Tatizo la mimba kutoka
au kutolewa ni jambo ambalo limewakumba kina mama wengi walio katika umri wa
kuzaa. Aidha mijadala kuhusu kuhalalishwa au kuendelea kuharamishwa kwa utoaji
mimba ni jambo linalochukua nafasi ya mazungumzo ya kila siku katika maisha yetu.
Kwa baadhi ya nchi, suala la utoaji mimba ni
jambo lililohalallshwa kisheria ingawa kwa nchi kama Tanzania, suala hili
halijahalalishwa isipokuwa tu pale panapokuwa na sababu za kitabibu
zinazolazimisha kufanya hivyo.
Nini maana ya mimba
kutoka (abortion)
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO),
utokaji mimba (abortion)
hutokea pale ambapo kiumbe (mimba) kilicho chini ya wiki 22 kinapotoka kwa
sababu moja ama nyingine, au kinapotolewa kwa njia yeyote ile. Aidha shirika la
Afya limekwenda mbali zaidi na kutoa maana nyingine ya utokaji mimba kuwa ni
pale mtoto (kiumbe) anapozaliwa akiwa na uzito wa chini ya gram 500.
Aidha baadhi ya matabibu hupendelea kutumia neno
'abortion' kumaanisha kitendo cha utoaji wa mimba
kinachofanywa na mtu mwingine ama kwa njia sahihi au zisizo sahihi na 'miscarriage' kumaanisha kitendo cha mimba kutoka yenyewe
kwa sababu nyingine yeyote. Ukiacha tofauti hizi za jinsi ya kuharibika kwa
mimba, abortion na miscarriage humanisha kitu kilekile cha mimba kutoka.
Aina za utokaji/utoaji
mimba (Classification of abortion)
Utokaji mimba umeanishwa katika aina zifuatazo
- Utokaji wa mimba wa hiyari yaani kitendo cha mimba kutoka yenyewe (spontaneous abortion)
- Mimba inayotishia kutoka ingawa bado haijatoka (threatened abortion)
- Utokaji wa mimba usioepukika (inevitable abortion)
- Utokaji wa mimba ulio kamili (complete abortion)
- Utokaji wa mimba usio kamili (incomplete abortion)
- Mimba iliyotoka bila kugundulika kuwa imetoka (missed abortion)
- Utokaji wa mimba unaojirudia rudia (recurrent abortion)
- Utoaji mimba kinyume cha sheria (illegal abortion)
- Utoaji mimba kwa sababu za kiafya (therapeutic abortion)
1. Utokaji mimba kwa
hiari au kitendo cha mimba kutoka yenyewe (spontaneous abortion)
Hii ni hali inayotokea pale mimba inapoharibika
na kutoka bila kuwepo kwa sababu yeyote iliyo dhahiri, kwa maana nyingine mimba
uharibika na kujitokea bila kusababishwa na mtu wala kitu chochote.
Utokaji mimba wa namna hii umegawanyika katika
aina kuu nne ambazo ni
- Mimba inayotishia kutoka ingawa bado haijatoka (threatened abortion)
- Mimba isiyoepukika kutoka (Inevitable abortion)
- Mimba inayotoka yote au kamili (complete abortion), na
- Utokaji mimba usio kamili (Incomplete abortion)
Mimba inayotishia kutoka
(threatened Abortion)
Tatizo hili hutokea mapema wakati wa ujauzito.
Hali hii hujionesha kwa damu kutoka ukeni wakati njia ya shingo ya uzazi ikiwa
bado imefunga. Mara nyingi mimba inayotishia kutoka haina tabia ya kuambatana
na maumivu yeyote ya tumbo.
Daktari anapompima mgonjwa hukuta shingo ya
kizazi ikiwa imefunga na hakuna dalili zozote za kiumbe kutoka ingawa mgonjwa
hutokwa na damu sehemu za siri. Aidha mgonjwa huwa hana maumivu yeyote ya
tumbo.
Mimba isiyoepukika
kutoka (inevitable abortion)
Hii ni hali inayotokea mapema wakati wa ujauzito
pale damu inapotoka ukeni wakati njia ya shingo ya kizazi ikiwa imefunguka au
kuwa wazi. Aidha, kwa kawaida, kiasi cha damu kinachotoka ni kingi na mgonjwa
hujisikia maumivu makali sana ya tumbo.
Utokaji mimba usioepukika waweza kupelekea
·
Utokaji mimba ulio
kamili (complete abortion), au
·
Utokaji mimba usio
kamili (incomplete abortion).
Utokaji mimba usio
kamili (incomplete abortion)
Utokaji mimba usio kamili huambatana na utokaji
damu kwa wingi sehemu za siri za mgonjwa, kufunguka kwa njia ya shingo ya
kizazi, kutoka kwa baadhi ya mabaki ya kiumbe (products of conception) ingawa
mengine hubakia, na mgonjwa kujisikia maumivu makali ya tumbo hususani sehemu
za chini ya kitovu.
