Saturday 3 May 2014

UFAHAMU UGONJWA WA MALALE TRYPANOSOMA





MALALE ni ugonjwa wa kusinzia
unaosababishwa na vimelea aina ya
protozoa vinavyojulikana kama ndorobo.
Kitaalamu hujulikana kama “Trypanosoma”.
Kwa mujibu wa Wataalamu wa ugonjwa huo

Kuna aina mbili za
ugonjwa wa malale kwa kutegemeana na
aina ya ndorobo.
Wataalamu anafafanua kuwa, ugonjwa huo
kwa binadamu huitwa malale na kwa
mnyama hujulikana kama nagana.

Anasema ugonjwa huu
husababishwa na ndorobo wajulikanao
kitaalamu kama ‘Trypanosoma brucei
rhodesiense’ na kwamba aina hii
hupatikana Mashariki na Kusini mwa Afrika
ikiwemo Tanzania.
Na kwamba idadi ya matukio ya wagonjwa
wa ndorobo kali kwa sasa ni ndogo.

Anasena aina ya pili ya ugonjwa huo ni
malale isiyo kali ambayo husababishwa na
ndorobo anayejulikana kitaalamu kama
‘Trypanosoma brucei gambiensen’ ambaye
hupatikana kwenye nchi zilizo Kusini mwa
Jangwa la Sahara.
Wanaelezea nchi zilizoathirika sana na malale
isiyo kali ni Jamhuri ya Congo, Angola,
Jamhuri ya Afrika ya Kati, Uganda na Sudan
ya Kusini.

 
Wataalamu wanasema uwepo wa malale
una uhusiano na mtawanyiko wa mbung’o.
Hivyo kwa kuwa hali ya hewa hairuhusu
mbung’o kuishi katika baadhi ya maeneo
barani Afrika, ugonjwa wa malale umejikita
kati ya latitude 14 kaskazini na latidude 29
kusini mwa Bara la Afrika.

Wataalamu wakizungumzia ukubwa wa ugonjwa
 huo
Afrika, mtaalamu huyo anasema inakadiriwa
kuwa watu milioni 60 wapo katika hatari ya
kupata maambukizi ya malale katika nchi 37
za Bara la Afrika.
Anaeleza kwamba takriban kilometa za
mraba milioni 10 zimeathiriwa na mbung’o,
watu kati ya milioni 4 hadi 5 pekee hufikiwa
kwa uchunguzi na kitabibu.

Hapa nchini kwetu, wataalamu wa Afya
Kuhusu
malale anasema kwa mara ya kwanza,
ugonjwa huo umeripotiwa 1922 wilayani
Maswa na baadaye kuenea mikoa ya Arusha,
Lindi, Ruvuma, Kagera, Kigoma, Tabora,
Mbeya na Rukwa.
Anasema katika historia idadi wa wagonjwa
kwa mwaka imekuwa ikikadiriwa kuwa
3,262 mwaka 1929 hadi 306 kwa mwaka
1937.
Anasema takriban asilimia 65 ya eneo
linakariwa kuwa na mbung’o na watu
milioni nne wapo katika hatari ya kupata
maambulizi ya ugonjwa huo.

Mwaka 1996 kulikuwa na
wagonjwa 380, mwaka 1997 ilishuka na
kufikia 351, mwaka 1998 walikuwa 291
wakati mwaka 2007 walikuwa 125.
Anasema mwaka 2008 kulikuwa na
wagonjwa 55, mwaka 2009 walikuwa 10,
mwaka 2010 walikuwa watatu na mwaka
jana idadi ilipungua na kufikia wawili.
(takwimu hizi ni kwa mujibu wa wizara ya afya na
ustawi wa jamii)

Ugonjwa huo huenezwa na
mbung’o anapofyonza damu kutoka kwa
wanyama au binadamu mwenye vimelea vya
ndorobo.

 
Shughuli zinazosababisha jamii
kupata ugonjwa huo kuwa ni urinaji asali,
uchotaji maji kwa wanaofanya shughuli
hiyo hasa kwenye mito yenye mbung’o,
ukataji mbao, uchomaji mkaa na
utengenezaji barabara kwenye maeneo
yenye mbung’o.

Nyingine ni uvuvi, ufugaji na ukulima, utalii,
ufanywaji kazi kwenye hifadhi za taifa,
uwindaji na uchimbaji madini.

 
 Dalili za awali huanza kati ya siku
7 hadi 14 baada ya kuumwa na mbungó
mwenye vimelea, ambazo ni uvimbe na
kuwashwa sehemu iliyoumwa, kuumwa
kichwa, homa za mara kwa mara, maumivu
ya misuli na viungo, mapigo ya moyo
kwenda kasi na kupoteza hamu ya kula.

