Thursday 1 May 2014

MAZOEZI KWA MTU MWENYE UGONJWA WA KISUKARI



MAKALA  HII  NI  MAALUMU  KWA  WANAO  SUMBULIWA  NA   TATIZO  LA  KISUKARI.

Kwa vyovyote vile utakuwa umewahi kuusikia au hata kupata uzoefu kuhusu ugonjwa wa kisukari. Eidha
kwa kuwa na ndugu, rafiki wa karibu au wewe mwenyewe kuwa mwathirika wa tatizo hili. Tatizo la
kisukari linaongezeka siku hadi siku, hususani kutokana na kuongezeka kwa tatizo la unene. Sababu
kubwa si ngumu kuifahamu, ni ulaji wa chakula unaozidi mahitaji ya miili yetu. Kwa lugha rahisi
tunaweza kusema, kula chakula bila kufanya mazoezi.
Ziko aina kuu mbili za ugonjwa wa kisukari. Ule unaotokea kwa sababu ya upungufu wa homoni ya
insulin mwilini 

( Type 1 diabetes),
 na ule unaotokana na homoni ya insulin kutokufanya kazi, japo kuwa
inatengenezwa kwa kiwango hata zaidi ya kawaida,

 (Type 2 diabetes). Asilimia 90 ya wagonjwa wa
kisukari wana kisukari cha aina ya pili(type 2 diabetes). Hivyo basi maelezo mengi yatakayoandikwa hapa
yatahusiana na kisukari cha aina ya pili.
 
Kisukari aina ya pili(Type 2 diabetes) ni nini haswa?
Ugonjwa huu huathiri uwezo wa mwili kutumia sukari, protini, mafuta na wanga. Miili yetu inahitaji
vichocheo mbali mbali ili kutengeneza nguvu na chembe hai na kutufanya tuendelee kuishi. Ugonjwa wa
kisukari huaribu uwezo wa mwili kufanya kazi wakati wa kawaida na hata wakati wa mazoezi.
Katika hali ya kawaida miili yetu hubadilisha sukari na wanga na kuwa glukozi au sukari kwa lugha ya
kawaida, ambayo hutumika mwilini kutengeneza nguvu zinazotuwezesha kuishi na kufanya shughuli za
kila siku. Glukozi husafirishwa katika damu na kupelekwa katika misuli, sehemu ambako kiasi kikubwa

cha glukozi hutumika kutengeneza nguvu na joto. Insulin, homoni itengenezwayo na kongosho,
inahitajika kuwezesha glukozi kuchukuliwa na misuli. Kwa maana hiyo basi, ili glukozi iweze kutumika
kutengeneza nguvu na joto, homoni inayoitwa insulini inatakiwa kuwepo. Glukozi ikishaingia kwenye
misuli, inatumika kutengeneza nguvu na joto au kutunzwa kwa matumizi ya baadaye.
Katika aina hii ya kisukari, ukikumbuka hapo awali tuligusia kwamba, homoni ya insulin inatengenezwa

lakini kutokana na sababu fulani(ambazo tutakuja kuziongelea siku nyingine) inashindwa kufanya
kazi.(Kumbuka ktk kisukari cha aina ya kwanza, uwezo wa kongosho kutengeneza insulin unakuwa
mdogo, hivyo kuathiri kiwango cha insulin inayotengenezwa). Kitendo cha insulini kutokufanya kazi licha

ya kutengenezwa kwa kiwango cha kawaida na wakati mwingine kiwango cha juu, kinatokana na misuli
kuwa sugu kwa insulin.Tatizo la mwili kuwa sugu kwa insulin linajulikana kitaalamu kama insulin
resistance. Kinachotokea ni kushindikana kwa sukari kuingia katika misuli hivyo kubaki katika damu. Hii
husababisha sukari kuwa nyingi zaidi ya kawaida katika damu.
Sukari kuwa nyingi katika damu kwa muda mrefu, kunaweza kusababisha magonjwa ya moyo, kufeli kwa
figo , upofu na matatizo ya mishipa ya fahamu.