Utokaji wa mimba ulio
kamili (complete abortion)
Hali hii huambatana na mama kutokwa damu sehemu
za siri, kujisikia maumivu makali ya tumbo pamoja na kutoka kwa kiumbe
ikiambatana na kondo lake la nyuma. Aidha baada ya muda, mgonjwa hueleza
kupotea kwa maumivu ya tumbo, damu kupungua kutoka sehemu za siri na kufunga
kwa njia ya njia ya shingo ya kizazi (cervix).
Mimba iliyotoka bila kugundulika
kuwa imetoka (missed abortion)
Hali hii hutokea pale ambapo, kiumbe kinapokuwa
kimekufa bila ya mimba kutoka. Mara nyingi, damu huwa haitoki sehemu za siri,
na mgonjwa huwa hajisikii maumivu yeyote ya tumbo. Aidha huwa hakuna dalili
zozote za ukuaji wa mimba na hata mapigo ya moyo ya mtoto hayawezi kutambulika
hata kama vipimo maalum vitatumika.
Utokaji wa mimba
unaojirudia rudia (recurrent abortion)
Hali hii hutokea pale ambapo mama huwa na
historia ya mimba kutoka mara tatu au zaidi kwa mfululizo.
Utoaji mimba kinyume cha
sheria (illegal abortion)
Utoaji mimba kinyume cha sheria ni usitishwaji
wa maisha ya mimba au kutolewa kwa kiumbe kinyume na sheria za nchi husika
zinavyoagiza. Katika mazingira kama haya, sababu dhahiri za kitaalamu
hukosekana isipokuwa wahusika hutenda kulingana na sababu zao binafsi zikiwemo
za kutoitaka mimba au kama ni muhusika ni mwanafunzi huogopa kufukuzwa shule.
Utoaji mimba kisheria
kwa sababu za kitabibu (therapeutic abortion)
Utoaji mimba ulioidhinishwa kitabibu ni
usitishwaji wa mimba kwa ajili ya kuokoa maisha ya mama. Usitishwaji huu ni
hufanywa kitaalamu na daktari. Sababu zinazoweza kufanya mimba ikasitishwa ni
pamoja na
·
iwapo kiumbe kina
mapungufu mengi ya kimaumbile (fetal anomally) ambayo yatamletea mtoto
atakayezaliwa matatizo na hata kusababisha kifo chake
·
iwapo mama mjamzito
alipata ujauzito kwa kubakwa na asingependa kuzaa, au
·
iwapo mama mjamzito ana
kansa , kwa mfano, kansa ya kiwanda cha mayai ya kike (ovarian cancer), kansa
ya damu (leukemia) au kansa ya tezi la goita (thyroid cancer)
Mambo gani hufanya mimba
kutoka kwa hiyari?
Kuna sababu kadhaa zinazoweza kupelekea mimba
kutoka kwa hiyari (spontaneous abortion). Miongoni mwa sababu hizo ni
·
Matatizo kwenye mfumo wa
jenetiki (genetic abnormalities) ambayo husababisha kuharibika na kutoka kwa mimba katika miezi
mitatu ya mwanzoni.
·
Matatizo kwenye mfuko wa
uzazi (uterine problems): matatizo kama vile kuwepo kwa uvimbe kwenye mfuko wa uzazi wa
mwanamke (uterine fibroids), au kulegea kwa milango ya shingo ya kizazi (cervical incompetence)husababisha mimba kutoka katika theluthi ya pili
ya ujauzito (second trimester).
·
Sababu nyingine ni
pamoja na maradhi wakati wa ujauzito kama malaria, kisukari, shinikizo la damu,
kifafa cha mimba, matatizo kwenye tezi ya 'goita' (hypothyroidism). Aidha maambukizi kama Rubella, toxoplasmosis na mengineyo nayo pia huweza kusababisha mimba
kutoka.
·
Kukosekana kwa
ulinganifu katika baadhi ya homoni mwilini (hormonal imbalance)
·
Matumizi ya baadhi
madawa kwa mfano zinazotumika katika kutibu msongo wa mawazo kama vile paroxetine auvenlafaxine nayo yaweza kusababisha utokaji wa mimba.
Tabia hatarishi
zinazoweza kusababisha utokaji wa mimba
·
Unywaji pombe
uliopitiliza.
·
Uvutaji sigara
·
Utumiaji madawa ya
kulevya kama vile kokeini (cocaine)
·
Utumiaji kwa wingi wa
vinywaji vyenye kiasili cha caffeine kama vile kahawa au
kakao.
