Monday, 5 May 2014

MATATIZO KATIKA SEHEMU ZA SIRI



Sehemu za siri ni zinazohusika na uzazi na mkojo kwa mwanaume na mwanamke. Kwa mwanaume, viungo vya uzazi vinatumika kwa malengo mawili. Kwanza ni utoaji wa mkojo na pili ni uzazi. Mwanamke katika sehemu zake za siri kuna sehemu ya kutolea mkojo na uzazi ambazo ni sehemu tofauti.
Matatizo yapo mengi kama utakavyokuja kuona. Matatizo yapo kwa nje na kwa ndani, matatizo katika sehemu ya mkojo ya mwanaume yanaweza kuathiri uzazi na matatizo katika sehemu ya uzazi wa mwanamke yanaweza kuathiri sehemu ya mkojo.
Matatizo katika sehemu za siri yanaweza kuwa ni maumivu, muwasho na kusinyaa. Matatizo yote haya yanaweza kuwapata wanawake na wanaume.

Matatizo kwa wanaume
Matatizo katika sehemu za siri za mwanaume yanaweza kuwa yale yanayoathiri ngozi mfano muwasho sehemu za siri, upele, vidonda, maumivu wakati wa kukojoa, maumivu ya korodani mara kwa mara, kupungukiwa nguvu za kiume na matatizo ya uzazi kwa kushindwa kuzalisha mbegu za uzazi.

Chanzo cha tatizo
Vyanzo vya matatizo haya ni vingi, magonjwa ya ngono kama Kaswende, Kisonono, magonjwa ya ngozi mfano fangasi na ukurutu. Matatizo katika  sehemu ya mkojo pia yanaweza kukusababishwa na vitu vingi mfano Yutiai, makovu ndani ya njia ya mkojo ambayo yanasababisha mkojo utoke kwa shida au kwa maumivu, uvimbe wa tezi dume (BPH) au saratani ya tezi dume.
Maumivu ya korodani yanaweza kuanzia hapo hapo kwenye korodani kwa kuumia au joto kali au kwa kuvaa nguo za kubana. Maambikizi kupitia njia ya mkojo pia yanaweza kujipenyeza na kuathiri mfumo wa uzazi kwa kuzorotesha uzalishaji wa mbegu za kiume.

Dalili za tatizo
Hakuna dalili moja au dalili maalum ya tatizo katika mfumo wa mkojo au mfumo wa uzazi. Hali ambayo si ya kawaida ambayo utaiona katika sehemu zako za siri ni dalili tosha ya matatizo haya katika sehemu za siri.

Uchunguzi
Vipimo mbalimbali vitafanyika kufuatana na hali inayojitokeza. Vipimo vya damu, mkojo au mbegu za kiume vitafanyika ili kuhakikisha tatizo ni nini.

Matatizo kwa wanawake
Matatizo kwa mwanamke ni kama vile yanavyojitokeza kwa mwanaume yaani inaweza kuwa muwasho kwa nje au ndani ukeni.
Mwanamke naye anaweza kupatwa na maumivu ya njia ya mkojo, kutokwa na vipele au vidonda  sehemu za siri. Anaweza kutokwa na vioteo sehemu za siri hali ambayo pia inaweza kumtokea mwanaume.
Mwanamke anaweza kutokwa na uchafu ukeni ukiambatana na muwasho na harufu, maumivu wakati wa tendo la ndoa na kupoteza raha na hamu ya tendo la ndoa. Mwanamke pia anaweza kupatwa na tatizo la kutofika kilele cha tendo la ndoa, kutokwa na damu wakati wa tendo la ndoa, kutokwa na usaha ukeni. Hali nyingine ambayo pia inaweza kuathiri mwanamke ni kuhisi joto na ganzi sehemu za siri.

Uchunguzi
Uchunguzi wa tatizo hili hufanyika kutokana na  jinsi mgonjwa anavyojihisi na kujiona katika maumbile yake ya siri.
Vipimo vya mkojo, damu, HVS na vya kuangalia ukeni hufanyika. Kipimo cha HVS ni cha kupima majimaji ya ukeni ili kujua chanzo halisi cha tatizo.

Athari za matatizo kwa mwanamke
Matatizo katika sehemu za nje ya uzazi yanaweza kusambaa hadi katika viungo vya uzazi vya ndani. Maambukizi haya yanapokuwa ukeni husambaa hadi katika mlango wa uzazi ambapo mwanamke hulalamika kupata maumivu baada ya kumaliza tendo la ndoa.
Baada ya hapo maumivu hupenya hadi katika tabaka la ndani la kizazi.


