UTAFITI : INZI WA KIJANI TIBA YA VIDONDA SUGU!
|
Inzi Wa Kijani. |
INZI wa kijani anayefahamika kwa jina la kitalaamu kama Lucilia Sericata (green bottle fly) ni kati ya wadudu wanaoogopwa na binadamu kwa sababu ni chanzo cha ugonjwa wa kipindupindu na magonjwa mengine ya kuhara.
Kuogopwa
huko kunatokana na ukweli kuwa nzi hao tofauti na wadudu wengine hupenda
kuishi katika mazingira machafu kama vyooni, kwenye mizoga ya wanyama
na mashimo ya taka.
Hofu ya
binadamu kuhusu mdudu huyo unaweza kuitambua anapopita karibu na meza ya
watu wanapokula nyumbani au hotelini. Baadhi wanaweza hata kukosa hamu
ya kuendelea kula.
Lakini
mtazamo kuhusu mdudu huyo ni tofauti kwa wanasayansi wa Taasisi ya
Utaifi wa Kilimo (KARI) ya nchini Kenya, hasa baada ya kuanza kuwatumia
funza wanaotokana na nzi hao katika utafiti wa tiba ya vidonda sugu,
visivyopona kwa dawa ya antibiotic.
Utafiti huo
unaendelea katika Hospitali ya Kenyatta na kwa mujibu wa Dk. Phoebe
Mukiria ambaye anasimamia utafiti huo, mwenendo wa utafiti wa tiba hiyo
umefikia hatua nzuri.
Dk. Mukiria
anaeleza kuwa kimsingi tiba hiyo ya kutumia funza wanatokana na nzi wa
kijani si ngeni na ilikwishawahi kutumika katika nchi zilizoendelea kama
Marekani na nchi za Ulaya katika miaka ya zamani.
Hatua ya kwanza
Kwa mujibu
wa mwanasayansi huyo hatua ya kwanza katika tiba hiyo ni ile ya kuweka
nyama iliyooza au chakula katika sehemu ya wazi ili kuwavutia nzi wa
kijani katika eneo hilo.
“Kutokana na
harufu mbaya ya nyama, nzi wa kijani huanza kujaa eneo hilo nasi
tunawatega kwa kutumia wavu maalumu na baada ya hapo tunawahifadhi
katika chombo chenye wavu (cages),” anaeleza.
Baada ya
hatua hiyo nzi hao huanza kutaga mayai ambayo baada ya siku tano hugeuka
kuwa funza kabla ya kuanza hatua ya kufikia au kuzaliwa nzi mwingine.
“Baada ya
hatua hiyo ndipo tunawachukua funza hao na kuwaosha vizuri kwa maji ya
uvuguvugu kisha tunaweka katika vyombo maalumu (container) na kisha
tunawasafirisha hadi Hospitali ya Kenyatta kwa ajili ya tiba kwa
wagonjwa,” anasema mtaalamu huyo.
Anaeleza
zaidi kuwa katika hospitali hiyo madaktari wanaotibu wagonjwa wenye
vidonda vikubwa ambavyo ni sugu, huwatumia funza hao kwa kuwafunga
katika sehemu yenye kidonda katika mwili wa mgonjwa, kwa kutumia bandeji
yenye matundu ya kuingiza hewa.
“Kwa kawaida
funza hujilisha katika tishu za mwili zilizokufa (dead tissue) na hatua
hiyo hufanya kidonda kuwa kisafi na tishu zilizohai kuanza kupona”
“Pia funza wana
midomo kama sindano ambayo husaidia kufyonza uchafu ulioko katika
kidonda hasa usaha na madaktari huwabadilisha funza kila baada ya siku
mbili au tatu katika kidonda,” anasema daktari huyo.
Lakini anawatoa
hofu wagonjwa na watu wanaotilia shaka tiba hiyo akisema; “Si rahisi
funza wazaliane katika kidonda kwa sababu kwa kawaida funza hujilisha
kwenye tishu za mwili zilizokufa na uchafu unaozalishwa katika kidonda
na si vinginevyo.
Dk. Mukiri
anasema, pamoja na watalaamu wenzake, wanashukuru tiba hiyo kuwa suluhu
ya vidonda sugu na tayari mafaniko yake yameleta matunda kwa baadhi ya
wagonjwa ambao wamepona vidonda vyao.
“Bado
utafiti zaidi unaendelea lakini niseme tu kwamba tayari baadhi ya
wagonjwa waliotibiwa kwa njia hiyo wamepona vidonda vyao na wengine
wameonyesha maendeleo makubwa,”anasema Dk. Mukiri.
Changamoto za tiba hiyo
Kwa mujibu
wa mwanasayansi huyo changamoto kubwa ya tiba hiyo ni ile ya wagonjwa na
ndugu zao kukataa aina hiyo ya tiba ambayo wengine wanaona kuwa ni ya
“aibu”.
“Wagonjwa
wengine na ndugu zao wanaowauguza wamekuwa wakikataa aina hii ya tiba,
wakidhani kuwekewa funza katika kidonda ni tiba ya aibu hivyo kuwapa
madaktari wakati mgumu katika kuwashawishi,” anaeleza Dk. Mukiri.
Anasema kwa
kawaida madaktari hawana mamlaka yoyote katika tiba hii kwa kuwa bado
iko katika majaribio, hivyo wanalazimika kwanza kupata ridhaa ya mgonjwa
mwenyewe na ndugu zake kabla ya kufanyiwa matibabu hayo.
Dk. Kimani
Wanjeri wa Hospitali ya Kenyatta ni miongoni mwa jopo la watalaamu wa
tiba wanaosimamia majaribio hayo ambaye anaeleza kuwa njia hiyo ya tiba
inaweza kuwa mkombozi kwa wagonjwa wenye vidonda sugu ambavyo haviponi
kwa kutumia dawa zaantibiotics.
“Tiba hii
pia haina maumivu kwa wagonjwa na ni rahisi zaidi kwa upande wa gharama
kwa wagonjwa na ndugu zao, hupunguza muda wa wagonjwa kukaa hospitalini,
”anaeleza.
Daktari huyo
anasema mzunguko wa funza katika kidonda hufanya damu katika eneo lenye
jeraha kuwa rahisi zaidi na kurahisisha hatua ya kuelekea kupona kwa
kidonda.
Anaeleza
zaidi kuwa baada ya tiba hiyo kuna vidonda vina pona kabisa na vingine
huendelea kutibiwa zaidi ikiwa pamoja na kufanyiwa upasuaji mdogo
(grafting).
Nchi nyingine ambazo zinatajwa kuwa tiba hiyo imekuwa ikitumika ni pamoja na Marekani na Afrika ya Kusini.
0 comments:
Post a Comment