Vipimo na Uchunguzi
Ili kutambua kuwepo kwa hali hii ya mimba
kutoka, vipimo vifuatavyo vyaweza kufanywa na tabibu
·
Kipimo cha mimba kwa
kutumia mkojo (Urine for hCG)
·
Kupima damu ili kufahamu
kiasi cha wingi wa damu (haemoglobin level), kundi la damu (blood group) na muda wa damu kuganda (bleeding and clotting
time).
·
Kuchunguza iwapo shingo
ya uzazi imefunga au ipo wazi, na pia kuchunguza iwapo kuna dalili ya kiumbe
kutoka ama la. Uchunguzi huu huitwa speculum examination.
·
Ultrasound ya nyonga
(pelvic utrasound) kwa ajili ya kutambua iwapo kiumbe kipo ama la, na kama kipo
je ki hai ama kimekufa.
·
Aidha ni muhimu pia
kufanya uchunguzi wa magonjwa mbali ya zinaa ambayo husababisha mimba kutoka.
Matibabu ya utokaji wa
mimba
Matibabu ya utokaji wa mimba hutegea sana aina
ya utokaji wa mimba. Hata hivyo, ni muhimu kuzingatia vitu vifuatavyo wakati wa
kutoa matibabu kwa mtu aliyepoteza mimba
Wahudumu wa afya huzingatia kanuni zote (ABC) za kuokoa maisha ya mgonjwa kama vile
Wahudumu wa afya huzingatia kanuni zote (ABC) za kuokoa maisha ya mgonjwa kama vile
·
kuhakikisha njia ya hewa
ya mgonjwa ipo wazi na hewa inaingia na kutoka vizuri kwenye mapafu
·
kuhakikisha mgonjwa
anapumua vizuri bila shida
·
kuhakikisha mishipa ya
damu ya mgonjwa imewekwa mrija wa veni (intravenous line) na mgonjwa anapewa dripu ya maji ya normal saline.
·
kuhakikisha mgonjwa
anaongezwa damu haraka iwapo vipimo vitaonesha kuwa alipoteza damu kwa wingi
Matibabu ya mimba
inayotishia kutoka (threatened abortion)
Kwenye hali hii, mgonjwa hutakiwa
·
kupumzika kitandani bila
kufanya kazi yeyote (complete bed rest) angalau kwa wiki moja au zaidi mpaka hapo damu itakapoacha
kabisa kutoka
·
kumpa ushauri na uhakika
mama ili kumfanya atulie kiakili (assurance and proper councelling)
·
Mama pia hupewa dawa za
kumtuliza na kumfanya apumzike (sedatives) kama vile phernobabitone
·
Aidha mama hupewa dawa
kwa ajili ya kupunguza kusukuma kwa uterus (antispamodics) kama vile salbutamol
·
Kutofanya tendo la ndoa
kwa wiki mbili au tatu
·
Aidha mama na mumewe
hupewa ushauri juu ya tatizo hilo na jinsi ya kuendelea na matibabu
Matibabu ya mimba
iliyotoka kamili (complete abortion)
Mara nyingi mgonjwa huwa haitaji matibabu zaidi
ya uangalizi wa karibu kwa vile kiumbe pamoja na kondo lake la nyuma vyote huwa
vimetoka kikamilifu. Mara chache sana, kulingana na jinsi daktari atakavyoona,
mgonjwa anaweza kupewa antibiotiki kwa ajili ya kuzuia uwezekano wa kupata
maambukizi.
Matibabu ya utokaji wa
mimba usiokuwa kamili (incomplete abortion)
Matibabu ya aina hii ya utokaji wa mimba uhitaji
mgonjwa kusafishwa kwa ajili ya kuondoa mabaki ya kiumbe (products of
conception) yaliyobakia. Usafishaji huu huweza kufanywa kwa kutumia njia
inayoitwa Manual Vacuum Aspiration (MVA).
Aidha mgonjwa hupewa dawa za antibiotiki kwa
ajili ya kuzuia uwezekano wa maambukizi ya vimelea vya bakteria.
Matibabu mimba iliyotoka
bila kugundulika kuwa imetoka (missed abortion)
Matibabu ya aina hii ya utokaji wa mimba ni
pamoja na mgonjwa kuwekewa maji ya uchungu ili kiumbe kiweze kutoka. Wakati
mwingine, daktari anaweza kuamua kusafisha mfuko wa uzazi (uterus) kwa kutumia njia inayoitwa dilatation and
curettage. Sambamba na matibabu
hayo, mgonjwa pia hupewa dawa za antibiotiki kwa ajili ya kuzuia maambukizi ya
vimelea vya bakteria.
Matibabu ya tatizo la utokaji
wa mimba unaojirudia (recurrent abortion)
Jambo la msingi katika matibabu ya tatizo la
utokaji mimba unaojirudia (recurrent abortion) ni kugundua na kutambua chanzo kinachosababisha tatizo hilo na
kisha kukishughulikia ili kuondoa kabisa kujirudia rudia kwa tatizo hili.
0 comments:
Post a Comment