MATATIZO KATIKA SEHEMU ZA SIRI - 2

  Kutokwa na damu ukeni bila ya mpangilio (DUB).

ding. Chanzo chake ni ‘Hormonal Imbalance’ yaani vichocheo vya mwili haviendi sawa na husababishwa na mabadiliko katika mfumo wa homoni endapo mwanamke anatumia dawa za homoni kama sindano za kuzuia mimba, vipandikizi au kitanzi.
Ingawa njia hizi pia zinaweza kukufanya usipate damu lakini unaweza pia kupata bila ya mpangilio.
 Damu inaweza kutoka mfululizo na kwa muda mrefu au ikatoka kwa kukata au ikatoka wakati au baada ya tendo la ndoa.

Mara nyingi damu hii inapotoka huwa haina maumivu ila huwa nyepesi na mabonge kidogo na wakati mwingine hutoa harufu mbaya ingawa siyo mara zote.
Utokaji huu wa damu pia unaweza kusababishwa na uwepo wa uvimbe ndani ya kizazi, kuharibika kwa mimba, kuweka kitanzi au ‘loop’ na nyingine kama tulivyoona.

Maumivu wakati wa hedhi (Dysmenorrhoea)
Maumivu wakati wa hedhi yamegawanyika katika makundi mawili. Kwanza ni maumivu ya awali ‘Primary dysmenorrhoea’.

Hapa mwanamke hana historia ya maumivu ndiyo kwanza yanaanza, maumivu mengine ni ya baadaye ’Secondary Dysmenorrhoea’ ambapo mwanamke alishakuwa na maumivu siku za nyuma halafu yakaacha.

Chanzo cha maumivu hasa haya ya awali, huwatokea wasichana wanaotaka kuvunja ungo na kikubwa ni mabadiliko katika mfumo wa homoni ambapo kizazi kinashindwa kukua vizuri.
Maumivu ya pili ‘Secondary Dysmerrhoea’ kugeuka kwa tabaka la ndani la kizazi ‘Endometriosis’, tutakuja kulichambua matoleo yajayo na maambukizi sugu ya kizazi.

Kuvurugika kwa mzunguko wa hedhi (Irregular Cycle)
Kuvurugika huku husababishwa na matatizo katika mfumo wa homoni, matatizo ndani ya kizazi na hali ya kisaikojia.

Matatizo ya mfumo wa homoni tayari tumeyaona, matatizo ya ndani ya kizazi pia tumeyaona.
Matatizo ya kisaikolojia kama ‘stress’, mshtuko wa habari ya furaha au huzuni pia huharibu mzunguko. Mabadiliko ya hali ya hewa nayo huchangia.
Mwanamke ambaye mzunguko siyo mzuri kwanza hawezi kutumia njia ya uzazi wa mpango wa kalenda, pili anaweza asipate kabisa mimba hata akipangilia.

Kuvurugika kwa mzunguko ni pale mara mwezi huu mzunguko mfupi, mwezi mwingine kawaida yaani hauko sawa.
Mwanamke huyu anaweza kukuambia mfano mwezi huu nitaona tarehe kumi na tano, ghafla anaona tarehe sita.

Kutokwa na majimaji ya muwasho ukeni kabla na baada ya hedhi
Ni tatizo linaloweza kuumiza vichwa vya wanawake na hata wanaume. Mwanamke anakuwa na hali nzuri wakati wote lakini majimaji na muwasho huu huchangia mambo makuu mawili.
Kwanza ni maambukizi sugu ya kizazi, pili ni mwanamke mwenye kutozingatia usafi makini baada ya kumaliza ngono.

Uchunguzi
Vipimo mbalimbali hufanyika kutegemea na ukubwa wa tatizo. Vipimo vya damu Ultrasound na vingine vitafanyika kadiri daktari atakavyoona inafaa.
Uchunguzi wa masuala haya ya afya ya uzazi hupatikana katika kliniki ya magonjwa ya kinamama.

UShauri
Suala la afya ya uzazi hutegemea zaidi watu wawili, kabla mume na mke hamjaamua kutumia njia ya uzazi wa mpango wa asili, ni vema mkaifuatilia kwa umakini.
 Wahi hospitali kwa uchunguzi na tiba.

0 comments:

Post a Comment