Katika makala yetu Leo hii tunaangalia maradhi ya
fangasi yanayoshambulia kichwa au mapunye ambayo kitaalam huitwa Tinea capitis.
Mapunye au Tinea Capitis ni nini?
Aina hii ya maradhi ya fangasi hushambulia eneo la
kichwa pekee ukiacha eneo la uso. Kwa maneno mengine, aina hii ya fangasi
haishambulii uso bali hushambulia eneo lililobaki la kichwa.
Huwashambulia kina nani?
Haya hushambulia watu wote wa jinsia na umri wote,
ingawa huonekana zaidi kwa watoto wadogo. Fangasi hawa hushambulia watoto
wadogo ambao hawajafikia umri wa balehe na mara nyingi huacha kushambulia pale
mtoto anapofikia umri huo wa balehe.
Mwonekano wake
Mapunye huweza kushambulia eneo lote la kichwa au
sehemu tu ya kichwa. Eneo la ngozi ambalo lina mashambulizi ya mapunye huwa na
umbo linalofanana na sarafu.
Eneo hili la ngozi lililoathirika kama lina
nywele, basi hunyonyoka na hivyo mwonekano wa mfano wa sarafu huonekana vizuri
tu hata bila kutumia jicho la kitaalam.
Dalili zake
Ukiachilia mbali mwonekano wa mapunye kama
nilivyoeleza hapo juu kuna dalili nyingine za maradhi haya. Hizo ni:
-Eneo la ngozi lililoshambuliwa kuwasha (ingawa si
mara zote)
-Kubadilika kwa rangi ya ngozi ya eneo lenye
maambukizi
-Ukitazama kwa makini eneo ambalo lina mashambulizi ya
maradhi haya utagundua kuna vidoti vyeusi ambavyo vinaonyesha eneo ambalo
nywele imeng`oka kutokana na maradhi.
-Ngozi kubanduka kwenye eneo lenye maambukizi
-Ngozi kukauka kwenye eneo lenye maambukizi
-Mara nyingine usaha pia huweza kuonekana kwenye eneo
la ngozi lililoshambuliwa na fangasi hawa (hii kwa kitaalam huitwa kerions)
-Kama maradhi haya yakikaa bila kutibiwa kwa muda
mrefu husababisha dalili nyingine kuonekana kama kutoka kwa maji maji kwenye
eneo la ngozi lililoathirika pamoja na kutoka kwa harufu mbaya kwenye eneo la
ngozi lililoathiriwa na vimelea hivi vya fangasi.
Yanavyosambaa
Kuna njia nyingi zinazoweza kusababisha uambukizi wa
mapunye lakini ili uambukizaji huu uwezekane lazima kuwa na mazingira rafiki ya
kuwezesha fangasi kuweza kuishi na kuhama kwa urahisi. Mazingira haya rafiki
kwa kuruhusu fangasi hawa kuweza kutoka kwenye kichwa cha mtu mmoja kwenda kwa
mwingine huhitaji uwepo wa hali ya joto pamoja na majimaji (unyevunyevu).
Huwa ni rahisi sana kwa mapunye kuambukizwa kutoka
kwenye kichwa cha mtu mmoja kwenda kwa mwingine kwa njia hizi:
-Kutumia vifaa vya kunyolea kwa zaidi ya mtu mmoja
bila kuvifanyia usafi wa kuua vimelea kama fangasi wa aina hii
-Kutumia taulo au nguo ya kujikaushia kwa mtu zaidi ya
mmoja hasa pale ambapo mmoja wa watumiaji hao ana maambukizi ya fangasi.
-Kutumia vifaa vya nywele kama chanuo la kuchania
nywele kwa zaidi ya mtu mmoja hususani pale ambapo mmoja wa watumiaji hao ana
maambukizi ya vimelea vya fangasi hao.
-Kugusana na mtu aliye na maambukizi tayari
-Kushirikiana mavazi aina ya kofia na mtu aliyekwisha
pata maambukizi hayo
Ni nani yuko hatarini?
Watu ambao huweza kupata maambukizi ya mapunye ni
wafuatao:
-Wale wanaoshirikiana na wenzao vifaa vya kunyolea
bila kuvisafisha vizuri
-Wanaoshirikiana vifaa vya kufanya usafi wa mwili
zikiwamo taulo
-Wanaotoka jasho hasa kichwani kwani huweza kuweka
mazingira mazuri zaidi kuruhusu maambukizi yatokee kirahisi
-Wanaofanya kazi zinazohusisha uwekaji vichwa kwenye
maji yaliyotuama kwa muda mrefu
-Wale ambao tayari wana fangasi za kichwani
kwani ni rahisi kwa fangasi hao kujirudia.
