Thursday 1 May 2014

MAMBO 10 AMBAYO UNGEPENDA UFAHAMU KUHUSU AFYA YA MENO YAKO.


 

watu wengi huwa na hofu ya sintofahamu
hasa wanapofikiria kwenda kumwona
daktari wa meno. mambo 10 yafuatayo
yatakusaidia sana kufahamu nini utarajie
unapokwenda kufuata uchunguzi wa afya
ya kinywa na meno ama matibabu ya
magonjwa ya kinywa na meno.

1. uchunguzi wa afya ya kinywa na
meno hujuimuisha uchunguzi wa kansa
kinywani
unapokwenda kwa daktari wa kinywa na
meno kwa uchunguzi wa kawaida wa
kinywa na meno (dental check up visit),
kwa kawaida daktari wa kinywa na meno
hutazama hali ya kinywa na meno pia
huchunguza uwepo wa dalili za kansa
kinywani. inakadiriwa kuwa mtu mmoja
hufa kila saa la kutokana na ugonjwa wa
kansa kinywani huko marekani. ugonjwa
huu hatari unaoshambulia zaidi kuta za
kinywa, midomo-hasa mdomo wa chini-
pamoja na koo unatibika ikiwa
utatambuliwa mapema na kutibiwa
kikamilifu.
 
 hivyo, kumwona daktari wa meno walau
mara mbili kwa mwaka (kila baada ya
miezi sita) na kuepuka matumizi ya
tumbaku/sigara vitakuwezesha kujikinga
na ugonjwa wa kansa ya kinywa na
madhara yake.

2. magonjwa ya fizi huathiri afya ya
mwili kwa ujumla

magonjwa ya fizi na meno ni chanzo kikuu
cha kupoteza meno kwa watu wenye umri
mkubwa/watu wazima, na pia magonjwa
haya huhusishwa na magonjwa ya moyo
na kiharusi (stroke).
ikiwa magonjwa haya ya fizi
yatatambuliwa mapema (gingivitis),
yanatibika vizuri na kuepusha madhara
zaidi.

 
 ikiwa tatizo hili halitopata tiba mapema,
ugonjwa hukomaa zaidi (periodontitis)
ambapo mfupa unaoshikilia jino/meno
hushambuliwa na kuharibiwa.
kusafisha meno kwa kupiga mswaki mara
mbili kwa siku, matumizi ya nyuzi-safishi
(dental floss), kumwona daktari wa meno
kwa uchunguzi mara kwa mara na
kusafisha meno kitaalamu kwa tatibu wa
meno, kutasaidia kuepuka madhara ya
magonjwa ya fizi.
 
 3. uchunguzi wa kinywa na kusafisha
meno kitaalamu ni tiba muhimu zaidi

ni wangapi kati yetu wenye desturi ya
kumwona daktari wa meno walau mara
mbili kwa mwaka (walau kila baada ya
miezi sita)? mara nyingi wengi wetu
huhangaika na foleni za kumwona daktari
wa meno pale tu tunaposumbuliwa na
maumivu ama ya jino ama kidonda
kinywani ama kwa sababi ya hali zinginezo
zinatotulazimisha kumwona daktari wa
meno.

 
 kusubiri mpaka tusukumwe na maumivu
ya meno/kidonda kinywani ama ajali
yoyote kunatunyima fursa bora zaidi ya
kuchunguzwa afya ya kinywa na meno na
kusafishwa meno ili kuepusha madhara ya
magonjwa ya kinywa na meno kabla
hayajatokea ama kukomaa.

4. kupiga mswaki mara mbili kwa siku
kunaepusha kuoza kwa meno.
 
 kupiga mswaki kwa ufanisi walau mara
mbili kwa siku huondoa ukoko
unaogandiana kinywani na kusababisha
kuoza kwa meno. ukoko huu ni ute laini
unaoganda kwenye sehemu mbalimbali za
jino/meno
huku ukiwa na mamilioni ya vimelea vya
magonjwa (bakteria). matumizi ya nyuzi-
safishi (dental floss) kila
siku husaidia kuondosha ukoko maeneo
ambako mswaki haufiki, vile vile
kuondosha ukoko huu kunasaidia
kujikinga na magonjwa ya fizi.