Baada ya dalili za mwanzo kati ya
miezi miwili hadi mitatu dalili za kulala mara
kwa mara wakati wa mchana hujitokeza.
Dalili nyingine ni kukosa usingizi nyakati za
kati wa usiku, kushindwa kutembea vizuri,
kuchanganyikiwa, kupungukiwa uzito
kusiko kwa kawaida, kupoteza fahamu na
kushindwa kuongea vizuri.

 
 Athari za kiuchumi zinazojitokeza ni
kupungua nguvu kazi kutokana na ugonjwa
na vifo hususan maeneo ya vijijini, kuathiri
sekta ya utalii, ardhi iliyokaliwa mbungó
kutotumika kwa makazi, ufugaji au kwa
kilimo.

Nyingine ni gharama kubwa kwa serikali
kuhudumia wagonjwa wanaolazwa na
ongezeko la matumizi ya fedha katika kaya.
Kwa upande wa athari za kijamii, mgonjwa
kuathirika kisaikolojia, kuathirika kwa
mfumo wa fahamu hata baada ya tiba,
unyanyapaa, mgonjwa kuwa tegemezi kwa
familia na wakati mwingine hali hiyo
huchangia ndoa kuvunjika.

Njia za kuuzuia ugonjwa
huo kuwa ni kuchunguza na kutoa tiba kwa
mifugo kuua vimelea wa ndorobo kabla
kuwahamisha kutoka sehemu moja kwenda
nyingine.

Kufunga vioo vya gari unapofika ama
kutembelea eneo lenye mbung’o, kuepuka
kuvaa nguo zenye rangi nyeusi na bluu
kwani huvutia mbung’o kuuma.

Pia, Njia zinazohitaji
kuchukuliwa kuwa ni kuogesha mifugo na
viuatilifu vinavyoua mbung’o, kupuliza
viuatilifu vya kuua mbung’o maeneo
waliopo kwa kutumia ndenge au ‘’fogging
machine’’ na kutumia madume ya mbung’o
yanayohasiwa.

 
 Nyingine ni kuondoa vichaka vilivyozunguka
eneo la nyumba ili mbung’o wasijifiche,
kupima afya yako unapohisi homa baada ya
kutembelea maeneo yenye ugonjwa wa
malale, wamba vyambo (vitambaa) vyenye
viuatilifu vya kuua mbung’o, kutega mitego
ya kukamata wadudu hao na kuogesha
mifugo kwa kutumia viuatilifu.

Serikali imefanya jitihada za kutengeneza
miongozo ya uchunguzi na tiba ya malale,
kutoa mafunzo juu ya uchunguzi na utoaji
wa tiba ya malale, kuhakikisha kuwa dawa
kwa ajili ya tiba kwa ugonjwa zinapatikana.

 
 Nyingine ni kusambaza vitambaa
vilivyowekwa viuatilifu kuua mbung’o
mbuga za taifa na maeneo mengine.
Mafanikio yaliyopatikana ni kuanzishwa kwa
vituo ‘surveillance site’ kwa ajili ya kufuatilia
mwenendo wa ugonjwa huo, kushirikisha
wadau mbalimbali kukabiliana na mbung’o,
kuelimisha jamii kuwa na uelewa juu ya
ugonjwa huo, kushirikiana na taasisi za
utafiti kukabiliana na ugonjwa huo na
nagana.

Mengine ni kupungua kwa idadi ya
wagonjwa kutoka katika miaka ya 2000 na
kufikia wagonjwa 386 hadi kufikia
wagonjwa wawili mwaka jana, mgonjwa
mmoja hadi Juni mwaka huu.

Mafanikio mengine ni kupungua kwa
ukubwa wa eneo lenye mbung’o kutoka
asilimia 65 (1973) ya eneo la nchi na kufikia
asilimia 45 (2012), kufanikiwa kuangamiza
mbung’o na nagana Kisiwa cha Unguja kwa
kutumia madume ya mbung’o yaliyohasiwa.
Anaelezea changamoto zilizojitokeza kuwa
ni uhamishaji holela wa mifugo kutoka
sehemu zenye maambukizi kwenda eneo
lisilokuwa na maambukizi, uchungaji wa
mifugo ndani au karibu na mbuga za
wanyama, uchache vituo vyenye uwezo wa
kutoa tiba ya malale, dalili zake kufanana na
magonjwa mengine kama malaria, ukimwi,
na kifua kikuu.

 
 Mipango ya baadaye iliyopo ni
kuendelea kuhamasisha jamii kutambua
ugonjwa huo na kuwahi vituo vya tiba,
kuendelea kutoa mafunzo kwa wataalamu
juu ya uchunguzi na utoaji wa tiba yake,
kuendelea kufuatilia mwenendo wa
ugonjwa kwa wanyama na binadamu.

0 comments:

Post a Comment