Saturday 27 September 2014

TIBA YA SARATANI YA MATITI - 6



Tumekuwa tukielezea ugonjwa wa saratani ya matiti kwa wiki tatu na hii ni sehemu ya mwisho nikiamini kuwa sasa wengi wameuelewa. Wiki iliyopita tulielezea tiba kwa kemikali na leo tunaendelea na tiba kwa njia ya homoni.
HOMONI
Tiba ya homoni ya ugonjwa wa saratani ni matibabu ambayo huondoa homoni au kuzuia utendaji wake na kuzuia seli za kansa zisiendelee kukua. Homoni hutengenezwa na tezi mwilini na huzunguka katika mkondo wa damu.
Baadhi ya homoni huweza kusababisha kukua baadhi ya kansa. Iwapo vipimo vitaonesha kuwa seli za saratani zina sehemu ambazo homoni zinaweza kujishikiza au Receptors, hapo ndipo matabibu hutumia dawa, kufanya upasuaji au tiba ya mionzi ili kupunguza uzalishaji wa homoni husika au kuzuia utendaji wake.
Homoni ya Estrogen inayotengenezwa na ovari huweza kushadidisha saratani ya matiti na katika hali hii, matibabu ya upasuaji ufanyika ili kuzuia utengenezaji wa homoni hiyo katika ovari.
Kama nilivyosema huko nyuma, seli za kansa kwa kawaida husambaa katika sehemu nyingine za mwili ambako huko nako huanza kukua na kuunda uvimbe au Tumor mpya na baada ya muda kupitia Tumor hizo huchukua nafasi ya tishu mpya.
Kitendo cha kansa kusambaa mwilini kupitia mkondo wa damu na limfu huitwa Metastasis.  Japokuwa kumekuwepo na maendeleo katika matibabu ya kansa ya matiti ambapo matibabu yamekuwa yakifanyika kwa kutegemea umri, historia ya kansa katika familia na aina ya kansa.
Itaendelea 

0 comments:

Post a Comment