5. magonjwa ya kinywa na meno
husababisha harufu mbaya mdomoni

takribani asilimia 85 ya watu wenye
harufu mbaya kinywani huwa na
magonjwa ya kinywa na meno,ikiwa
harufu mbaya kinywani inasababishwa na
magonjwa kinywani, dawa za kusafisha
kinywa (mouthwash) haziwezi kuondoa
tatizo zaidi ya kulifunika kwa muda tu.

 
 hakuna sababu ya kuona haya
kumwambia daktari wa meno kuhusu
harufu mbaya kinywani inayokusumbua,
kwa vile kumwambia na kujadili tatizo lako
ni njia ya kuelekea kwenye tiba ya uhakika.
matumizi ya nyuzi-
safishi (dental floss) kila siku, kusafisha
meno na ulimi kwa mswaki walau mara
mbili kwa siku yaweza kuondoa harufu
mbaya kinywani kwa kiasi kikubwa.

6. chakula bora ni muhimu kwa afya
bora ya kinywa na meno

ulaji wa vyakula na vinywaji vyenye sukari
na visivyo na virutubisho vya mwili
vinapochanaganyikana na vimelea vya
magonjwa (bakteria) hutengeneza tindikali
ambayo hushambulia ukuta wa nje wa jino
(dental enamel). kushambuliwa kwa
enameli na tindikali husababisha mashimo
kwenye meno na magonjwa ya fizi.
kudhitibi na kupunguza ulaji wa vyakula
vyenye sukari kwa wingi itakuepusha na
magonjwa ya kinywa na meno.

7. bila matibabu, magonjwa ya kinywa
na meno hayaponi wala kupata nafuu

pale daktari wako wa meno anapokupa
mpango makakati wa matibabu ya kinywa
na meno yako, jukumu lako
ni kuzingatia maagizo na maelekezo ya
daktari ili upate matokeo mazuri.
inapotokea una mashimo makubwa
kwenye meno, bado inawezekana kutibu
meno kuanzia kwenye mzizi kabla meno
hayajang'olewa.

8. tiba ya mzizi wa jino haina maumivu
amini usiamini,
sio jambo la kustaajabisha
kusikia mgonjwa aking'ang'ania jino
ling'olewe kwa madai kuwa matibabu ya
jino kuanzia kwenye mzizi wake ni yenye
maumivu ya kupindukia, yasiyovumilika.
ukweli ni kwamba, maendeleo ya
teknolojia tiba yamefanya matibabu ya jino
kuanzia kwenye mzizi kuwa rafiki na
rahisi, tena hayana sifa yoyote ya maumivu
makali kupindukia kama ambavyo watu
wengi wanaamini, tiba hii ni moja ya tiba
rafiki sana kwenye ulimwengu wa
matibabu ya kinywa na meno.
 
 9. badili mswaki mara kwa mara
umri wa miswaki tunayotumia unapaswa
kuwa miezi mitatu (siku 90),
 baada ya
muda huu ufanisi wa mswaki hupotea.
ikiwa unasumbuliwa na magonjwa ya fizi
unashauriwa kubadili mswaki kila baada
ya majuma manne
hadi sita (wiki 4 – 6), kwa sababu vimelea
vya magonjwa (bakteria) hijificha kwenye
brush za mswaki. vile vile unashauriwa
kuosha mswaki wako kwenye maji ya
moto kila baada ya kuutumia na
kuubadilisha kila unapopata mashambulizi
ya ugonjwa wa fizi.
 
 10. ni rahisi sana kutunza afya ya
kinywa na meno.

watu wengi hifikiri kuwa kuwa na afya
bora ya kinywa na meno kunahitaji
jitihada za ziada, ukweli ni kuwa,
kumwona daktari wa meno mara kwa
mara (walau mara mbili kwa mwaka kila
baada ya miezi sita), na
kusafisha meno kitaalamu, kupiga mswaki
walau mara mbili kwa siku (asubuhi baada
ya kupata kifungua kinywa, na usiku kabla
ya kulala), kutumia nyuzi-safishi (dental
floss),
ulaji wa chakula bora chenye
virutubisho ni vigezo muhimu sana vya
kuwa na afya njema ya kinywa na meno,
sasa ugumu upo wapI?

0 comments:

Post a Comment