Wednesday 26 November 2014

MAMBO YANAYOHARIBU AFYA YAKO-2

Hali ya miili ya wanawake
hutofautiana na wanaume na hata
kazi na shughuli wanazozifanya
pia huweza kuathiri afya zao kwa
ujumla. Kwa mfano, kubeba
mimba na kujifungua, kansa ya
ovari na kizazi huathiri afya ya
wanawake katika hali ambayo
wanaume hupatwa na kansa ya
tezi kibofu na ya korodani.
Wakati wa vita wanaume hushiriki
kwa wingi kuliko wanawake na
matokeo yake ni kuuawa au
kujeruhiwa. Wanawake na
wasichana huenda wakawa
wahanga wa vitendo vya utumiaji
mabavu dhidi yao na ukatili kuliko
watoto wa kiume na wanaume.
Katika baadhi ya jamii watoto wa
kike na wanawake huwa
hawapewi fursa ya kupata elimu
na kujiendeleza kama wanaume,
suala ambalo huathiri afya zao pia.
Tafiti nyingi zimeonyesha ubaguzi
wa kijinsia katika utoaji huduma
za afya hata katika nchi
zilizoendelea.

Miongoni mwa mambo muhimu
yanayoijenga afya ya mwanadamu
ni kula lishe salama na mlo
uliokamilika. Tunaposema lishe
salama na mlo uliokamilika au
healthy balanced diet kwa
kimombo, tunamaanisha masuala
muhimu mawili.

Moja ni kula kiwango
kinachotakiwa cha chakula kwa
mujibu wa harakati na hitajio la
mwili wako, na pili ni kula aina
tofauti za vyakula vinavyotakiwa
ili kuijenga siha ya mwili.
Tunapaswa kufahamu kwamba,
kula lishe bora ni suala muhimu
linalochangia kuimarisha afya ya
mwili. Lishe salama na iliyokami
inamaanisha kula vyakula tofauti
kutoka katika mafungu manne
makuu ya vyakula na kupunguza
baadhi ya vyakula katika milo
tunayokula kila siku.

Aina ya vyakula vinavyopaswa
kuwepo kwenye milo yetu ni
pamoja na matunda na mboga
kwa wingi. Kiwango cha kutosha
cha wanga kama vile mkate, wali,
viazi, pasta na vinginevyo na ni
bora viwe vinatokana na aina
mbalimbali za nafaka kamili
zisiokobolewa.

Maziwa na vyakula vinavyotokana
na maziwa kama mtindi na jibini.
Vyakula vyenye protini kama
vyama, samaki, mayai, maharagwe
na vinginevyo na vilevile kiasi
kidogo cha sukari , mafuta na
chumvi.

Ufuatao ni ushauri au vidokezo
muhimu (tips) kuhusiana na
namna ya kula vyema ili kuzilinda
na kuziimarisha afya zetu.
Tunashauriwa mlo tunaokula uwe
na kiasi cha kutosha cha wanga,
kwani aina hiyo ya chakula huipa
miili yetu nguvu.

Tunashauriwa kula matunda na
mboga kwa wingi kila siku.
Baadhi wanasema, ni bora kula
aina 5 za matunda tofauti na
mboga kwa siku.

Pia tunashauriwa kula samaki kwa
wingi kwa uchache mara mbili kila
wiki na kama hatutoweza kufanya
hivyo au kwa wale ambao samaki
wanawadhuru na wale wasiokula
nyama, wanapaswa kula
virutubishi muhimu
vinavyotupatia mada
zinazopatikana kwenye samaki
kwa ajili ya afya ya miili yetu.
Tunashauriwa kupunguza kwa
kiasi kikubwa sukari na mafuta
katika milo yetu.

Vilevile tunashauriwa kula chumvi
kwa kiwango kidogo, isizidi gramu
6 kwa siku kwa watu wazima.
Tunapaswa kufahamu kuwa,
baadhi ya vyakula tayari vina
kiwango cha chumvi ndani yake
kwani karibu theluthi moja ya
chumvi katika milo yetu hutoka
katika vyakula ambavyo tayari
vimeshatengeneza kama supu iliyo
tayari, sosi, mikate, asusa (snacks),
pai, pizza vyakula vinavyosindikwa
na kuhifadhiwa. Hivyo kuna
umuhimu wa kula vyakula hivyo
kwa kiasi kidogo.

Hii ni kwa sababu ongezeko la
chumvi mwilini huweza kumfanya
mtu apatwe na shinikizo la damu,
hali ambayo huweza kusababisha
ugonjwa wa moyo na kiharusi.
Suala jingine tunalopaswa
kuzingatia ni kunywa maji ya
kutosha, tunashauriwa kila siku
kunywa kiasi cha gilasi 6 hadi 8 za
maji au vyakula vingine vya
majimaji kama juisi na kadhalika,
ili kuzuia upungufu wa maji
mwilini.

Maji yana faida nyingi na baadhi
yake ni kuusaidia mwili kuondoa
kwa urahisi sumu na mabaki
yasiyotakiwa mwilini.
Kusaidia kulainisha macho na
maungio ya mwili na pia
hutusaidia wakati wa kumeza.
Jambo jingine tunaloshauriwa ni
kuupa mwili harakati, mazoezi ya
mara kwa mara na kuwa na uzito
unaotakiwa kiafya.
Jengine ni kutoacha kula kifuangua
kinywa.

Tunatakiwa kustaftahi kila siku
kwa sababu chakula hicho cha
asubuhi huupa mwili nguvu ya
kuanzia siku na huamsha utendaji
kazi wa mwili kwa ajili ya siku
nzima.

0 comments:

Post a Comment