Saturday, 3 May 2014

MALARIA UGONJWA UNAOWAUMIZA VICHWA WANASAYANSI



Malaria ni ugonjwa unaoathiri watu wengi duniani ikiwamo Tanzania.  Ugonjwa huo husababisha vifo vya watu milioni 2.7 kote duniani, ambapo vifo vingi hutokea barani Afrika.
Ugonjwa wa malaria huonekana katika nchi 100 duniani na umeshaleta athari kubwa hasa kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano.
Kwa upande wa Tanzania, mikoa ambayo inayoongoza kwa maambukizi ya malaria ni Kagera (41.1%), Lindi (35.5%), Mtwara (36.6%), Mwanza (31.4%), Mara (30.3%).
Mikoa ambayo  maambukizi ya malaria ni kidogo  ni Manyara (1%), Kilimanjaro (1%) na Dar-es-Salaam (1.2%). Visiwani Zanzibar, maambukizi ya malaria ni kwa asilimia 0.8.
Malaria huonekana zaidi katika Ukanda wa Tropiki. Ugonjwa huu wa malaria uligunduliwa mwaka 1880 na Charles Louis Alphonse Laveran, katika Hospitali ya Jeshi ya Constatine, Algeria, baada ya kuona vimelea vya plasmodium, kutoka kwa mgonjwa aliyefariki kwa ugonjwa huo.
  Malaria ni kati ya magonjwa ya maambukizi ambao husababishwa na vimelea vya plasmodium, ambavyo humfikia binadamu kupitia kung’atwa na Mbu jike wa aina ya anopheles.
Hivi karibuni watafiti wamebaini kuwepo kwa vijidudu vya malaria ambavyo haviteketezwi na dawa za malaria zilizopo.
Vijidudu hivyo vimepatikana magharibi ya nchi ya Cambodia nani tofauti na vijidudu vingine duniani.
Imeelezwa kuwa vijidudu hivyo vimekuwa sugu hata kwa dawa bora dunini ya artmisinin.
Plasmodium falciparum - Hupatikana sana katika nchi zilizopo katika jangwa la sahara.
Asilimia 75 ya wagonjwa wote wa malaria barani Afrika husababishwa na vimelea hivi. Mwaka 2006, kati ya watu 
milioni 247 duniani waliougua malaria, asilimia 91 walisababishwa na vimelea hivi (Afrika 98%) na kusababisha vifo kwa asilimia 90 mwaka huo huo barani Afrika.
Plasmodium malariae - Hawa hupatikana katika nchi zilizopo katika Jangwa la Sahara, Asia ya Mashariki, 
Indonesia na katika visiwa vya magharibi mwa Pacific. Kati vya vimelea vyote vya malaria, plasmodium malariae ndio huonekana kwa uchache zaidi.
Plasmodium ovale - Hupatikana zaidi Afrika Magharibi, Ufilipino, Mashariki mwa Indonesia, Papua New Guinea, Cambodia, Bangladesh, India, Thailand na Vietnam.
Plasmodium vivax - Huonekana katika bara la Marekani, Latin Amerika na baadhi ya sehemu za bara la Afrika.
Plasmodium knowlesi - Hupatikana katika bara la Asia ya mashariki katika nchi za Bormeo, Myanmar, Malaysia, Ufilipino, Singapore na Thailand. Haipatikani katika bara la Afrika.
Mzunguko wa maisha ya vimelea vya malaria
Mwenyeji wa msingi ya vimelea vya malaria ni mbu aina ya anopheles wa kike, ambae pia ni msambazaji, na binadamu ni mwenyeji wa kati.
Mbu anapokuwa anajipatia chakula kwa kunywa damu kwa kumuuma binadamu mwenye maambukizi ya vimelea vya malaria, ndio mzunguko wa kwanza huanza.
‘Gametocyte’ za vimelea vya plasmodium hugawanyika ndani ya mbu na  kutengeneza gametocyte za kike na za kiume 
na baada ya hapo gametocyte hizo za kike na za kiume, hujiunga ndani ya mfumo wa chakula wa mbu na 
kutengeneza Ookinete ambayo hupenyeza kwenye kuta za mfumo wa chakula na kutengeneza Oocyst nje ya ukuta wa mfumo wa chakula.
Hapo hupasuka na kutengeneza sporozoites na kuhamia kwenye tezi za mate za mbu, na kuwa tayari kuambukiza binadamu mwengine pindi mbu anapojitafutia chakula.
Kwa mbu jike damu ndiyo lishe yake wakati dume lishe yake ni nekta ya mimea, hivyo mbu dume hasambazi ugonjwa huu.
Hivyo basi, mbu jike aina ya anopheles ndiye anayeambukiza ugonjwa wa malaria  na hupenda kujipatia lishe kipindi cha usiku.
Maambukizi ya malaria yanaweza kupatikana kwa kuongezewa damu ingawa ni nadra sana.

