Wednesday 30 April 2014

JINSI VYAKULA TULAVYO NA NDIVYO VINAVYO TUMALIZA.




LEO napenda kuchukua fursa hii kueleza kwa mapana na marefu suala la vyakula na namna ambavyo vimekuwa chanzo kikuu cha maradhi sugu yanayotukabili leo, ambayo mengi mwisho husababisha vifo.

Kuanzia wiki hii, taandika mfululizo wa makala kuonesha ni jinsi gani vyakula tunavyokula vimekuwa hatari kwa afya zetu. Naamini ukiungana nami kuanzia mwanzo hadi mwisho, utanielewa na bila shaka utachukua hatua za kubadili mtizamo wako kuhusu chakula.
Tukumbuke kwamba uzima wa mtu unategemea sana kinga aliyonayo mwilini, kinga ambayo hujengwa na ulaji wa vyakula vyenye virutubisho vya aina mbalimbali. Kwa namna ambavyo Mungu ametuumba, mwili unapaswa

kujilindi wenyewe dhidi ya maradhi ya kila aina. Ukiwa na kinga imara ya mwili siyo rahisi kuugua mara kwa mara.
Magonjwa yanayojitokeza haraka pale kinga ya mwili inapokuwa chini, ni pamoja na kuugua malaria mara kwa mara, kifua kikuu, kutokwa na majipu, kutokwa uvimbe wa ajabuajabu katika mwili, kupatwa na mkanda wa jeshi,

kupatwa na saratani na magonjwa mengine ya maambukizi.
Huo ni mfano wa kundi moja la magonjwa ya maambukizi, lakini hata
magonjwa mengine hatari kama shinikizo la damu, magonjwa ya moyo, magonjwa ya viungo, kisukari, macho, na mengine mengi, huwa ni matokeao ya ulaji wa vyakula visivyo sahihi au uachaji wa ulaji vyakula muhimu.
CHANZO CHA KUSHUKA KWA KINGA
Ili uwe na kinga imara ya mwili, ni lazima uwe unakula mlo kamili unaojumuisha matunda, mboga za majani, nafaka na vyakula vingine vya asili, kwa sababu kila unachokula kina faida yake mwilini. Lakini siyo tu kula chochote kinachoitwa ‘chakula’, bali ule kilichosahihi na kilichosahihi.
Katika maisha tunayoishi sasa, hasa mijini, idadi Kubwa ya watu hawali kabisa vyakula sahihi, badala yake wanakula vyakula ambavyo si tu ni hatari kwa afya zao, bali pia hudhoofisha kinga ya asili ya mwili na hivyo

kuufanya mwili kubaki dhaifu na unaoweza kupatwa na ugonjwa wowote.
Chanzo kikuu cha kushuka kwa kinga ya mwili kunasababishwa na ulaji wa vyakula visivyo sahihi ambavyo ndivyo vinavyopatikana kwa wingi kila
mahali, hasa sehemu za mijini. Vyakula visivyofaa ndivyo vinavyotangazwa na kunadiwa kwenye vyombo vya habari kuwa bora.

VYAKULA HATARI VINAVYOLIWA KILA SIKU
Kuna orodha ndefu sana ya vyakula hatari ambayo huliwa kila siku, kuanzia asubuhi hadi jioni. Vyakula hivi yumkini huliwa kwa takriban maisha yote ya mtu na huonekana ni vya kawaida. Baadhi ya vyakula hivyo ni kama vile unga wa ugali, mkate, chips na juisi.

UNGA WA UGALI
Unga wa ugali unaotumiwa na watu wengi nchini ni sembe nyeupe. Chakula kikuu katika kaya nyingi zinazotumia ugali kama mlo wa kila siku huwa ugali mweupe uliotokana na mahindi yaliyokobolewa na kusafishwa,

kisha kusagwa na kutoa unga safi mweupe. Kwa mtizamo wa macho na ladha ya mdomoni, wengi wanaamini kuwa ugali wa aina hii ndiyo mzuri na unaotakiwa kuliwa.
Ulaji wa ugali wa aina hii hauna faida yoyote mwilini, kwani hauna virutubisho, kwa sababu vilishaondolewa vyote wakati wa kukoboa. Virutubisho muhimu vya muhindi viko kwenye kiini chake, hivyo
unapokiondoa unakuwa umeondoa lishe muhimu. Ndiyo maana hata panya hawali mahindi yaliyokobolewa

