Ndugu msomaji nimeona ni muhimu kuandika tofauti ya ugonjwa wa
kaswende na kisonono kwa sababu kumekuwa na idadi kubwa ya wagonjwa ambao
wanapotoa maelezo au malalamiko yao wamekuwa wakichanganya ugonjwa wa kaswende
na kisonono.
Kawaida daktari anatakiwa amsikilize mgonjwa anavyojieza kuhusu
anavyojisikia kwa wakati huo, alianza kuumwa vipi na magonjwa mengine aliyowahi
kuumwa hapo nyuma. Maelezo haya kutoka kwa mgonjwa, na majibu mengine
atakayojibu baada ya kuhojiwa na daktari humsaidia daktari kujua vipimo vya
aina gani akufanyie ili aweze kuelewa una ugonjwa gani na uko katika hatua gani
ili kukupa matibabu yanayostahili.
Inapotokea mgonjwa akatoa maelezo ambayo si sahihi, inaweza
kumfanya daktari atoe matibabu ya ugonjwa totafuti na ule unaaumwa na matokeo
yake ni kuendelea kuumwa na kuzababisha usugu wa ugonjwa kwa baadhi ya dawa.
Kisonono ni ugonjwa tofauti na kaswende kwa njia mbalimbali kama
ifuatatavyo; kwanza kabisa tofauti kubwa ni dalili za magonjwa haya, Kisonono
kina dalili ya kutokwa na usaha sehemu za siri ambao huambatana na maumivu
makali sana wakati wa kukokojoa kwa wanaume na wanawake husikia mkojo kuchoma
sana wakati wanapokojoa.
Kwa watoto wanaozalia na mama mwenye ugonjwa wa kisonono, mtoto
atazaliwa na ugojwa wa macho kwa kutokwa na matongotongo mengi na macho kuwa
mekundu kwa sababu ya kushambuliwa na bakteria wa kisonono. Ukweli Kisonono
hutambulika mapemba kuliko kaswende kwa sababu dalili zake ni bayana na
zinamlazimisha mgonjwa kwenda hospitali au kununua dawa kutuliza maumivu.
Kaswende tofauti na kisonono dalili zake ni za kuota vipele
mwilini na hata uambukizaji wake ni zaidi ya kisonono, japo magonjwa yote
yanaweza kuambukizwa kwa njia ya kujamiiana, Kaswende inaweza kuambukizwa kwa
kugusa majimaji yanayotoka kwenye vipele vya mgonjwa wa kaswende.
Hata kuchangia taulo au shuka na mgonjwa huyo unaweza kupata
maradhi hayo iwapo majimaji yanayotoka kwenye vipele hivyo, yamegusa ngozi
yako. Wadudu wa kaswende wanaweza kupenya ngozi ya kawaida tofauti na magonjwa
kama UKIMWI ambayo yanahitaji kuwepo michubuko ili yaingie mwilini.
Dalili za kaswende ni hatari sana kwani ugonjwa zaidi ya vipele
huendelea kukua ndani kwa ndani bila kujua na dalili kubwa zinajitokeza wakati
ugonjwa umefikia hatua ya juu.
Dalili hizi ni pamoja kuongezeka kwa vipele sehemu za siri na
mwili mzima, kwa kina mama mimba hutoka mara kwa mara na kwa wale
watakaojifungua salama basi utakuta mtoto ana kasoro za maumbile. Kaswende
imeishawafanya wengi kuishia kuwa vichaa na kuokota makopo barabarani
Hata hivyo njia za kuyaepuka magonjwa haya zinafanana sana;
Kuacha kufanya ngono ni bora kuliko kupata magonjwa haya mawili, hii
itakusaidia kuwa na nafasi ya kujipanga na kutafuta mpenzi au mchumba na wakati
utakapofika mnakubaliana maisha ya pamoja na kuwa na mahusiano ya ngono yaliyo
salama.
Kuwa na mpenzi mwaminifu ni muhimu sana, kama wote mtatunziana
heshima na asiingizwe mtu wa tatu katika mahusiano yenu ya kingono basi ujue
kuwa magojwa hayo mtayasikia kwa wengine kwani nyie mkiwa salama itaendelea
hivyo maisha yenu yote.
Mwisho nasisitiza matumizi sahihi na ya mara kwa mara ya mpira
wa baba au wa mama maarufu kama kondomu. Hii imeishawasadia wengi sana, kondomu
zinazuia magonjwa ya zinaa na hata mimba zisizotarajiwa. Hivyo basi, tujitahidi
kuuliza na kuzijua dalili za magonjwa mbalimbali ili tusiwachanganye madaktari
wanapotuhudumia.
0 comments:
Post a Comment