama vidonda vya tumbo vitakuwa
vimesababishwa na 'NSAIDs' na hana
maambukizi ya bakteria H.pylori atapaswa
kutumia dawa Proton Pump Inhibitors
'PPIs' mfano Omeprazole, Esomeprazole &
Lansoprazole.
Proton Pump Inhibitors 'PPIs' hufanya kazi
kwa kuvunja/kuzuia kazi ya protini ziitwazo
'Proton Pump' ambazo huhusika katika
utengenezaji wa asidi tumboni.
Matumizi ya NSAIDs kwa ajili ya kuondoa
homa na maumivu yatalithiwa na dawa
kama Paracetamol.
Vilevile dawa aina ya H2-Receptor
Antagonists mfano Cimetidine,    hutumika
kama mbadala kama dawa aina ya 'PPIs'
hazitokuwepo.
H2-Receptor Antagonists hufanya kazi ya
kuzuiia utendaji wa protini iitwayo
'Histamine' ambayo inahusika na
kuchochea utengenezaji wa asidi tumboni.
Matibabu yaliyozungumziwa hapo juu
yanaweza kuchukua muda kabla ya kuanza
kufanya kazi hivyo daktari anaweza
kuongeza matibabu mengine kama vizuia
asidi 'Antiacids' & 'Alginates' kwa ajili ya
nafuu ya haraka.
Usitumie dawa hizi ndani ya lisaa moja
baada ya kunywa PPIs mfano Omeprazole
au H2-Receptor Antagonists mfano
Cimetidine.
Makala ijayo itakusaidia jinsi ya kujizuia
usipate vidonda vya tumbo na jinsi kuishi
na vidonda vya tumbo.

0 comments:

Post a Comment