KATIKA makala zetu zilizopita, tulishaelezea madhara ya kula ugali uliotokana na mahindi yaliyokobolewa, tuliona kwamba chakula hicho kinapoingia mwilini hugeuka na kuwa sukari ambayo baadaye huweza

kusababisha ugonjwa wa kisukari. Mgonjwa wa kisukari hukatazwa kula ugali wa aina hii na badala yake hutakiwa kula ugali wa dona, mtama au ulezi.
Kwa faida ya afya zetu na kwa ajili ya kuimarisha kinga ya miili yetu, sote tunatakiwa kula ugali wa dona, mtama au ulezi kabla hata ya kuugua.

Vyakula hivi ni muhimu sana na siyo vya kimasikini kama ambavyo watu wengi wanadhani. Kwa bahati mbaya, upatikanaji wa unga wa dona umekuwa mgumu na ghali kuliko sembe nyeupe, hivyo kuwafanya watu wengi kukimbilia sembe nyeupe ambayo inapatikana kirahisi kila kona ya nchi na kwa bei nafuu.

Kwangu mimi naliona tatizo hili ni la kitaifa na kisera. Serikali kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, ilipaswa kutoa elimu ya kutosha ya kuelezea
madhara yatokanayo na ulaji wa sembe nyeupe kisha kuweka sera itakayokataza uzalishaji wa kibiashara wa sembe nyeupe kama ilivyo sasa. Sera ya namna hii ingeokoa maisha na afya za Watanzania wengi wanaoteketea kila situ kutokana na ugonjwa wa kisukari.

Naamini kaya nyingi nchini hazijui kabisa kama ugali utokanao na sembe nyeupe wanaokula kila siku iendayo kwa Mungu, una madhara kiafya. Ni vigumu kuzieleza na zikakuelewa familia ambazo kwa maisha yao yote
zimekuwa zikiamini kwamba kula ugali mweupe ndiyo kitu bora.
Serikali ilipaswa kuliangalia suala hili na kuona kama janga la kitaifa, ilipaswa kuanzisha kampeni maalum ya kutoa elimu kuhusu vyakula na lishe kwa njia mbalimbali, zikiwemo za matangazo redioni na kwenye televisheni.

ULAJI WA MATUNDA NA MBOGA
Hakuna kitu muhimu kwa mwili wa binadamu kama kujenga kinga ya mwili. Mwili unapokuwa na kinga imara, si rahisi kuugua magonjwa ya ajaba. Miongoni mwa kazi nyingi za matunda na mboga za majani, ni pamoja na hiyo kazi ya kujenga mwili na kuujengea uwezo wa kujikinga wenyewe.
Pamoja na umuhimu huo, ni watu wachache sana hula matunda na kuyachukulia kama sehemu ya milo yao ya kila siku. Watu wengi hula matunda au mboga za majani ‘kwa bahati mbaya’, huona siyo chakula muhimu sana. Hili ni kosa kubwa miongoni
mwa makosa mengi yanayofanywa na watu katika masuala ya afya.
Matunda yanatakiwa kuliwa kila siku na kwa wingi, vivyohivyo mboga za majani. Unapoacha kula matunda na mboga za majani za aina mbalimbali, jua unaukosesha mwili wako kinga dhidi ya maradhi yanayoweza kujitokeza mwilini.

VYAKULA HIVI NDIYO VINAVYOTUMALIZA
Vyakula tunavyotakiwa kuvila, hatuvili tena na pengine upatikanaji wake ni wa shida, hivyo tunalazimika kula vilivyopo licha ya kuwa vina madhara kwa afya zetu. Hali hii imeongeza idadi ya wagonjwa na magonjwa sugu.
Chakula kikuu cha mijini ni chips, kuku, mayai, soda, juisi za makopo au paketi, nyama choma na pombe. Pia kuna mkate mweupe, maandazi na chapati. Vyakula hivi huliwa kila siku, lakini ukivichambua utagundua havina faida yoyote mwilini zaidi ya kuingia na kutengeneza maradhi.

0 comments:

Post a Comment