Tofauti na aina ya kwanza ya kisukari, ambacho husababishwa na matatizo yanayouwa chembehai
zinazotengeneza insulin kwenye kongosho, ugonjwa wa kisukari cha aina ya pili unauhusiano mkubwa na
mifumo ya maisha hususani lishe na mazoezi. Watu wenye uwezekano mkubwa wa kupata tatizo hili
wana historia ya ugonjwa huu katika familia zao, na pia mara nyingi wanakuwa na magonjwa ya shinikizo
la damu na moyo. Mara nyingi ugonjwa huu huwapata watu wenye maisha ya kibwanyenye, ambayo
huwafanya kula chakula kingi zaidi ya mazoezi. Wengi wao wanakuwa ni wanene na wenye mafuta
mengi mwilini.
Kinachotumika kuzuia ugonjwa huu wa kisukari aina pili, ndicho kinchotumika kuzuia usilete madhara
makubwa kama magonjwa ya moyo na figo. Na si kitu kingine bali mazoezi na lishe bora.

Mazoezi yanaweza saidia
Matokeo ya tafiti chungu nzima yameyapa mazoezi kipau mbele katika kuzuia, na kutibu ugonjwa wa
kisukari aina pili, kwa sababu mazoezi yanauwezo wa kupunguza usugu wa insulin unaosababisha
homoni hii isifanye kazi. Kufuatia mazoezi ya mara kwa mara, chembe hai za mwili zinaweza kutumia
insulin kuchukua sukari kutoka kwenye damu, kuitumia na hivyo kuipunguza.
Mazoezi pia yanaweza kupunguza uwezekano wa kupata magonjwa ya moyo kwa kupunguza kiasi cha
mafuta mwilini na shinikizo la damu. Kwa kila kilo tano mtu mwenye kisukari anazopoteza, anapunguza
usugu wa insulin kwa asilimia ishirini.
 
Ushauri wa mazoezi
Kama unakisukari aina ya pili, unashauriwa kufanya mazoezi yafuatayo
 
1. Mazoezi yanayoufanyisha kazi mfumo wa damu na moyo(cardiovascular exercise):
Weka lengo la kufanya mazoezi ya wastani, kama vile kutembea, na mazoezi mengine
yasiyotumia nguvu nyingi kama vile kuendesha baiskeli na kuogelea, angalau mara tatu mpaka
nne kwa wiki. Kumbuka, kufanya mazoezi ya namna hii kila siku kunaleta matokeo mazuri zaidi.
 
2. Mazoezi ya kunyanyua au kusukuma vitu vizito(Resistance exercise):
Watu wengi hukosa kufanya mazoezi haya, kwa kudhani kwamba ni kwa ajili ya wabeba vyuma
na wapiganaji tu. Mazoezi haya ni muhimu sana, na siku zijazo nitaelezea kwa undani umuhimu
wa mazoezi haya. Weka lengo la kufanya mazoezi ya kunyanyua au kusukuma vitu vyenye uzito
wa wastani angalau mara mbili kwa wiki. Akikisha unafanyisha kazi misuli yote muhimu ya mwili
wako. Fanya walau marudio kumi mpaka kumi na tano kwa kila aina ya msuli.
 
3. Mazoezi ya kulainisha viungo(flexibility exercises):
Angalau mara mbili au tatu kwa wiki fanya mazoezi ya kunyoosha viungo muhimu vya mwili ili
kulainisha viungo na misuli. Fanya kwa angalau dakika kumi na tano mpaka thelathini, mara
mbili mpaka nne kwa kipindi.
Undani zaidi kuhusu mazoezi haya, utaelezewa katika makala zifuatazo. Makala hii inagusia aina
ya mazoezi tunayotakiwa kufanya ili kupunguza uzio na sukari mwilini.
Niandikie kwa maoni na maswali,

0 comments:

Post a Comment