-Wanaofanya usafi wa mwili kwa kutumia maji yaliyobeba
vimelea
-Wasiojikausha vichwa baada ya kuoga au kufanya usafi
wa kichwa
-Watu wenye maradhi yanayosababisha kushuka kwa
kingaikiwamo kisukari.
-Wale wanaokunywa dawa za kuua vimelea (antibayotiki)
kwa muda mrefu
-Watoto wadogo ambao hawajafikia umri wa balehe.
Jinsi ya kuyatambua
Mara nyingi aina hii ya fangasi hugundulika kwa macho
hasa kwenye maeneo ambayo fangasi hao wapo kwa wingi. Kwa kutazama
ngozi ya sehemu ya kichwa iliyoathirika na maambukizi ya fangasi hao, utaweza
kuona madhara yanayokukabili.
Kwenye uhitaji wa vipimo basi sehemu ya ngozi
iliyoathirika huchukuliwa kwa ajili ya kufanya vipimo vya maabara na kuangalia
aina sahihi ya fangasi.
Matibabu
Mara nyingi mapunye hutibika kwa dawa za kutibu
fangasi za kupaka ambazo hutibu mapunye na kuyaponyesha kabisa bila kuhitaji
kutumia dawa za kumeza. Hii ni kwa kuwa ni rahisi kwa dawa ya kupaka kupenya
kwenye ngozi na kusababisha matokeo yanayohitajika.
Matibabu ya mapunye huchukua muda mfupi kuonyesha
matokeo mazuri au
Matokeo chanya mara zote, ila pia huwa ni rahisi kwa
maradhi hayo kurudi baada ya kumaliza matibabu kama hatua madhubuti za kujikinga
na maradhi haya hazitochukuliwa.
Kwa sababu hiyo, ni vizuri kwa mgonjwa wa
fangasi kutumia dawa mpaka wiki mbili baada ya dalili za maradhi kutoweka.
Pia, ni vizuri dawa zake ukashauriwa na daktari
Kulingana na jinsi ulivyoathirika na Mapunye hayo.
Jinsi ya kujikinga
Kuna mbinu mbalimbali za kujilinda usipatwe na
fangasi:
-Hakikisha mwili wako hasa kichwani yanabaki na ukavu
muda wote
-Osha nguo, taulo na mashuka kuhakikisha fangasi
wanaondolewa
-Epuka kushirikiana vifaa vya kunyolea nywele hasa kama
hakuna namna ya kuvisafisha na dawa maalum ya kuua vimelea kabla hujatumia
-Epuka kushirikiana katika utumiaji wa vifaa vya
kufanya usafi wa mwili kama mataulo. Kama kazi yako inahusisha ukaaji wa
muda mrefu kwenye maji basi hakikisha unakausha mwili hasa sehemu za
kichwa au uweke dawa ya kuzuia fangasi kwenye maji hayo.DAWA YA MAPUNYE KWENYE KICHWA FANYA HIVI:
(1) Ndimu au limau: Kabla kwenda kukoga jisugue limau ndani ya kichwa na baadae yale maganda ya limau yatie katika maji ya kukoga yaani yawe maji ya Uvuguvugu halafu ukoshe kwa maji yale kwanza na baadae utumie maji yaliyo safi.
(2) (Fenugreek) kwa lugha ya kiswahili inaitwa Uwatu. Uwatu unachukua vijiko 2 vya chai vya Uwatu (fenugreek) unazirowesha katika maji usiku mzima ili zipate kulainika, halafu unazipoda ponda na baadae unapakaa ndani ya kichwa na uwache kwa muda wa saa moja na baadae kuzikosha ikiwa utafanya hivi siku zote mbaa wataondoka Inshallah bila tabu yoyote.
(3) DAWA YA MAPUNYE AU MASHILINGI: Chukua magamba ya parachichi anika juani halafu kisha yatwange ule unga wake changanya na mafuta ya Zaituni,kosha sehemu ile na maji ya uvuguvugu halafu pakaa ule unga mara tatu kwa siku 7,Utapona..
0 comments:
Post a Comment