Kwa Binadamu pindi anapong’atwa na mbu hupata maambukizi kupitia mate ya mbu, na vimelea vya plasmodium huingia kwenye damu na kuelekea kwenye ini na baadaye kwenye damu.
                              
Dalili zake
·       Homa
·         Maumivu ya kichwa
·         Kichefuchefu
·         Kutapika
·         Maumivu ya misuli
·         Manjano
·         Degedege
·         Kupoteza fahamu
·         Kukua kwa wengu
·          
Dalili za mwanzo hutokea kati ya siku 10 hadi wiki 4, na dalili nyingi hutokea pale hatua ya merozoites inapoachiwa nyingi kwenye damu baada ya schizonts kupasuka.
Madhara ya malaria
·         Malaria ya kichwa (cerebral malaria) huweza kusababisha magonjwa ya akili.
·         Mishipa ya damu kupasuka na kusababisha kifo.
·         Matatizo ya kupumua (pulmonary edema)
·        
 Viungo kushindwa kufanya kazi (organ failure)
·         Upungufu wa damu
·         Upungufu wa sukari mwilini (hypoglycemia)
·         Shinikizo la chini la damu (hypotension)
·         Haemoglobinuria
Vipimo na uchunguzi
·       Kipimo cha damu na kutumia hadubini
·       Thin film--hutumika kutambua aina ya vimelea vya plasmodium (falciparum,ovale,vivax,malariae)
·       Thick film---hutumika kutambua idadi ya vimelea/µL
·       Kipimo cha damu bila kutumia darubini
Malaria Rapid Diagnostic Test
PCR
Matibabu
Dawa za malaria
Mstari wa kwanza (dawa mseto)
Artemether plus Lumefantrine
Dihydroartemisinin plus Piperaquine
Mstari wa Pili
Amodiaquine
Mstari wa tatu
Quinine
Dawa za kushusha homa na maumivu
Dawa za maumivu kwa mfano, Paracetamol
Kama sehemu ya tiba, mgonjwa anashauriwa pia kula na kunywa maji ya kutosha.
Jinsi ya kuzuia maambukizi ya malaria
·       Kuzuia mazalio ya mbu
Fyeka vichaka na ondoa madimbwi ya maji katika  maeneo yanayokuzunguka.
Kuzuia kung’atwa na mbu
·       Matumizi ya vyandarua vyenye dawa ya kuua mbu
·       Matumizi ya dawa za kupulizia za kuua mbu majumbani
·       Matumizi ya dawa za kupaka za kuua mbu.
·       Dawa za kuzuia malaria kwa wasafiri watokao nchi sizizo na malaria.
Proguanil
Malarone
Mefloquine
·       Dawa za kuzuia malaria kwa kina mama wajawazito (IPT)

Sulfadoxine Pyrimethamine (SP) hutolewa kwa kina mama katika wiki ya 20 na wiki ya 36 ya ujauzito.

0 comments:

Post a Comment